MOMBASA, KENYA
SERIKALI ya Kenya imetangaza hatua za usalama katika eneo la pwani kabla ya Uchaguzi Mkuu kesho kutokana na vitisho vinavyotokana na kundi la Al-Shabaab.
Mratibu wa kikanda, Nelson Marwa, amesema wameimarisha usalama kuhakikisha upigaji kura hauingiliwi na makundi ya kigaidi ya ndani au kigeni.
Alibainisha kwamba tayari wameshapeleka maofisa wa usalama wa kutosha ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Kenya imepata habari kuwa makundi kadhaa ikiwa ni pamoja na Al-Shabaab wanapanga kufanya mashambulizi wakati wa uchaguzi.
Miongoni mwa maeneo, ambayo usalama umeimarishwa ni kaunti za Lamu na Tana River, ili kuhakikishia wakazi wa maeneo hayo wanapiga kura kwa amani.
Al-shabaab imetishia kufanya mashambulizi kadhaa ili kusababisha hofu kwa Wakenya na kuwazuia kushiriki katika uchaguzi huo hasa katika miji iliyoko mipakani mwa Kenya na Somalia .