Kenya mabingwa Chalenji wanawake

0
1107
Mchezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake Kilimanjaro Queens, Fatma Issa (kulia) akimtoka mchezaji wa timu ya Kenya, Corazone Aquino wakati wa mechi ya fainali ya CECAFA Challenji iliyochezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam jana.Kenya ilishinda 2-0.

*Yaichapa Kilimanjaro Queens 2-0, Uganda washindi watatu

GLORY MLAY NA TIMA SIKILO

TIMU ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens’, imevuliwa ubingwa wa michuano ya Chalenji Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), baada ya kufungwa na Kenya mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Kilimanjaro Queens walikuwa mabingwa kwa misimu miwili mfululuzo, lakini wameshindwa kutetea taji lao baada ya kupata kichapo hicho.

Mabao ya Kenya katika mchezo huo wa jana ulioanza kwa kasi, yalifungwa na Jentrix Shikangwa.

Kilinjaro Queens walikuwa wa kwanza kufanya shambulizi dakika ya nane, baada ya Anastazia Katunzi kupiga shuti na kipa wa Kenya, Kundu Annedy kudaka.

Baadaye, Kilimanjaro walifanya shambulizi lingine dakika ya 16 na kupata faulo, lakini Julieth Singano alishindwa kufunga.

Dakika ya 22, Mwanarima Jereko wa Kenya alishindwa kufunga mpira wa faulo baada ya shuti lake kutoka nje.

Kenya alimanusura wapate bao dakika ya 29, baada ya Mercy Airo kupiga shuti, lakini kipa wa Kilimanjaro Queens, Najat Idrisa aliwahi na kuondoa hatari hiyo.

Mshambuliaji wa Kilimanajro Queens, Asha Rashid ‘Mwalala’, alishindwa kufunga dakika ya 45 baada ya shuti lake kutoka nje.

Timu hizo zilikwenda mapumziko kila moja ikiwa haijaona lango mwa mwenzake.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Kenya kwa kumtoa Janeti Bundi na kuingia Jentrix Shikangwa, yalileta makunda kwa timu hiyo.

Jentrix ndiye aliyefunga bao la kwanza dakia ya 70 kwa mkwaju wa penalti baada ya mchezaji wa Kilimanjaro Queens kufanya madhambi eneo la hatari.

Badaye Jentrix alifunga bao la pili dakika ya 85 kwa shuti kali kutoka nje ya 18 na kuiwezesha timu yake kuondoka na ushindi huo.

Kilimanajro Queens: Najat Idrisa, Happiness Mwaipaja, Amina Bilali, Donisia Minja, Mwanahamisi Omari, Anastas Katunzi/Stumai Abdallah, Julitha Tamuwai, Fatuma Salum na Asha Rashid

Kenya: Annedy Kundu, Mwanalima Jereko, Nelly Sawe, Janet Bundi/Jentrix Shikangwa, Mercy Airo, Dorcus Nixon, Sheril Andiba, Ruth Ingosi, Cynthia Musungu, Vivian Makokha na Corazone Aquino.

Mshindi wa tatu katika michuano hiyo ni Unganda baada kuifunga Burundi mabao 2-0.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here