Nairobi, Kenya
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ametangaza siku 7 za maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, kilichotokea jana Machi 17, 2021, na bendera ya nchi hiyo pamoja na ile ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zitapepea nusu mlingoti.
Rais Kenyatta ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ametangaza siku hizo za maombolezo kitaifa nchini humo kwa heshima ya Rais Magufuli, ambapo pia amemuomba Mungu aendelee kusaidia ili waweze kuendelea na msimamo aliokuwa nao Rais Magufuli wa kuunganisha watu wa Afrika Mashariki
“Kwa niaba ya serikali na watu wa Kenya natuma salamu za pole na rambirambi kwa mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, watoto na familia yote ya Magufuli na Watanzania, nakumbuka mara nyingi ambapo tumeweza kukutana na kuongea maendeleo ya nchi zetu, nimepoteza rafiki, mfanyakazi mwenzangu na mshirika wangu, Kenya tunasimama imara wakati huu mgumu na Watanzania,” amesema Rais Kenyatta