Sharifa Mmasi,Mtanzania Digital
KATIBU Mkuu wa Chama cha Waendesha Baiskeli Mkoa wa Lindi (CHABALI), Said Kengele, amemsihi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwatazama kwa jicho la tatu ili kuendelea kuinua vipaji vya vijana vinavyoendelea kupotea kila siku.
Akizungumza na Mtanzania Digital, Kengele amesema kuwa, miaka ya nyuma aliwahi kumgusia Waziri huyo suala hilo na mwelekeo ulikuwa mzuri lakini baada ya kugubikwa na majukumu mengi ya serikali amewapa kisogo.
Aidha, Kengele amesema kwa sasa upande wa mchezo wa baiskeli Lindi hawawezi kufanya mashindano yoyote kutokana na ukata unaowakabili lakini pia, vifaa kwao ni changamoto kwani bado wanaendelea kutumia baiskeli za zamani ambazo hazina viwango.
“Mkoa wa Lindi una viongozi wengi sana wa Serikali lakini bado kwenye baiskeli tumepewa kisogo, mimi namuomba sana Waziri Mkuu atusaidie kutuinua nikiamini kwamba yeye ni mzawa wa huku na hashindwi kutusaidia hata baiskeli maana tuna hali mbaya,” amesema Kengele.