26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

VYOO VYA KISASA VILIVYOIBADILI KEKO

Mojawapo ya choo kilichojengwa katika Mtaa wa Keko Machungwa kwa kutumia chupa za plastiki na udongo wa mfinyanzi.
Mojawapo ya choo kilichojengwa katika Mtaa wa Keko Machungwa kwa kutumia chupa za plastiki na udongo wa mfinyanzi.

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

TATIZO la ukuaji kasi wa miji mingi ya Afrika ukiwemo Dar es Salaam umechangia kukuza changamoto ya usafi wa mazingira hasa katika makazi holela.

Mji wa Dar es Salaam unakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya milioni tano ambao huzalisha taka tani 3,100 kwa siku lakini zinazozolewa ni 1,200 tu kwa siku.

Pia idadi kubwa ya wakazi wa jiji hilo wanatumia vyoo vya shimo ambavyo vingi haviko katika hali nzuri na hivyo kuchangia milipuko ya magonjwa.

Mtaa wa Keko Machungwa ulioko katika Kata ya Miburani, Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa maeneo ya makazi holela ambayo awali yalikuwa yakikabiliwa na kero kubwa ya usafi wa mazingira.

Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, mtaa huo una wakazi zaidi ya 14,000 huku kaya moja ikiwa na wastani wa watu watano hadi saba.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Keko Machungwa, Mashaka Hamad, anasema kaya nyingi zilikuwa hazina vyoo na hata zile chache zilizokuwa navyo havikuwa katika ubora unaotakiwa.

“Miaka ya nyuma kipindupindu kilikuwa kama kimeota mizizi Keko Machungwa kwa sababu watu walikuwa hawana vyoo na wengine unaweza kwenda akakuambia ana choo lakini ukikiangalia unakuta hana tofauti na yule ambaye hana,” anasema Hamad.

Anasema ujio wa Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala ya kijamii (CCI), katika mtaa huo umebadilisha taswira iliyokuwapo awali kutokana na kuwezesha wananchi katika suala la usafi wa mazingira hasa katika ujenzi wa vyoo bora na vya gharama nafuu.

Shirika hilo lilianzisha programu ya usafi wa mazingira mwaka 2006 katika mikoa mbalimbali nchini ukiwamo Dar es Salaam.

Shirika hilo linafanya kazi katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Arusha, Tanga na Zanzibar ambapo lina vikundi zaidi ya 20,000.

Mtaa wa Keko Machungwa ni miongoni mwa maeneo yaliyoingizwa katika programu hiyo baada ya kubainika kuwa na kero kubwa ya ukosefu wa maji na vyoo bora.

Mkurugenzi wa CCI, Dk. Timoth Ndezi, anasema walipata mkopo kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID) na miongoni mwa fedha hizo zilielekezwa katika jamii hasa katika miradi ya maji na usafi wa mazingira.

Wawakilishi wa DFID wiki iliyopita walitembelea katika mtaa huo kujionea utekelezaji wa shughuli za usafi wa mazingira na kuzungumza na jamii zilizonufaika na programu hiyo.

Shughuli za ujenzi wa vyoo pamoja na uchimbaji visima hufanywa na vikundi vya kijamii (Federation) ambavyo viko chini ya shirika hilo.

Kiongozi wa kitaifa wa vikundi hivyo, Husna Shechonge, anasema wana vikundi hukutana kisha hufanya tafiti katika mitaa husika na kuibua changamoto za kufanyiwa kazi.

Anasema katika Mtaa wa Keko Machungwa, vikundi hivyo vimefanikiwa kujenga vyoo 51 vya gharama nafuu na kusaidia kaya ambazo zilikuwa hazina vyoo bora.

“Kati ya vyoo hivyo 22 ni vya kumwaga maji na 29 ni vya ikolojia ambavyo vimejengwa kwa kutumia chupa za plastiki. Tunaishirikisha jamii kwa kutoa elimu kuhusu usafi binafsi, mazingira na kushiriki katika uzoaji taka za majumbani,” anasema Shechonge.

Kuhusu vyoo vilivyojengwa kwa kutumia chupa za plastiki, anasema baada ya chupa kuokotwa huwekwa mchanga ndani yake na kupangwa juu kwa kubebana kisha kusilibwa na udongo wa mfinyanzi na kamba.

Anasema vyoo hivyo huwa na chemba nne ambapo baada ya chemba mbili kujaa hufunikwa kisha mtumiaji huamia katika chemba zingine. Kinyesi kilichokuwa katika chemba za awali huvunwa na kutumika kama mbolea na kuacha chemba hiyo kuwa wazi kwa matumizi mengine.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maji katika kikundi cha Amka, Mwamvua Omary, anasema wameweza kuchimba kisima kimoja kinachosambaza maji katika vituo saba, Zahanati ya Keko Machungwa na kwa wanajamii 10.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles