24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

KCMC yahitaji Sh bilioni 5 miundombinu ya saratani

Na UPENDO MOSHA-MOSHI

HOSPITALI ya Rufaa ya Kikanda ya KCMC, inahitaji zaidi ya Sh bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mashine za mionzi zitakazotumika kutoa tiba kwa wagonjwa wa saratani.

Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Gliad Massenga, wakati akizungumza katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani iliyofanyika nje ya viwanja vya kitengo cha saratani katika Hospitali ya KCMC, mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.

Dk. Massenga alisema kwamba, fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa jengo maalumu la kuhifadhi mashine hizo za mionzi, hatua ambayo itasaidia wagonjwa wa saratani kupata tiba kamili hospitalini hapo.

“Pamoja na mahitaji hayo, hadi sasa Serikali imesema itatoa shilingi bilioni moja ambazo hazitoshi,” alisema Dk. Massenga.

Alisema kwamba, hospitali hiyo inatoa huduma za tiba ya saratani kupitia kitengo chake cha saratani na kwamba, kukamilika kwa jengo hilo kutawezesha kuwapo kwa huduma za wagonjwa wengi kwani mahitaji bado ni makubwa.

Mbali na hayo, alisema mwaka 2020 hospitali hiyo itaanza ujenzi wa wodi kwa ajili ya kulaza wagonjwa wa saratani yenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 60 kwa wakati mmoja na kwamba, hadi sasa zaidi ya Sh milioni 200 zimeshapatikana kwa ajili ya ujenzi huo.

Wakati huo huo, Dk. Massenga alisema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa saratani kwa kuwa takwimu zinaonyesha mwaka 2012 hadi mwaka 2018, hospitali hiyo ilipokea wagonjwa wa saratani 9,312 wakiwamo wapya 1,445.

Awali, Mkuu wa Kitengo cha Saratani wa hospitali hiyo, Furaha Severine, alisema asilimia 65 ya wagonjwa wa saratani wanatoka katika nchi zinazoendelea.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kina Mama, Bariki Mchome, alisema saratani inayoongoza kwa vifo kwa wanawake ni saratani ya shingo ya kizazi na husababishwa na mwanamke kuwa na wapenzi wengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles