Na Brighiter Masaki
KAMPUNI ya KC Land Development Plan imeingia mkataba wa ununuzi wa viwanja na wasanii wa filamu nchini wanaounda chama cha Uzalendo Kwanza.
Mkataba huo wa viwanja vilivyopo eneo la Mwasonga, Kigamboni jijini Dar Es Salaam, ulisainiwa na Mkurugenzi wa kampuni ya KC Halid Mwinyi pamoja Mwenyekiti wa Uzalendo Kwanza Steve Nyerere kwa niaba ya wasanii mbele ya mwanasheria wa kampuni hiyo pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni Rahel Mhando.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti Steve Nyerere amesema anaishukuru kampuni hiyo kwa kuwafikiria wasanii maskini katika kuwawezesha kwenye suala la kumiliki ardhi na kuwa na makazi yao.
“Ni kweli wasanii tumekuwa tukitangatanga katika nyumba za kupanga, tunawashukuru KC kwa kutuona na kutuwezesha kupata ardhi kwani mngeweza kuwauzia hata matajiri lakini mmetufikiria sisi wasanii tunashukuru na tuna waahidi kuwa hatutauza viwanja bali tutajenga, mtaa utakuwa ni wetu wasanii, tutauita Kijiji cha Wazalendoa,” alisisitiza Nyerere
Kwa Upande wake Halid Mwinyi ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya KC, amesema kuwa wamejipanga kuwakwamua wananchi wa chini hivyo wameanza na wasanii kwa kuwaonyesha maeneo yao ya viwanja na kuingia mkataba wa kupeana viwanja.
“Tumeanza na wasanii baada ya hapo tutafuata makundi mengine kwa mkopo usio kuwa na riba na viwanja ni kwa muda wa miaka miwili tu. Tumewaonyesha viwanja vya Kigamboni japo kuna maeneo tofauti tofauti mkoa wa Pwani pamoja na Dodoma kama mnavyoona tunaendelea kuweka barabara na hospitali na umeme wamepapenda na ndio maana wamekubali na tumesaini mkataba” amesema Mwinyi