22.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Kaya 391 zakosa makazi kwa mafuriko

mhagamaNa Elias Msuya, Dodoma

WATU 571 hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba 391 kuathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani hapa.

Akizungumza katika ziara ya kutathmini athari ya mvua hizo katika Kijiji cha Mpunguzi wilayani Dodoma jana, mkuu wa wilaya hiyo, Jasmine Tiseku, alisema nyumba zilizobomoka kabisa ni 164 na jitihada za kuwapa misaada zinaendelea.

“Vijiji vilivyoathirika ni Mpunguzi A na B, Mkulabi na Makumbulu. Mvua hii ilianza Januari mosi na kuleta maafa halafu ikarudia tena Januari 18 hadi sasa. Tunaomba wananchi waondoke kwenye maeneo hatarishi,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Akizungumza katika eneo hilo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Vijana, Jenister Mhagama, alisema Serikali imetenga msaada wa chakula tani 700 kwa ajili ya walioathirika na mafuriko katika mkoa huo.

“Tumepanga kuleta chakula cha kutosha kwa walioathirika na mafuriko. Tutaleta tani 700 na pia tutaleta chakula kingine kiuzwe masokoni kwa bei nafuu ili kusaidia kupunguza bei ya chakula wakati huu wa mvua,” alisema Mhagama.

Mbali na chakula, Waziri Mhagama alisema watagawa magodoro kwa familia zilizoathiriwa na mafuriko hayo.

Aliwataka wananchi kuchukua tahadhari na mvua hizo kwa kuhama kwenye maeneo hatarishi, hasa ya bondeni, huku akisema tayari Kamati ya Maafa ya Wilaya imeshaanza kufanya tathmini ya uharibifu uliojitokeza.

“Taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imesema mwaka huu kutakuwa na mvua za El-nino, kila mkoa umeathirika na hali hii, hivyo kila mwananchi ajihadhari kwa kuhama kwenye maeneo hatarishi,” alisema Mhagama.

Akizungumzia chanzo cha mafuriko hayo, Mhandishi wa Kampuni ya Technics Construction Group inayojenga daraja la Mto Mpunguzi, Thobias Kiwando, alisema maji yalikuwa mengi kiasi cha kushindwa kupita kwenye daraja la mto huo na kupasua tuta linaloyazuia kwenda kwenye makazi ya watu.

“Hapa kuna makutano ya mikondo mitatu, baada ya kuhamishwa kwa barabara hii maji yote yanakutana kwenye daraja hili, hivyo yakizidi ndiyo yanapaswa tuta kama hivi,” alisema Kiwando na kuongeza:

“Ujenzi huu utatumia siku 14 au chini ya hapo na utarudisha tuta kwenye hali yake na kuilinda barabara isiendelee kulika.”

Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Vijana ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini, Anton Mavunde na mbunge wa viti maalumu wa mkoa huo, Felister Bula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,205FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles