24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kauli za Museveni zazua sintofahamu

Kampala, Uganda

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, amekuwa mara kwa mara akizitaka mahakama zihakikishe wauaji wananyongwa ili kumaliza uhalifu nchini Uganda.

Museveni ambaye amekuwa akitoa kauli hiyo katika mikutano ya hadhara, hivi karibuni ameahidi kukabiliana na mahakama ili kuhakikisha wauaji wananyongwa.

Gazeti la The Monitor nchini humo lilieleza wiki mbili zilizopita kuwa kiongozi huyo alimwagiza Mkuu wa Polisi, Meja Jenerali Sabiti Muzeeyi kuandaa mpango wa kumaliza ongezeko la silaha na ghasia za uhalifu katika mji mkuu wa nchi hiyo Kampala zinazotekelezwa na watu wenye silaha.

“Nina vita na mahakama, sitavumilia watu wanaowaua watu wengine. Yeyote anayewaua watu wengine atauawa,” Museveni amenukuliwa na vyombo vya habari akisema alipokuwa akizungumza na vijana wanaoishi maeno ya mabanda (ghetto) mjini Kampala hivi karibuni.

Mwanasheria na mbunge nchini Uganda, Asuman Basalirwa, ameiambia BBC kuwa kunyongwa ni moja ya adhabu zinazotolewa na mahakama kwa mujibu wa sheria na katiba ya Uganda.

Hata hivyo, alisema uamuzi na mamlaka ya kumnyonga mtu au kutomnyonga hutolewa na jaji wa mahakama, na Rais Museveni hana mamlaka yoyote, wala ushawishi wowote wa kubadili uamuzi wa mahakama.

“Maneno ya Rais Museveni hayawezi kuilazimisha mahakama kubadili maamuzi yake wala kumpatia mtu fulani hukumu ya kunyongwa.

“Kile anachoweza kukifanya ni kutoa msamaha kwa mfungwa au wafungwa kwa misingi ya huruma, jambo analokubaliwa kikatiba,” alisema Basalirwa.

Katika magereza nchini Uganda kuna idadi kubwa ya wafungwa ambao tayari wamehukumiwa adhabu ya kifo, lakini adhabu ya kunyongwa haitekelezwi kutokana na kwamba wengi wanasita kutoa hukumu hiyo.

Visa vya uhalifu vimekuwa vikiripotiwa katika maeneo ya mitaa ya mabanda ya Najjanankumbi Ndeeba ambako kuna magenge kama vile lile linaloendesha wizi wa simu na bidhaa nyingine, linalofahamika kama Kifeesi.

Kundi hilo limekuwa likiripotiwa kuwagonga wapitanjia kwa vyuma na kuwaibia mali zao.

“Tutatumia sheria ya Musa; jicho kwa jicho na jino kwa jino. Mtu yeyote atakayewaua watu wengine atakufa pia,” alisema Museveni.

Wiki mbili zilizopita polisi waliandaa mpango utakaowezesha kuongeza juhudi zao zaidi katika kuwasaka watu wanaorudia makosa, kuimarisha mawasiliano na umma na kushughulikia matukio haraka pale yanapotokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles