ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM
VIONGOZI wa vyama vya upinzani wamesema wanaunga mkono kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru kutaka vyanzo vya fedha za Uchaguzi Mkuu kwa vyama vya siasa vichunguzwe, wakitaka awe tayari uchunguzi huo uanzie pia katika chama chake.
Wakizungumza na MTANZANIA jana kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani walisema hatua hiyo ni ya muhimu, hasa wka kuwa pamoja na kwamba CCM ina vyanzo kadhaa vya fedha, lakini inahitajika ifanyiwe uchunguzi pia kuhusu vyanzo vyake ambavyo havijawekwa hadharani.
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema hana tatizo na suala hilo la uchunguzi, lakini lihusishe pia uchunguzi wa CCM na vyanzo vyake.
Alisema suala hilo lihusishe uchunguzi na ukaguzi maalumu wa vyanzo vya fedha kwa CCM katika chaguzi zilizopita na baada ya hapo wakae mezani na kufanya tathmini.
“Dk. Bashiru akubali kwanza uchunguzi na ukaguzi maalumu wa wakaguzi huru kwa matumizi ya CCM katika uchaguzi wa 2005, 2010 na 2015 kisha tuanze kujadilianamambo mengine,” alisema Zitto.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CUF,Abdul Kambaya alisema hiyo ni hoja nzuri sana na wanaiunga mkono kweli kweli, ila wanataka uchunguzi huo ufanyike kwa kina na uhusishe wachunguzi ambao utavihusu vyama vyote.
Alisema katika hilo, CCM haiwezi kukwepa uchunguzi huo, nao lazima wachunguzwe na matokeo ya uchunguzi yawekwe hadharani, siyo atoe ushauri huo kwa ajili ya kuwachunguza wapinzani tu.
“Nina uhakika, katika uchunguzi huo CCM hawatakuwa salama kwa sababu wana vyanzo vingi vya kificho, ukiangalia wana matumizi makubwa sana ambayo hayaendani na mapato halisi ya chama, kwa maana ya ruzuku, ada na miradi.
“Ni kweli kwamba kuna vyama vya siasa vinapata fedha kutoka nje na CCM pia wanapokea fedha hizo na hatujui hesabu zake, wala hatujui makubaliano yao,” alisema.
Alisisitiza kuwa hapo ndiyo kuna tatizo kwa sababu hatujui hao watu wanaowapa fedha wanawaahidi nini na mara nyingi huwa kuna makubaliano ya kulipa fadhila na hapo ndipo unapokuta wanalazimika kuingia mikataba ya hovyo ya madini na rasiolimali zetu zinaondoka tu.
Kambaya alisema kw aupande wa chama chake, hawana mashaka kabisa na uchunguzi wa namna hiyo, wako tayari wakati wowote kwa kuwa wana uhakika na vyanzo vyao.
Kwa upnde wake, Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chauma), Hashim Rungwe alisema hayo ni maoni yake lakini anakubaliana na uchunguzi iwapo utafanyika kwa kuwa vyama vingi vina vyanzo vya mapato ambavyo havina shaka.
Alisema kwa kauli hiyo akubali tu kwamba wao, CCM ndiyo wanaostahili kuanza kuchunguzwa kwa sababu wanaopata fedha nyingi za ruzuku ambapo alidai zinatoka serikalini na baadhi ya vyama vyenye wabunge, ambavyo pia vinapata ruzuku hiyo.
Rungwe alisema vyama vingi vimekuwa vikishiriki katikia chaguzi kwa kutumia rasilimali za viongozi na za baadhi ya wanachama wenye mapenzui mema ambao hutoa misaada na ni vyama vichache ambavyo hata hupokea fedha kutoka nje, ikiwemo CCM.
“Wao ndiyo wanaopata fedha kutoka Serikalini, ndio wanaopata fedha kutoka kwa marafiki wa nje. Mimi nafikiri wachunguze, kama anaona kwamba inafaa na uchunguzi uanzie kwao,” alisema.
Kauli ya Dk. Bashiru
Akiwa katika ziara yake ya kichama kwenye Mkoa wa Kusini, Zanzibara mwishoni, wakati akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali za CCM mkoani humo, Dk. Bashiru, aliishauri Serikali kuhakikisha inachunguza vyanzo vyote vya fedha za vyama vya siasa, zitakazotumika Uchaguzi Mkuu ujao kama zinatokana na vyanzo halali.
Alisema kuna vyama havina wanachama wala miradi ya kuwaingizia kipato, lakini wakati wa uchaguzi vinatumia fedha nyingi bila ya kujulikana vyanzo vya upatikanaji wa fedha hizo.
Dk. Bashiru alisema Serikali ihakikishe vyama vyote vya siasa ikiwamo CCM vinatumia vyanzo halali vya fedha za Uchaguzi Mkuu ujao ili kuepuka fedha kutoka vyanzo haramu.
Alisema CCM inajipanga kutekeleza kwa vitendo sheria ya gharama za uchaguzi kwa kuhakikisha inatumia fedha zake za ndani zilizotokana na vyanzo vyake halali.
Dk. Bashiru alisema kuna baadhi ya vyama vya siasa vimekuwa na tabia zisizofaa za kupita kila kona wakiomba fedha za uchaguzi kutoka vyanzo haramu kwa lengo la kushindana na CCM.
“Chama Cha Mapinduzi kina wanachama wengi wanaolipa ada, tuna uwezo wa kuendesha uchaguzi bila kutegemea fedha za misaada.
“Lazima na vyama vya upinzani viweke wazi vyanzo vyao vya mapato kama tunavyofanya sisi, bila kufanya hivyo tutakuwa na mashaka na upatikanaji wa fedha zao katika uchaguzi,” alisema Dk. Bashiru.
Alizielekeza kamati za siasa za mikoa yote ya CCM Tanzania, kuanza maandalizi ya kukusanya fedha za uchaguzi kutoka vyanzo vinavyotambulika katika mikoa hiyo.
Aliwaambia viongozi hao wa mikoa kuwa Uchaguzi Mkuu ujao CCM makao makuu haitatoa fedha za uchaguzi, hivyo kila mkoa utajigharamia, na makao makuu kazi yake itakuwa kuratibu uchaguzi ufanyike kwa ufanisi.
Alisema mwaka 2020 CCM kwa mara ya kwanza itafanya uchaguzi wa gharama nafuu kwani hata katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu, walitumia fedha zisizozidi Sh milioni 300 badala ya bilioni 8 zilizokuwa katika bajeti ya awali.
Alizitaka pia kamati za siasa za mikoa zinazoandaa mapendekezo ya uteuzi wa wagombea udiwani, kuwasilisha katika halmashauri za mikoa kwa uteuzi wa wagombea katika kura za maoni kuepuka hila na upendeleo.
Alisema hata kwa wabunge na wawakilishi, utaratibu wa kupatikana wagombea wa CCM watapita katika mchujo na kutathiminiwa kwa kina ili wapatikane wenye sifa na uwezo unaokubalika kikatiba na wanaokwenda na kasi ya sasa CCM mpya.
“Uchaguzi ujao ushindi wa kura za maoni hautokuwa kigezo cha kuwa kiongozi, lazima tujiridhishe kwa sifa za kila mgombea kwa kuangalia rekodi yake kiutendaji na uchapakazi wake ndani na nje ya chama,” alisema Dk. Bashiru.