KATIBU MKUU CHADEMA AKAMATWA NA POLISI

1
587
KATIBU Mkuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji
KATIBU Mkuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji

Na Waandishi Wetu – DAR/MIKOANI  

KATIBU Mkuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji na wabunge wawili wa chama hicho, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kuvamiwa katika kikao cha ndani kilichokuwa kikifanyika katika mji wa Mbamba Bay, Wilaya ya mkoani Ruvuma.

Taarifa iliyotolewa jana jioni na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Gemin Mushy, iliwataja waliokamatwa kuwa ni sita.

Iliwataja watu hao mbali na Dk. Mashinji kuwa ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini Masasi, Fecil David, Katibu Mwenezi Chadema, Charles Makunguru na Filbert Ngatunga ambaye ni Katibu wa chama hicho Kanda ya Kusini Masasi.

Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Sakuru na Sauda Manawa ambaye ni Katibu wa Ulinzi Chadema Taifa.

Taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi ilieleza sababu za kuwakamata viongozi hao kuwa ni katazo la Serikali la kuzuia maandamano, mikutano na mikusanyiko yeyote ya kisiasa inayohusisha watu wengine tofauti isipokuwa kwa viongozi wa eneo husika.

“Kwa taarifa za hivi punde, mbunge wa viti maalumi, Mh. Zubeda Sakuru aliomba kufanya maandamano na baadae akaibua maandamano ambayo yalikwishazuiliwa, yalihusisha misafara ya watu na pikipiki 11 zilizobeba abiria zaidi ya mmoja (mishkaki), watu ambao walileta fujo katika maeneo mbalimbali ya barabara ya Wilaya ya Nyasa,” inasomeka taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi.

Jeshi hilo lilisema linaendelea na kukamata waandamanaji wengine ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema mbunge mwingine aliyekamatwa pamoja na Dk. Mashinji ni Cecil Mwambe wa Ndanda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kusini.

“Wamepelekwa kituoni kuhojiwa ambapo Katibu Mkuu, Dk. Mashinji ametakiwa kueleza kwa nini yuko Mbamba Bay na aeleze amekwenda kufanya nini,” alisema Makene.

Alisema polisi waliwakamata viongozi hao wakiwa katika kikao cha ndani, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Katibu Mkuu huyo kukagua shughuli za Chadema katika majimbo ya kanda hiyo iliyoanza jana.

Wakati jeshi hilo mkoani Ruvuma likiwakamata viongozi hao wa Chadema, jana hiyo hiyo Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete walikuwa wakifanya mkutano katika Jimbo la Bagamoyo na mbunge wa jimbo hilo Shukuru Kawambwa.

Hali kama hiyo ya Ruvuma nusura itokee Igoma mkoani Mwanza baada ya Jeshi la Polisi kutaka kuzuia Kongamano la Chadema lililofanyika katika Ukumbi wa Hill Front.

Inaelezwa saa chache kabla ya mkutano huo kuanza, polisi walifika katika eneo hilo na kudai kuwa ni la wazi na si salama.

Jambo hilo liliibua mvutano mkubwa wa hoja kati ya Jeshi la Polisi na viongozi wa Chadema Kanda ya Ziwa Magharibi,  waliokuwa wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar, Salum Mwalim ambao walidai kuwa eneo hilo ni ukumbi.

Mwalim aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa baada ya kushinda hoja hiyo, polisi waliibua hoja nyingine wakidai kuwa eneo hilo lina sehemu ya baa, hivyo wakija wateja wanaweza kuwafanyia vurugu.

Alisema baada ya malumbano, hoja hiyo ikaonekana kukosa nguvu na hivyo kusababisha mkutano huo uliokuwa uanze saa nne asubuhi kuchelewa kwa saa nne zaidi na kuanza saa nane mchana.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alikiri kutokea kwa mvutano kidogo ambao alisema lengo la polisi lilikuwa ni kutaka kujiridhisha kama eneo hilo ni salama.

Msangi alisema baada ya kujiridhisha waliruhusu Chadema waendelee na mkutano wao.

 Habari hii imeandaliwa na Grace Shitundu (Dar), Amon Mtega (Ruvuma) na Frederick Katulanda (Mwanza).

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here