33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Katiba yapokewa kwa hisia tofauti

Kikwete na SheinNA WAANDISHI WETU

SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kukabidhiwa Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba, watu wa kada mbalimbali wameipokea kwa hisia tofauti.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, walisema kuna mambo mengi muhimu ambayo yameachwa ingawa imechukua zaidi ya asilimia 81 ya mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

PROFESA MPANGALA

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha Iringa, Profesa Gaudence Mpangala, alisema licha ya Katiba inayopendekezwa kuchukua asilimia 81.8 ya mambo yaliyokuwamo kwenye Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, haimaanishi mambo yote muhimu yamepitishwa.

Alisema miongoni mwa mambo muhimu yaliyoachwa ni muundo wa Muungano ambao umekuwa ukipigiwa kelele kwa muda mrefu.

“Ninahitaji kufanya uchambuzi wa kina wa Katiba inayopendekezwa kulingana na Rasimu ya Tume ya Katiba ili nitoe maoni, lakini naona kuna mambo ya msingi yaliyoachwa ambayo ndiyo yalikuwa yanabeba mabadiliko ya Katiba hii.

“Kwa mfano, suala la Serikali tatu lilikuwa jambo la msingi lakini limeachwa. Kama muundo huo ungebadilishwa kulingana na mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tungekuwa na mabadiliko ya kweli,” alisema.

Alitaja suala la kuwawajibisha wabunge, alisema lilikuwa limebeba dhana nzima ya madaraka ya wananchi kwa viongozi wao.

“Kuna suala la kuwawajibisha wabunge ambapo wananachi wangepata madaraka kwa viongozi wanaowachagua, lakini wamelitoa. Lipo pia suala la mawaziri kutokuwa wabunge limeachwa,” alisema.

TUCTA

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA), Nicholas Mgaya, alipinga suala la kuongezwa kwa idadi ya wabunge akisema litasababisha kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge, idadi ya wabunge haitapungua 340 wala kuzidi 350.

“Kuongezeka kwa wabunge ni gharama, kama tukiharakisha yanaweza kutupata kama yale yaliyotokea Kenya, waliweka vyeo vya maseneta na wabunge, sasa wamejikuta wanatumia gharama kubwa za kulipa mishahara na posho,” alisema Mgaya.

NCCR-MAGEUZI

Chama cha NCCR-Mageuzi kimesema hotuba ya Rais Kikwete imekuwa ya kuhadaa wananchi kutokana na kuwapo kwa mkanganyiko katika baadhi ya mambo.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe, alisema hotuba ya Rais Kikwete ina mikanganyiko kadhaa ikiwamo suala la kura ya maoni.

“Hotuba hii ni ya kuhadaa watu, anaposema mambo machache yafanyiwe marekebisho na Bunge la kawaida kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani, unashindwa kujua kinachofuata,” alisema Nyambabe.

SHEIKH ALHAD

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema kuwapo kwa tofauti za mawazo katika mchakato huo kusichukuliwe kama uadui kati ya wanasiasa.

“Hotuba ilikuwa nzuri haijawagawa Watanzania pamoja na changamoto zilizotajwa, lakini sisi ndio wenye kauli ya mwisho kama wananchi, hivyo tusubiri wakati wa upigaji kura za maoni utakapofika.

“Inawezekana wengine wakawa na mawazo tofauti, hivyo wasichukuliwe kama maadui, wawekane sawa ili tuvuke salama katika mchakato huu,” alisema Sheikh Salum.

TUNDU LISSU

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alishiriki kuwahamasisha wananchi waliofika katika viwanja vya Kilombero Samunge, Arusha kupiga kura ya hapana.

Alisema Katiba hiyo inayopendekezwa haijakidhi matakwa ya wananchi kutokana na mapendekezo mengi kuachwa.

Habari hii imeandaliwa na Nora Damian, Elias Msuya (Dar) na Janeth Mushi (Arusha)

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Mapendekezo si yale ya awali yaliyotokana na wananchi. Huu ni mtandao wa kundi fulani la majitu (siwezi waita watu)uliotumia mamlaka ghilba na uchu wao wa madaraka kuiteka dhamira njema ya kuunda katiba mpya ili kuendelea wanyonya wananchi waliokuwa na ndoto ya kujinasua katika mikono yao michafu iliyoshindwa kuwaletea maendeleo. Dhambi kubwa, katiba hiyo haramu inayopendekezwa haitodumu, ni uchafu na hauna suluhu yoyote ktk mustakbari wa Taifa na wananchi. Hatutosahau kudai katiba mpya kamwe. kwa namna yoyote fikra na akili za watu hazizimwi kirahisi hivi, katiba inayotufaa ipo siku itapatikana na si muda mrefu. tuwe watulivu, TIME wiLL tELL. Nafsi zao zitawasuta na hawatokuwa na pakujificha zaidi ya kufunika nyuso zao chini. Walichokifanya kina impact kubwa kwa siku za usoni. si wao (Viongozi na wana Chama Chao)wala sisi wanaotupuuza watakao salimika. Dhambi hii ya ulaghai ipo siku itawashukia . Yarrabi Salama

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles