31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

KATIBA INAYOPENDEKEZWA INASUBIRIWA SANA

BADO Watanzania wanasubiri kwa hamu sana kuipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa.

Baadhi ya vyombo vya habari vilizungumzia suala hili wiki iliyopita kama kukumbushia. Muda si mrefu mwaka jana pia Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) lilimshauri Rais Dk. John Magufuli, kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kukamilisha mchakato wa Katiba mpya.

Vile vile liliishauri Serikali kutekeleza ahadi yake iliyoitoa kwenye mkutano wa Kimataifa wa Universal Period Review Mechanism (UPR), Mei 2016 Geneva, Uswisi.

Katika mkutano huo, iliahidi kupitisha Katiba mpya mapema iwezekanavyo. Ahadi hiyo ya Serikali ilitolewa wakati wa kuwasilisha hali ya haki za binadamu Tanzania chini ya mpango huo.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Rais Dk. Magufuli hakuwa mgombea binafsi bali alipitia kwenye chama cha siasa cha CCM ambacho kilikuwa na Ilani yake, hivyo anapaswa kuitekeleza bila vikwazo.

Kwamba kwa kuwa CCM iliwaahidi wananchi ambao ndio waliompigia kura Rais Dk. Magufuli, litakuwa ni jambo jema kutimiza ahadi hiyo kwa faida ya Taifa.

Huu ni mwendelezo wa mchakato mrefu ambao umekwisha kufanyika tayari yapata karibu miaka mitatu sasa. Mwaka 2013 ulikuwa wa mvutano kati ya vyama vya upinzani na chama tawala, CCM, kuhusu aina ya Katiba mpya itakayoratibu maisha ya Watanzania kwa miaka mingi ijayo.

Tangu Bunge Maalumu la Katiba lilipoanza kikao chake mjini Dodoma Februari 18, 2013, liligeuzwa kuwa mkusanyiko wa watu wasio na mwelekeo na ambao hawakuonekana kujua tofauti kati ya ukumbi wa Bunge na vilabu vya pombe!

Lilikuwa Bunge la matusi kwenda mbele na hakuna kiongozi yeyote wa ngazi ya juu aliyesimama kukemea mwenendo huo wa kishetani!

Wajumbe wa Bunge hilo waliendelea kuvutana, kukejeliana, kukashifiana na hata kutukanana matusi ya nguoni na kufanya siasa badala ya kutumia muda mwingi kuangalia njia bora ya kupata Katiba mpya kwa pamoja.

Tunasema kuwa hii haikuwa sahihi, ulikuwa ni uhuni uliokuwa unaelekea kulipasua Taifa moja kwa moja. Wajumbe wanaounda Ukawa hatimaye walilisusia Bunge hilo kabla ya Katiba Inayopendekezwa kutolewa bila kuwapo kwao na kwa maridhiano!

Mara kadhaa kupitia safu hii tumekuwa tukisisitiza kuwa Katiba ya nchi hupatikana kwa maridhiano na njia za wazi zisizo na ila pamoja na hila. Bila mambo haya, katu Katiba haipatikani na ikipatikana itakuwa Katiba inayofusha moshi na ya kuvunja nchi vipande vipande!

Tunasema hii isiruhusiwe, hata wakati ukifika wa kuipigia kura ya maoni Katiba Iliyopendekezwa.

Hatuna budi kukumbusha kuwa Katiba Inayopendekezwa ilipitishwa kwa mbinu chafu, bila kuwapo kwa maridhiano kati ya wajumbe wa CCM na Ukawa.

Aidha, mambo mengi ya msingi ambayo watu walipendekeza yaliondolewa kitendo ambacho hakileti tija kwa ustawi wa nchi yetu.

Tunasema kuna haja ya kuangalia upya kuyarejesha kwenye Katiba Inayopendekezwa yale ambayo yanaipa nchi manufaa na tija kwa maendeleo yake na kuipa heshima Katiba mpya itakayopatikana.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles