30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Katambi apongeza ubunifu Bonnah Segerea Cup, ataka vijana walindwe

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, amempongeza Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, kwa kuandaa mashindano ya vijana na kutoa wito kwa jamii kuisaidia Serikali kuhakikisha kundi hilo ambalo ndiyo nguvu kazi ya taifa inalindwa.

Mashindano hayo yaliyoanza kutimua vumbi Aprili 5,2024 yameshirikisha timu 61 za mitaa ya Jimbo la Segerea na timu tatu za makundi ya waendesha bajaji, bodaboda na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi (Wapili kushoto) akiwa kwenye mazoezi wakati wa fainali za mashindano ya Bonnah Segerea Cup viwanja vya Kecha Kinyerezi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na Wapili Kulia ni Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli.

Akizungumza leo Juni 9,2024 wakati wa fainali zilizofanyika uwanja wa Kecha Kinyerezi, Dar es Salaam amesema mashindano hayo yanaongeza chachu kwa vijana kudumisha undungu, kukuza vipaji, kuiimarika kiafya na kupata fursa za ajira.

“Tunao wajibu mkubwa kama taifa kumsaidia Rais Samia kuhakikisha vijana ambao ni asilimia 34.6 ya watu wote nchini wanalindwa. Usipowalinda na kuangalia masilahi yao maana yake hakutakuwa na mwendelezo wa taifa, huwezi kupata viongozi wazuri kwa sababu utakuwa umepuuza kundi la vijana.

“Tuangalie makuzi yao, tuwatambue popote walipo, tuwasilikize na kuwahudumia kupitia sheria na sera zilizopo zinazotoa fursa kwa vijana kuongoza uchumi,” amesema Katambi.

Naibu Waziri huyo pia amewaasa vijana kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwani kundi hilo limeathiriwa zaidi hasa kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 25.

Naye Bonnah amesema amekuwa akiandaa mashindano hayo kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM hasa ikizingatiwa kwamba michezo ni ajira na afya.

“Mashindano haya yanalenga kuibua na kukuza vipaji vya vijana sambamba na kuwapatia fursa mbalimbali, kupitia michezo tutaweza pia kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yetu,” amesema Bonnah.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amempongeza Bonnah kwa kuandaa mashindano hayo ambayo yanaimarisha umoja na mshikamano kuanzia ngazi ya mtaa, kata hadi wilaya.

“Jimbo la Segerea limepiga hatua kubwa kimaendeleo siyo kwenye michezo pekee, kazi nzuri imefanywa na mheshimiwa Bonnah na inaonekana, zaidi ya shule tano za ghorofa zinajengwa, kuna mradi mkubwa wa maji, vituo vya afya na mingine,” amesema Mpogolo.

Katika mashindano hayo timu ya soka ya Kisiwani kutoka Kata ya Bonyokwa imeibuka mshindi na kuzawadiwa fedha taslimu Sh milioni 5 wakati Mivinjeni ya Buguruni iliyoibuka mshindi wa pili imezawadiwa Sh milioni 3.

Fainali hizo zilitanguliwa na Jogging ambapo mbio zilianza asubuhi katika Uwanja wa Toto Tundu (Segerea) na kuishia viwanja vya Kecha.

Mbunge huyo pia aligawa viti 75 kwa Kikundi cha Jogging cha Segerea ili kiweze kujiimarisha kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles