JANA Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilizindua ripoti mpya yenye jina ‘Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara Tanzania Bara’ ya mwaka 2018/19 ambayo pamoja na mambo mengine, imebaini changamoto luluki zinazowakumba wafanyakazi maeneo mbalimbali nchini.
Ripoti hiyo imeibua madudu zaidi, hasa kwa wafanyakazi wa viwandani ambao kwa kiasi kikubwa wengi wanafanya kazi bila mikataba, masilahi duni, kutothaminiwa na waajiri na hata kunyanyaswa kijinsia.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wafanyakazi wengi wa viwandani na maeneo mengine nchini hawana mikataba ya ajira na hata pale ambapo wana mikataba ya ajira, masilahi wanayolipwa hayaendani kabisa na makubaliano yaliyoko kwenye mikataba hiyo.
Tunaamini kasoro kama hizi mbali na kuminya haki za mfanyakazi, zinadumaza uchumi wa nchi kwani imebainika wafanyakazi wengi ambao hawana mikataba ya kueleweka hawalipi kodi na hivyo Serikali kupoteza mapato mengi.
Kwa vyovyote vile na hata kwa kufuata misingi ya kisheria, ni kosa kumwajiri mfanyakazi kwa muda mrefu bila kumpa mkataba wa makubaliano ya ajira.
Hivyo sisi wa MTANZANIA tunatoa rai kwa waajiri hasa wenye viwanda kutimiza wajibu wao muhimu kama wawekezaji kwa kutii sheria za nchi bila shuruti, kwani kwa kupuuza sheria hizi Serikali haitasita kuchukua hatua.
Ndiyo maana tunaamini kuwa macho ya Serikali ni makubwa na katu hawawezi kufumbia macho uvunjifu huu wa sheria za nchi unaoendelea katika sehemu mbalimbali.
Vilevile, tunaamini kuwa kituo cha haki za binadamu watawasilisha vielelezo na nyaraka muhimu wa tafiti zao kuhusu kadhia hii kwa mamlaka za Serikali ili ziweze kuchukua hatua stahiki na haraka kabla ya hali kuendelea kuwa mbaya.
Pia ripoti hiyo imegundua kwamba idadi ya wafanyakazi ambao hawana mikataba ya ajira inaongezeka kila mwaka kwani imebainika katika utafiti wa mwaka huu kuwa idadi ya asilimia imekuwa nyingi kuliko za mwaka jana.
Kwa matiki hiyo, ongezeko hili la watu kutokuwa na mikataba ni ishara kwamba kuna ufuatiliaji finyu wa mamlaka zinazohusika kulinda haki ya mfanyakazi au kwa maneno mengine ripoti za aina hii hazifanyiwi kazi kwa kasi inayopaswa.
Vilevile, katika ripoti yao wamebaini kwamba kuna wafanyakazi wengi wanatumika kwa muda wa ziada bila kulipwa malipo ya ziada.
Tunaamini kwamba kumtumikisha mfanyakazi kwa muda wa ziada bila masilahi ya ziada ni unyonyaji na uvunjifu wa utu wa mwanadamu.
Pamoja na imani hiyo, pia kiafya sio jambo jema sana kumfanyisha mtu kazi kwa muda wa zaidi ya saa nane ambazo zimeidhinishwa na Shirika la Kazi Duniani kwa mtu kufanya kazi kwa siku.
Kibaya zaidi ripoti hiyo imebaini kuwapo kwa ubaguzi katika sehemu za kazi. Unyanyasaji wa kijinsia, ubaguzi wa rangi katika ofisi nyingi ambazo zinamilikiwa na wageni, ni moja ya kero kubwa ambazo tungependa zifuatiliwe kwa kasi na hatua madhubuti zichukuliwe.
Hivyo basi, ni matumaini yetu kwamba kero zote zilizoibuliwa zitafanyiwa kazi na wahusika ili mwakani ripoti ionyeshe ahueni. Tunaamini kwa kuondoa kero kazini tunajenga jamii imara ambayo itajenga uchumi imara wa taifa letu.