Na Clara Matimo, Magu
Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza imemkosha Mkuu wa mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel baada yakuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo imekusanya zaidi ya Sh bilioni moja kutoka malengo ya Sh milioni 800.
Hayo yamebainishwa Juni 25, mwaka huu na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mpandalume Simon wakati akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa nje (CAG) kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kwenye mkutano maalumu wa baraza la madiwani uliolenga kujadili hoja hizo.
Simon amesema kiasi hicho cha fedha ni sawa na asilimia 130 ya makusanyo ya ndani ambayo walipanga kuyakamilisha ifikapa Juni 30, mwaka huu huku akieleza kwamba fedha za mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalumu walipanga kutenga Sh milioni 200 lakini wameishapeleka Sh milioni 260.
“Tunakushukuru sana Mkuu wa Mkoa wetu, Mhandisi Robert Gabriel, kwa maelekezo yako, ulifanya ziara ya kutuelimisha kuhusu fedha zilizokuwa zinapotea kwenye mikopo ya asilimia 10 ulituelekeza tufanye ziara ya kukagua vikundi tulitekeleza na tumebaini vipo ambavyo vimekufa na vingine vimeteteleka kwenye marejesho.
“Lakini kwa maelekezo yako tulifanya ufuatiliaji na nikiri kwamba ziara hiyo tuliifanya kwa sababu ya maelekezo yako maana huko nyuma hatukuwahi kufanya hivyo kwa kweli tunakushukuru sana kwa usimamizi wako mzuri na maelekezo ambayo umekuwa ukiyatoa kwa sisi viongozi wenzio, tuko tayari kuendddele kuyatekeleza maana yanatija kwa mustakabali wa maendeleo ya halmahsuri, mkoa na nchi yetu,” amesema Simon.
Aidha, ameeleza kwamba usimamizi wa mali za umma unahitaji watu wanyoofu wa moyo na vitendo nao wamedhamiria kuwatumikia wananchi hivyo badala ya kutawanya fedha kwenye miradi mingi ambayo inabaki bila kukamilika watahakikisha wanatoa kipaumbele kwa ile ambayo jamii inauhitaji nayo zaidi ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa huduma kwa raia wake.
Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Nje (CAG) Mkoa wa Mwanza, Waziri Shabani, amesema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 halmashauri ya wilaya ya Magu ilipata hati inayoridhisha, jumla ya hoja 32 sawa na asilimia 39 hazijatekelezwa kikamilifu ziko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji 51 zimefungwa.
“Tunakushukuru sana mkuu wa mkoa kwa elimu unayoitoa kwenye halmashauri zote ambazo umepita kuongoza mkutano wa aina hii hakika elimu hiyo inatusaidia kupunguza pengo la uelewa wa ukaguzi kwa madiwani jinsi wakaguzi tunavyofanya kazi tunatarajia wazuea hoja mapema wakati wa ukaguzi kwa kuboresha mifumo ya ndani ili waendelee kupata hati safi,” amesema Shabani.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, amesema: “Hapa hatuna mzee wote ni kazi tutasimamia kikamilifu miradi yote kikamilifu pia tutahakikisha tunajibu hoja zote zilizopo ili tuzimalize maana zinajibika, wakuu wa idara wote tunajenga nyumba moja tuendelee kushirikiana na ofisi yangu kutekeleza ilani ya CCM,”amesema.
Kwa upande wake, Mhandisi Gabriel ameiipongeza halmashauri hiyo kwa kudhibiti upotevu wa fedha na kutekeleza miradi ambayo ina thamani halisi ya fedha huku akishauri kufanya tathmini ya vyanzo vyote vya mapato waimarishe vilivyopo na kubuni vipya ili kuongeza mapato pia waimarishe mifumo ya udhibiti wa upotevu wa fedha za umma.
“Hii halmashaur ni tofauti na zingine ambazo nimeishapita kule tunatafuta wabadhilifu wa fedha za umma hapa haupo pongezi kwa mkurugenzi na wakuu wote wa idara kwa kuwa waadilifu kwenye fedha za umma mafanikio haya yanathibitisha hanna migogoro wote mnafanya kazi kwa kushirikiana maana katika kila mgogoro kuna anayefaidika fanyeni tathmini ya bajeti muweze kumaliza maboma ambayo yanazidi kuongezeka.
“Halmashauri hii ya Magu inautofauti wa pekee na zingine ambazo nimeishapita haijapuuza maagizo ya CAG hapa hakuna hoja ambayo hamjaitekeleza pamoja na kwamba baadhi zinamajibu dhaifu lakini zote mmezitekeleza, halmashauri zingine ingawa kuna wataalamu lakini unakuta hoja ina miaka mitano bila utekelezaji hoja inaonyesha uwezo wa kusimamia halmashauri,” amesema Mhandisi Gabriel.