24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

KASI YA TALAKA MAHAKAMANI YATISHA

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

KESI za kudai talaka zimeongezeka kwa kasi katika mahakama mbalimbali nchini, huku sababu za nyumba ndogo na ujana zikitawala, MTANZANIA Jumapili limebaini.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unaokadiriwa kuwa na idadi kubwa ya watu inayofikia milioni tano ndio unaoongoza kwa kesi hizo.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba mwaka jana, kulikuwa na kesi 1,847 za madai ya talaka zilizofunguliwa katika mahakama za Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kaimu Msajili wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam, Mustapha Siyani, kesi hizo ni zile zilizofunguliwa katika Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Kivukoni, mahakama za wilaya na za mwanzo.

Inaelezwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa mwaka jana kulikuwa na kesi nne za madai ya talaka, ikifuatiwa na ile ya Hakimu Mkazi Kisutu ambayo ilipokea kesi 57 huku ya Kivukoni ikipokea 190.

Wilaya ya Kinondoni ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya kesi za talaka zilizofunguliwa katika mahakama za wilaya na za mwanzo. Jumla ya kesi 613 zilifunguliwa kwa mwaka jana pekee.

Upande wa Ilala, jumla ya kesi za talaka 570 zilifunguliwa katika mahakama zake zote idadi ambayo inaifanya manispaa hiyo kushika nafasi ya pili nyuma ya Kinondoni kwa idadi ya kesi hizo.

Madai ya talaka kwenye mahakama ya Wilaya ya Temeke na mahakama zake za mwanzo kwa kipindi cha mwaka jana ilikuwa ni 413 idadi ambayo ni ya chini ikilinganishwa na ya mahakama za Kinondoni na Ilala.

TALAKA ZILIZOSAJILIWA

Taarifa iliyotolewa Juni mwaka jana na Wakala wa Usajili wa Vizazi, Vifo, Talaka na Ndoa (RITA), inafafanua kuwa mwaka 2013/14 jumla ya talaka 99 zilisajiliwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jumla ya talaka 150 zilisajiliwa mwaka 2014/15.

Mbali na taarifa hiyo, takwimu za Mahakama ya Kadhi Zanzibar, zinaonyesha kuwa zaidi ya talaka 1,600 zilitolewa visiwani humo kati ya mwaka 2012 na 2013.

Aidha mahakama sita za kisiwani Unguja zilikuwa na jumla ya kesi 1,917 za talaka.

SABABU ZA NDOA KUVUNJIKA

Sababu mbalimbali zimeelezwa kama chanzo cha wanandoa wengi kwenda mahakamani kutaka kutalikiana, huku ujana na nyumba ndogo zikitawala.

Akifafanua zaidi juu ya sababu hizo, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Kawe wilayani Kinondoni, Gladness Anthony, alisema kuwa kundi kubwa la wanandoa wanaoongoza kwenda mahakamani kutaka kutalikiana ni vijana huku wanawake wakiongoza.

“Kuna sababu nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa na wanandoa pindi wanapofika mahakamani, lakini kubwa imekuwa ni nyumba ndogo kwani wengi wamekuwa wakilalamika kuwafumania wenzi wao, hasa wanaume.

“Hali hiyo inachangiwa zaidi na makundi, ulevi na klabu za usiku. Lakini suala la ukatili, matusi na vipigo wanavyopata wanawake kutoka kwa wanaume pindi wanapoolewa, imekuwa ni sababu nyingine inayofanya wanawake wengi kukosa uvumilivu na kuona bora kutalikiana.

“Mfano unaweza kukuta mama anakuja kuomba talaka anakwambia kuwa mume wake amekuwa akimzimia sigara kwenye mapaja yake, hivyo wengi wanaona bora waondoke kuliko kuishi kwenye manyanyaso,” alisema Gladness.

Kwa mujibu wa hakimu huyo, sababu nyingine ni pamoja na ugumu wa maisha, kwamba wanawake wengi wamekuwa wakidai kukosa mahitaji yao ya msingi na hivyo kuomba utengano ili kutafuta mahala wanakoweza kupata mahitaji.

“Kuna sababu nyingine ambazo hizi zinahusisha ugumu wa maisha. Hii imekuwa ikichangiwa na wanaume, ambao pindi inapotokea wamepata nyumba ndogo, wamekuwa wakiwanyanyapaa wake zao wa ndoa na hivyo kusababisha furaha kukosekana ndani ya nyumba.

“Wengi wanadai kuwa wanakosa unyumba, mahitaji muhimu kama chakula, mavazi, baba kushindwa kulipia ada za watoto licha ya kuwa na uwezo,” alisema.

Kwa mujibu wa hakimu huyo, ndoa za vijana ndio zinaongoza kuvunjika.

“Zaidi ya asilimia 56 ya kundi linaloongoza kudai talaka mahakamani ni pamoja na vijana ambao wamekuwa wakieleza kuwa wanafikia uamuzi huo kwa kuwa walikuwa hawajawa tayari kuwa kwenye ndoa.

“Utakuta vijana wanakueleza kuwa ‘tulikuwa tunaishi tu, lakini hatujajitambua, hivyo tulifunga ndoa kimakosa ila ukweli ni kwamba hatukuwa tayari kuingia kwenye ndoa’ na utabaini kuwa ndoa nyingi za vijana wengi zinakuwa hazizidi miaka minne,” alisema.

Hakimu mwingine kutoka katika Mahakama ya Mwanzo Mbagala, Dar es Salaam, ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, aliitaja sababu nyingine inayosababisha kuvunjika kwa ndoa hizo kuwa ni pamoja na ugumba.

“Kukosa mtoto ni sababu ambayo imeendelea kuwa mwiba kwa wanandoa, kwani unakuta wanandoa wameishi miaka mitatu bila ya kuwa na mtoto na hapo ndipo mwanzo wa vurugu unapoanza,” alisema.

Wanawake wenye kipato kikubwa kuliko waume zao nao wanatajwa kuchangia ongezeko la talaka.

 “Unakuta mwanamke anamwambia mwanamume aoshe vyombo, apike, afue na mambo mengine chungu nzima kwa vile tu mke wake huyo ana kipato jambo ambalo wanaume wengi wamekuwa hawako tayari kukubaliana nalo, lakini pia wamekuwa wakitaka kutumia mwanya huo kuwanyanyasa, ikiwamo kuchelewa kurudi kwa madai ya kazi nyingi.

“Mwanamume anafika mahakamani anaeleza kuwa mke wake anamnyanyasa na kwamba hana uhuru kama mwanamume kulingana tu kwamba mkewe huyo ana kipato na hivyo kuhitaji kutalikiana,” alisema.

Inaelezwa kuwa kati ya mashauri 100 ya talaka yanayofunguliwa kwenye mahakama hizo, ni asilimia moja tu ya kesi ambazo wanandoa wamekuwa wakirudiana huku nyingine zikisambaratika kabisa.

“Kwenye madai mengi ya talaka yanayofunguliwa huwa ni kazi kubwa kuwashauri wanandoa kurudiana pamoja na kuishi kama zamani, hivyo wengi wakishachukua uamuzi wa kufungua kesi ya madai ya talaka huwa hawako tayari kurudi nyuma licha ya athari wanazoambiwa mahakamani iwapo watatengana,” alisema.

SHERIA YA NDOA

Kwa mujibu wa sheria ya ndoa tafsiri ya ndoa namba 5 ya mwaka 1971, ndoa ni muunganiko wa hiari  kati ya mwanamume na mwanamke, unaokusudiwa kudumu kwa muda wote wa maisha yao.

Muungano huo ni lazima kati ya watu wa jinsia tofauti na uwe umefungwa kwa hiari, iwapo hakukuwa na hiari kwa mmoja katika wafunga ndoa, hiyo si ndoa ya kisheria.

Sheria hiyo inaenda mbali zaidi kwa kusema kuwa ndoa inaweza kuwa batili endapo tu, mmoja wa wafunga ndoa hana uwezo wa kutimiza tendo la ndoa, kuwa na wazimu, kukutwa na ugonjwa wa zinaa, kubeba ujauzito wa mwanamume mwingine.

Sababu nyingine ni juu ya mke kuwa chini ya umri wa miaka 18 na kutokuwa na idhini ya wazazi/walezi na mmoja wa wafunga ndoa kukataa kutimiza tendo la ndoa kwa makusudi.

TALAKA

Kwa mujibu wa sheria hiyo ya ndoa tofauti kubwa na ya wazi kati ya kutengana na talaka, ni kuwa wakati wa kutengana, mume na mke huishi mbalimbali na masuala ya unyumba au tendo la ndoa huwa halipo.

Hali hiyo ni tofauti na utaratibu wa kawaida katika mahusiano ya ndoa ambapo talaka ni kuvunjika kwa ndoa na hakuna uhusiano wa mume na mke tena bali wanakuwa watalikiwa.

Mahakama imepewa uwezo na mamlaka kisheria kutoa amri kwa waliooana kupeana talaka, kwamba sheria hiyo inatambua kutengana kwa hiari kunakofanywa na wanandoa wenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Wanaofungisha ndoa wafundishwe sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ili wawe wanawafundisha walioko kwenye ndoa na wanaotaka kufunga ndoa.Pia walioko kwenye ndoa na wanaotaka kufunga ndoa wafundishwe taratibu za ndoa za dini yao.Mfano kwa dini ya Kikristo Ayubu alikuwa na mke dhaifu lakini hakumwacha, Abigaili alikuwa na mume dhaifu lakini hakumwacha. Hekima ni ulinzi, hekima humlinda aliye nayo Mhubiri 7:12

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles