TOKYO, JAPAN
KASHFA ya kumpendelea rafiki yake wa muda mrefu, inaonekana kuathiri umaarufu wa Waziri Mku wa Japan, Shinzo Abe.
Lakini Abe jana alikana kuwahi kuwaagiza maafisa wake kumpendelea Kotaro Kake, akiongeza kuwa rafiki huyo hakuwahi kuomba au kutaka asaidiwe.
Abe na wasaidizi wake mara kadhaa wamekana kuingilia kati kuisaidia taasisi ya elimu ya Kake Gakuen, ambaye mkurugenzi wake ni rafiki huyo.
Upendeleo huo unadaiwa ni kumwezesha Kake kupata kibali cha kuanzisha chuo cha matibabu ya wanyama katika kanda muhimu ya kiuchumi.
Uungwaji mkono wa Abe umeporomoka chini ya asilimia 30 baada ya Wajapan kupitia kura ya maoni kuwa na shaka kuhusu kashfa hiyo.
Kwa mujibu wa kura ya maoni, mtazamo wa wapiga kura wengi, kwamba utawala wake hauwajali.
Uungaji mkono wa Abe unawahimiza wapinzani wake na kutilia shaka uwezekano wa Abe kuwa waziri mkuu wa Japan wa muda mrefu.
Hilo linaweka uwezekano wa utawala wake kukomea Septemba 2018 wakati muhula wake wa pili utakapomalizika badala ya kuendelea na muhula mwingine wa tatu wa miaka mitatu.