27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kashfa ya ubakaji inavyo hatarisha utajiri wa Ronaldo

NA BADI MCHOMOLO

WANAMICHEZO wengi wanakuwa matajiri sio kwa sababu ya mishahara wanayolipwa kwa wiki au mwezi kwenye timu zao, kuna kiasi kikubwa cha fedha ambacho wanakipata zaidi ya mishahara kutokana na mikataba ya matangazo.

Mbali na kufanya matangazo, wanamichezo wengi wanatumia kiasi chao kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye biashara mbalimbali ili kuja kunufaika mara baada ya kutangaza kustaafu mchezo husika.

Cristiano Ronaldo ni mmoja kati ya wanamichezo matajiri duniani, mchezaji huyo ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Juventus ya nchini Italia akitokea Real Madrid wakati huu wa majira ya joto, anaongoza kwa kuchukua kiasi kikubwa kuliko wanasoka wote nchini Italia.

Anachukua kiasi cha pauni milioni 19.4 kwa mwaka, huku kabla ya mchezaji huyo alikuwa anaongoza Gonzalo Higuain anayechukua kiasi cha pauni milioni 8.6 kwa mwaka baada ya kuondoka Juventus na kujiunga na AC Milan.

Hata hiyo Ronaldo anachukua kiasi cha pauni 538,000 kwa wiki, ambazo ni zaidi ya bilioni 1 na milioni 500 kwa wiki kabla ya kufanyiwa makato mbalimbali ya kodi.

Kwa sasa tajiri huyo ameingia kwenye kesi ya kashfa ya ubakaji, ambapo tukio hilo alilifanya mwaka 2009, katika hoteli jijini Las Vegas.

Inadaiwa kwamba mchezaji huyo alilazimisha kufanya mapenzi na mrembo Kathryn Mayorga, kitendo hicho cha ulazimishaji kinajulikana kama ubakaji.

Hata hivyo Ronaldo mwenyewe amekanusha kashfa hiyo, huku polisi jijini Las Vegas wakiweka wazi kuwa, wapo kwenye uchunguzi wa tukio hilo ambalo lilitokea miaka tisa iliopita.

Katika wachezaji wa soka, Ronaldo anatajwa kuongoza kwa kuwa na mikataba mingi ya matangazo na makampuni ya biashara kama vile Nike, Herbalife, JBS, Samsung, Exness, PanzerGlass, Egyptian Steel, American Tourister, EA Sports na Toyota.

Hizo ni baadhi za kampuni ambazo hadi sasa bado ana mkataba nazo na zinamfanya aonekane kuwa miongoni mwa wachezaji matajiri kutokana na kiasi cha fedha anazochukua kwa kila kampuni hadi sasa.

Mwaka 2010 mchezaji huyo alisaini mkataba wa maisha na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike, huku mkataba huo ukitajwa kuwa na thamani ya dola bilioni 1.

Lakini baada ya wiki iliopita kuenea kwa taarifa za kashfa ya ubakaji kwa mchezaji huyo, Nike imeonesha dalili za kutaka kuvunja mkataba na mchezaji huyo.

Nike wamedai kuwa, kwa sasa wanasubiri uchunguzi unaofanywa na polisi juu ya tuhuma hizo ili na wao waweze kuchukua hatua, wamesema hawawezi kusapoti vitendo hivyo vya unyanyasaji wa kijinsia kama tuhuma hizo zitakuwa za kweli.

Nike imekuwa ikipambana kumtengenezea viatu mchezaji huyo ambapo hadi sasa tangu mwaka 2003 ametengenezewa zaidi ya viatu 70 vyenye muonekano tofauti uwanjani.

Mbali na Nike kuoneshwa kuguswa na kitendo hicho, kampuni ya EA Sports, imejitokeza na kusema wanafuatilia tuhuma ambazo zinamkumba mchezaji huyo na kama zitakuwa na ukweli basi na wao watatoa tamko lao.

Hizo ni baadhi ya kampuni ambazo anazitangazia mchezaji huo na kumuongezea kipato chake, lakini kama kutakuwa na ukweli wa tuhuma hizo basi kuna uwezekano mkubwa wa kampuni zingine kujitokeza na kutoa matamko mazito.

Endapo itafikia hatua hiyo, basi Ronaldo atapoteza kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinamfanya awe juu katika pato la mwaka.

Klabu ya Juventus kwa kutetea maslahi yao wameonesha wazi kumtetea mchezaji huyo huku wakidai kuwa ni mchezaji mwenye nidhamu ya hali ya juu hivyo hawezi kufanya jambo kama hilo.

Makampuni ya matangazo siku zote yamekuwa yakijitoa kwa mastaa ambao wanafanya kitu kinachopingwa na jamii.

Bingwa wa zamani wa mchezo wa tenisi kwa upande wa wanawake nchini Urusi, Maria Sharapova, aliwahi kuingia kwenye msukosuko wa baadhi ya kampuni kujitoa kwenye udhamini baada ya kugundulika kuwa alitumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Tukio hilo lilitokea mwaka 2016, hivyo Nike ambao walikuwa miongoni mwa kampuni ambazo zilikuwa zinamdhamini mchezaji huyo ilitangaza kuvunja mkataba wake wa udhamini na mchezaji huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles