26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kashfa ya rushwa yanyemelea Bunge

3-naibu spika wa Bunge Job Ndugai akifafanua miongozo mbalimbali Buungeni leo-742501NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wameanza kutuhumiana kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wenye ukwasi mkubwa na watumishi wenye nyadhifa za juu katika ofisi za umma ili wawasaidie kulinda maslahi yao.

Baadhi ya wabunge waliozungumza na   MTANZANIA mwishoni mwa wiki   katika ofisi za Bunge, Dar es Salaam kwa sharti la majina yao kuhifadhiwa kwa sababu siyo wasemaji wa Bunge, walisema tayari majina ya watuhumiwa hao yamefikishwa  ofisi ya Spika, Job Ndugai.

Walisema walibaini kuwapo  tuhuma hizo  baada   Ndugai kuwaita baadhi ya wenyeviti wa Kamati za Bunge na kuwaonya kuhusu mienendo yao ya uongozi huku akiwataka kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ya zamani kwa vile mambo yamebadilika.

Mmoja wa wabunge aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la jina lake kutotajwa gazetini, alieleza kuwa  vyombo vya uchunguzi vilimkabidhi Spika Ndugai, majina ya wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge waliobainika kuhongwa na wafanyabiashara na maofisa waandamizi wa ofisi za umma.

Alisema katika orodha hiyo, wapo pia wabunge ambao wameingizwa kwenye orodha ya malipo ya kila mwezi ya mamilioni ya shilingi ya wafanyabiashara na maofisa hao wa umma, lengo likiwa kulinda maslahi yao.

Mbunge huyo alisema  Spika Ndugai alikutana na watuhumiwa hao ofisini kwake wiki iliyopita na kuwaonya kuwa vitendo vyao vya kuchukua mamilioni ya shilingi kutoka kwa wafanyabiashara na watumishi waandamizi wa umma kwa lengo la kutumia Bunge kuwalinda, vinakwenda kinyume na majukumu ya kazi za ubunge.

“Spika aliwaambia  amepata taarifa za uhakika kutoka kwa maofisa wa Serikali wanaohusika na mambo ya uchunguzi kuwa wamehongwa mamilioni kwa ajili kujiandaa kujenga hoja za kutetea au kushambulia wabunge wenzao watakaogusa maslahi ya wafanyabiashara na maofisa hao wakati wa mkutano wa Bunge la Bajeti,” alisema.

Alisema  tangu kuzunduliwa Bunge la 11, zimekuwapo ziara zisizoisha za wafanyabiashara wakubwa na maofisa waandamizi wa Serikali kuwafikia wenyeviti wa Kamati za Bunge, lakini baada ya uchunguzi wa sasa ndiyo imebainika  zina lengo la kuwanunua.

“Unajua, hili Bunge la 11 linawachanganya sana watu kwa sababu hata ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuna wabunge wanaotofautiana sana kwa misimamo. Sasa wapo ambao wameapa kutofumbia macho ufisadi na wanapata nguvu kutokana na msimamo wa rais wa kutumbua majipu.

“Sasa tulishangaa hapo mwanzoni tulipoanza kuwaona wafanyabiashara na wakati mwingine maofisa wa juu wa Serikali wakikutana mara kwa mara na baadhi ya wenyeviti wetu na baadaye ndiyo imebainika  kumbe lengo lao lilikuwa  kujenga ushawishi wa kutetewa bungeni.

“Majina yao wote yako kwa Spika na kila kitu kuhusu kashfa yao hii. Spika mwenyewe amekwisha kukutana nao na amewaonya, nasikia kuna hatua zaidi zinakuja.

“Ila tafadhali sana usinitaje mimi siyo msemaji, nasema nikiwa bungeni siyo huku nje, nyie subirini nadhani mtapewa taarifa tu viongozi wetu wa Bunge,” alisema mbunge huyo.

Alipotafutwa, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah  kuzungumzia suala hilo na hasa iwapo barua hiyo yenye tuhuma nzito dhidi ya wenyeviti wa Kamati za Bunge imefika mezani kwake, simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi hakujibu.

Naye Spika Ndugai alipotafutwa, simu yake ilikuwa haipatikani na jitihada za kuwatafuta wenyeviti wa kamati za Bunge wanaotuhumiwa kupokea rushwa hazikuweza kufanikiwa jana hadi tunakwenda mitamboni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles