28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kasha la mazimwi wa dunia lilipofunguliwa Panama

MWANZONI mwa mwezi uliopita nyaraka za Panama zilizua taharuki iliyohanikiza dunia nzima zilipoibuka kashfa iliyojitofautisha na kashfa zinazohusisha nchi moja moja. Lundo la nyaraka milioni 11.5 lina taarifa za kampuni zaidi ya laki mbili za ugenini ziliyomo katika orodha ya kampuni za ushauri ya Mossack Fonseca zinazobainisha wamiliki, wenye hisa na viongozi wakuu wa kampuni hizo.

Ni kawaida katika mfumo wa kibiashara kuendesha kampuni nje ya nchi anayotoka mmiliki lakini kisichokuwa cha kawaida kuhusu nyaraka za Panama, ni utajiri wa viongozi mbalimbali duniani ulivyofutikwa usifahamike kwa sababu zinazotia shaka. Awali walitajwa vigogo wachache na ndugu zao lakini baadaye ikadhihirika kuwa visiwa vya Virgins vinavyomilikiwa na Uingereza na visiwa vya Hong Kong ndipo vichaka vya maficho vilipo.

Kumiliki kampuni nje ya taifa si uvunjaji sheria lakini kampuni hizo zimetumika kwa uhalifu ukiwamo ukwepaji kodi na ufisadi. Kasha la mazimwi wa uhalifu huo lilifunguliwa na Mwandishi aliyejipa jina la bandia ‘John Joe’ aliyeanika mambo hayo hadharani, katika gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung mapema mwaka jana kuhusu mchezo huo mchafu ulioanza mwaka 1970. Baadaye nyaraka hizo zilisambazwa kwa waandishi 400 kupitia muungano wa waandishi wa habari za kipelelezi duniami (ICIJ), katika vyombo vya habari 107 kwenye nchi 76.

Kama ilivyokuwa katika hekaya za kale za Kigiriki za Esopo ambapo kasha lililofungiwa mazimwi (Pandora’s Box), lililodhibitiwa na mwanamke thabiti wa kwanza duniani (Pandora) aliyeumbwa kwa maji na udongo, lakini kasha hilo lilipovunjika liliyamwaga maovu yote duniani kama nyaraka za Panama zilivyoibua mazimwi (ufisadi) kutoka nchi mbalimbali zikiwamo Argentina, Armenia, Australia, Azerbeijan, Bangladesh, Brazil, Canada, Chile, China, Colombia, Cyprus, Misri, Ufaransa, Hong Kong, Iceland, India, Indonesia na Israel.

Nyingine ni Italy, Malta, Mexico, New Zealand, Norway, Pakistan, Urusi, Saudi Arabia, Singapore, Hispania, Sweden, Switzerland, Thailand, Tunisia, Ukraine, Falme za Kiarabu, Uingereza na Marekani.

Umiliki kampuni nje ya nchi hizo na kinga ya kudhihirishwa taarifa zao na tozo ndogo ya kodi, umetumiwa vibaya kifisadi kwa manufaa ya wanene wa nchi hizo.

Mossack Fonseca inayosimamia kampuni laki tatu inalaumiwa kwa kuzichezea nyaraka hizo ili kuwakinga wateja wake, kuzuia utambulisho wa wamiliki na kutatanisha hesabu za matumizi na faida ili kuwaneemesha kinyemela hivyo kuathiri uchumi duniani.

Pengo baina ya matajiri na masikini limeongezeka kwa ukwepaji kodi stahiki zinazohitajika huku waathirika wakubwa zikiwa nchi zilizoendelea, zilizokosa mapato yanayokadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 213 kwa mwezi Julai pekee mnamo mwaka jana.

Mossack Fonseca ilidai kuhujumiwa mawasiliano yake ya mtandao lakini baada ya nyaraka kuanza kuvuja ikakana kuhusika nazo, upekuzi wa kitaalamu ukadhihirisha kwamba ilikuwa ikichezea mtandao kwa nyaraka zenye nakala zisizorandana ili kuficha ukweli.

Aliyevujisha siri hiyo alisema aliamua kufanya hivyo ili dunia ifahamu ukweli ingawa hadi tuhuma hizo zidhibitishwe ndipo itakapojulikana ithibati yake. Majina yanayotajwa ni pamoja na Rais wa UAE Khalifa bin Zayed Al Nahyan, Mfalme Salman wa Saudi Arabia na Waziri Mkuu wa Iceland Sigmundur Gunnlaugsson. Wamo pia viongozi wa zamani akiwamo Rais wa Sudan Ahmed Al-Mirghani, Mtawala wa Quatar Hamad bin Khalifa Al Thani.

Wamo pia mawaziri wakuu wa zamani wa (Georgia): Bidzina Ivanishvili, (Iraq): Ayaq Allawi, (Jordan): Ali Abu al-Ragheb, (Quatar): Jaber Al Thani, (Ukraine): Paylo Lazarenko na (Moldova): Ion Sturza. Majina mengine maarufu ni baba wa Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, shemeji wa Rais wa China Xi Jinping, mtoto wa Waziri Mkuu wa Malaysia Najib Razak, watoto watatu wa Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif, Clive Khulubuse Zuma mpwa wa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, mtoto wa Katibu Mkuu wa zamani wa UN Kojo Annan, Mark Thatcher mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Waziri Mkuu wa zamani wa Italy Silvio Berlusconi na waigizaji filamu Jack Chan na Amitabh Bachchan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles