NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imelipa hadhi ya mkoa maalumu wa kodi eneo la Kariakoo Dar es Salaam kwa vile ni kitovu cha biashara nchini.
Ikizungumzia mapato ya Agosti 2016, TRA imesema imevuka lengo kwa kukusanya Sh trilioni 1.158 ambako lengo lilikuwa ni trilioni 1.152 ambayo ni asilimia 100.57.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema jana kuwa hiyo imetokana na mikakati endelevu ambayo mamlaka imejiwekea kuhakikisha inakusanya mapato stahiki na kwa wakati.
Alisema makusanyo hayo yametokana na matunda mazuri ya mikakati iliyowekwa na kwamba makusanyo hayo yamevuka lengo ikilinganishwa na yale ya Agosti 2015 ambako zilikusanywa Sh bilioni 923.
Alisema lengo kuu wa mamlaka ni kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na kukusanya mapato kwa ukamilifu kuweza kufikia lengo la mwaka wa fedha wa 2016/17 na kuvuka.
“Sambamba na hayo pia tunaomba wananchi na wafanyabiashara kuendelea kujitokeza kuhakiki taarifa zao za usajili wa namba za utambulisho kabla ya Oktoba 15 mwaka huu katika vituo husika.
Baada ya muda huo kuisha hautaongezwa muda na badala yake hatua hiyo itahamishiwa katika mikoa mingine,” alisema Kayombo.
Kayombo aliwataka wafanyabiashara wa vituo vya mafuta wawe wamefunga mashine za EFDs ifikapo Septemba 30, mwaka huu na kwamba Oktoba mosi itaanza hatua ya ukaguzi kwa vituo vitakavyokuwa vimekaidi ili hatua zichukuliwe dhidi yao.
Alisema katika kuhakikisha VAT inakusanywa kwa wakati, walipa kodi wote waliosajiliwa na VAT wanatakiwa kuwasilisha mrejesho wa hesabu ya biashara zao ya kila mwezi ifikapo tarehe 20 ya kila mwezi badala ya 27 iliyokuwa ikitumika mwaka wa fedha uliopita.