26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kariakoo ilivyofanikiwa kupata uongozi imara, kulipa madeni

 MANENO SELANYIKA

SHIRIKA la Masoko ya Kariakoo (SMK) limeendelea kujidhatiti kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni moja ya jitihada zake za kuwekeza zaidi kibiashara. 

Hetson Msalale Kipsi, ni Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, anasema katika kipindi hiki cha uongozi wa serikali ya awamu ya tano, shirika limefanya mageuzi makubwa ambayo mbali na kuongeza wigo wa mapato pia huduma kwa wananchi zimeboreshwa.

Anafafanua kuwa shirika limekuwa katika mpango mkakati wa kutaka kutekeleza miradi mikubwa ikiwamo kuboresha Jengo la Soko Dogo kwa kujenga jengo la kibiashara kubwa na la kisasa. 

Anasema kuwa mradi huo unakadiriwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni 23.

“Haya ni mafanikio makubwa kwetu kwani tumepanua huduma zetu ili wateja wetu waweze kufanya biashara zao katika mazingira bora zaidi,” anasema. 

Msalale anafafanua kuwa shirika pia lipo katika hatua ya kutekeleza miradi mingine mmoja ukiwa ni ujenzi wa soko jingine katika viwanja vyake vilivyopo eneo la Mbezi Beach, Makonde, Manispaa ya Kinondoni. 

Msalale anasema kuwa mradi huu pia unakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 500 hadi kukamilika kwake. 

Anasema uwekezaji mwingine unakusudiwa kufanywa katika viwanja vya shirika viliyopo Tabata Bima katika Manispaa ya Ilala.

Shirika la Masoko ya Kariakoo, kuanzia bodi ya wakurugenzi, menejimenti na wafanyakazi wake wanatambua na kuthamini mchango mkubwa wa uongozi wa awamu hii ya tano tangu ilipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2015 hadi kufikia sasa katika kulifufua shirika na kulisimamia kwa karibu kiutendaji. 

Hapana shaka kwamba chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, shirika litaendelea kupiga hatua zaidi kiuchumi na kuwa miongoni mwa mashirika ya umma ambayo yataendelea kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Judith Magoto ni mkazi wa Jijila Dar es Salaam, analishauri Shirika la Masoko Kariakoo kuendelea kuboresha huduma zake.

“Waendelee kuboresha huduma zao… waboreshe usafi hayo ndiyo tunayoyataka wateja wa soko hili,” anasema.

Kariakoo ni eneo maarufu la kibiashara si kwa hapa nchini tu, bali kwa eneo zima la Afrika Mashariki na Kati.

Ni katika eneo hilo kuna soko maarufu na kubwa katika nchi yetu soko ambalo limesheneni aina mbalimbali ya bidhaa ambazo pia husafirishwa na kuingizwa sokoni hapo kutoka kona zote za nchi yetu na hata nchi jirani kama vile Zambia na Malawi, ambako baadhi ya mazao yanayozalishwa katika nchi hizo huingizwa katika Soko kuu la Kariakoo. Mfano Karanga kutoka Malawi na matunda aina ya matikiti kutoka Zambia.

Anasema Shirika la Masoko Kariakoo ambalo lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 36 ya Mwaka 1974 limepita katika vipindi mbalimbali vya kimaendeleo pamoja na changamoto. Shirika limekuwa likitekeleza majukumu yake kwa miaka 45 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1974 kisheria. 

Anafafanua kuwa sasa miaka 45 ya kiutekelezaji “Operational period” tangu lilipozinduliwa rasmi na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hapo Desemba 8, mwaka 1975.

Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa Fedha 2015/2016 hadi 2019/2020 Shirika la Masoko ya Kariakoo limefanikiwa kutekeleza yafuatayo:-

Kuongeza mapato ya shirika kutoka Sh 2,114,836,256.00 mwaka 2015/2016 hadi kufikia Sh 3,351,087,049.29 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 63.1 kutokana na kuongeza ufanisi katika usimamizi matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato ya Serikali “Local Government Revenue Collection Information System” (LGRCIS) na kufanikiwa kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya shirika.

Msalale anafafanua kuwa mengine ni kuimarisha usafi wa soko hususani katika uondoshaji taka na mazingira kwa ujumla, hivyo kumefanikiwa kudhibiti magonjwa ya mlipuko kwa muda mrefu na kuepusha athari nyingine zinazotokana na uchafu. 

Aidha, mifumo ya hewa katika eneo la shimoni imeboreshwa na kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara hivyo kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara katika eneo hilo.

“Shirika limegharamia na kufunga mfumo wa CCTV kamera kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa soko kwa ajili ya wafanyabiashara na mali zao pamoja na wateja wanaotembelea soko kwa ajili ya kujipatia mahitaji mbalimbali,” anasema. 

Mafanikio mengine ni kuboresha maeneo ya kufanyia biashara kwa lengo la kuongeza mapato ya shirika kwa kujenga miundombinu mbalimbali.

Anayataja mafanikio mengine ni ujenzi wa maduka 94 kuzunguka jengo la soko kuu, ujenzi wa paa katika eneo la soko la wazi, ujenzi wa maduka 19 katika Mtaa wa Tandamti.

Anasema kuwa kwa idadi ya maduka yaliyoongezeka katika miaka hii mitano ni maduka 113. Ongezeko la maduka hayo limewezesha kuongezeka kwa mapato ya wastani wa Sh 56,500,000.00 kwa mwezi ambayo ni sawa na Sh 678,000,000.00 kwa mwaka.

Mafanikio mengine ni kugharamia maandalizi kuelekea biashara ya saa 24 katika eneo la Kariakoo, ambapo maeneo mbalimbali kuzunguka soko yamefungwa taa na jumla ya CCTV camera 24 kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama.

Shirika limefanikiwa kuboresha mazingira ya watumishi kufanya kazi kwa kuongeza vitendea kazi kama vile kompyuta na samani za maofisini pamoja na kununua gari jipya la shirika.

Meneja Mkuu huyo anasema shirika limefanikiwa kulipa mchango kwa Serikali kuu ambapo katika mwaka wa fedha 2018/2019, Shirika limelipa jumla ya Sh 50,000,000.00.

“Shirika limefanikiwa kuandaa rasimu ya marekebisho ya sheria ya shirika ili kuendana na wakati uliopo ambapo wanahisa wote wawili (Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Msajili wa Hazina) wamekwisha toa maoni yao. Hatua inayofuata ni ya kukusanya maoni ya wadau wengine ili kukamilisha rasimu na kuiwasilisha Ofisi ya Rais –Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa “OR-Tamisemi.” 

Anafafanua kuwa kuhuisha mipaka ya maeneo yanayomilikiwa na shirika kupitia Idara ya Upimaji na Ramani ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kuhakikisha maeneo hayo yanalindwa kwa maslahi ya shirika na kuepuka uvamizi. 

Kurejesha kwenye umiliki wa shirika jengo la ghorofa lililopo katika eneo la Tabata Bima ambalo lilikuwa limeuzwa kwa njia ya mnada wa mahakama. Aidha, shirika limefanikiwa pia kurejesha eneo lake lililovamiwa la Mbezi Beach Makonde (Viwanja Na.2002 hadi 2003) lenye ukubwa wa mita za mraba 6,119.

Anafafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano (2015/2016 hadi 2019/2020) shirika limefanikiwa kutoa nafasi za ajira kwa watumishi/wataalam wapya 45, ambapo kati ya hao, 29 ni waajiriwa wa kudumu na 16 ni watumishi wa mkataba.

Msalale anasema Shirika la Masoko ya Kariakoo katika kipindi hiki Rais Dk. Magufuli amelipatia uongozi kamili kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Namba 36 ya mwaka 1974 iliyoanzisha shirika. 

Anabainisha kuwa amewezesha kuundwa kwa bodi ya wakurugenzi kwa kumteua mwenyekiti wa bodi pia kumteua mtendaji mkuu wa shirika ambaye ni meneja mkuu. 

Ni muhimu kufahamu kwamba Shirika la Masoko ya Kariakoo kuanzia mwaka 1999 hadi Desemba 2015, lilikuwa halina uongozi na utawala unaoelezwa katika sheria yake iliyotumika kuanzisha shirika. 

Kutokana na hali hiyo, shirika lilikosa uongozi kwa mujibu wa sheria. Matokeo ya hali hiyo ilikuwa na madhara kwa shirika ikiwa ni pamoja na kuyumba kiutendaji pamoja na kukwama kwa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Aidha, katika kipindi hicho cha miaka 16 ya kukosekana kwa uongozi sahihi shirika liliingia katika madeni makubwa yakiwamo Payee ,SDL na kodi ya ardhi, yaliyokuwa yanafikia kiasi cha Sh bilioni 1.3. 

Ali Shija, ni mfanyabiashara wa Kariakoo kwa muda mrefu, analipongeza soko hilo kwa kuboresha mazingira.

“Kwa sasa, hali ya usafi na usalama umeimarika na tunaweza kufanya kazi zetu kwa salama zaidi,” anasema.

Anaushauri uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo kuwekeza katika maeneo mengine kando kando ya jiji ili kusogeza huduma zake karibu na wananchi.

Msalale anasema Shirika la Masoko ya Kariakoo katika Kipindi hiki limefanikiwa kuwa na ongezeko la bajeti kwa asilimia 32.4 kutoka Sh bilioni 2.5 kwa mwaka wa fedha 2015/2016 hadi kufikia bilioni 3.7 katika mwaka wa fedha 2019/2020. 

“Ukuaji huu wa bajeti ya shirika umekua kwa wastani wa asilimia 8.1 kila mwaka,” anasema.

Ulipaji Malimbikizo Madeni ya Shirika kwa Serikali Kuu

“Kama ilivyotangulia kudokezwa katika sehemu ya kwanza ya mafanikio kwamba shirika limepata uongozi wenye kutambuliwa kisheria na tatizo la uongozi lililodumu katika kipindi cha miaka 16 na kusababisha shirika kuwa na deni kubwa kiasi cha Sh bilioni 1.3 limepata ufumbuzi,” anasema.

Anafafanua kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2019/2020, Shirika la Masoko ya Kariakoo likiwa chini ya bodi na menejimenti mpya, limefanikiwa kulipa madeni mbalimbali kwa Serikali jumla ya Sh milioni 800 kati ya Sh bilioni 1.3 ambayo shirika lilikuwa linadaiwa. 

Aidha, sambamba na kulipa kiasi hicho cha deni la nyuma, pia limeweza kuwasilisha makato yote stahiki ya kisheria kila mwezi katika mamlaka husika ikiwamo PAYEE katika mamlaka ya Mapato Tanzania yaani TRA. 

 “Haya ni mafanikio makubwa ndani ya shirika chini ya uongozi wa Rais Dk. Magufuli, tangu alipoingia madarakani na kuamua kuweka uongozi madhubuti katika shirika,” anafafanua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles