30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kardinali Pengo ang’atuka, Askofu Ruwa’ichi amrithi

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis ameridhia ombi la Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo kung’atuka madarakani.

Papa Francis amemteua Askofu Mkuu Mwandamizi wa jimbo hilo, Yuda Thaddeus Ruwa’ichi kuchukua nafasi ya Kardinali Pengo.

Taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa Vatican News jana, ilisema; “katika maadhimisho ya sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni, mwili na roho, Agosti 15, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la Kardinali Polycarp Pengo, kung’atuka kutoka madarakani.

“Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Mkuu Mwandamizi, Yuda Thaddeus Ruwa’ichiwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kuanzia sasa kuwa ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.”

Pia taarifa iliyotolewa jana na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), iliyomnukuu Balozi wa Papa Francis nchini, ilikazia taarifa ya Vatican ikisema Ruwa’ichi anachukua rasmi majukumu ya kuliongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Vatican News, ilisema katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 75 ya kuzaliwa kwa Kardinali Pengo, aliwaambia watu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwamba anasubiria wakati wowote kumtii Baba Mtakatifu Francisko atakapomwambia apumzike katika utume wa kiaskofu.

“Anasubiria pia kumtii Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, wakati wowote atakapomwita na kumwambia kupumzika katika usingizi wa amanina maisha ya uzima wa milele,” ilisema taarifa hiyo.

Ilisema pia kuwa Kardinali Pengo alisema kaburi lake liko Pugu, kwenye Kituo cha Hija, mahali ambako wamelala mashuhuda wa imani na uinjilishaji nchini.

Taarifa hiyo ilisema Kardinali Pengo alisema anaamini katika utii, kama alivyoambiwa kwamba baada ya Daraja Takatifu, angeteuliwa kuwa Katibu wa Askofu Jimbo Katoliki la Sumbawanga.

“Baada ya miaka miwili akatumwa kwenda Roma kujiendeleza kwa masomo ya juu katika masuala ya maadili. Aliporejea nchini Tanzania mwaka 1977, akapangiwa kufundisha Seminari Kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo Kuu la Tabora,” inasema taarifa hiyo.

Inaeleza kuwa baadhi ya wanafunzi wake ni Askofu Ruwa’ichi ambaye sasa ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Askofu Almachius Vincent Rweyongeza wa Jimbo Katoliki Kayanga.

Taarifa hiyo inasema mwaka 1978 Kardinali Pengo aliitwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kuambiwa kuwa ameteuliwa kuwa Gombera na mwasisi wa Seminari Kuu ya Segerea, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Ilisema baada ya hapo, Kardinali Pengo aliendelea na huduma nchini katika malezi na majiundo ya majandokasisi hadi mwaka 1984.

“Kardinali Pengo kwa unyenyekevu mkubwa anasema hajawahi kuwa kiongozi seminarini, anakumbuka tu kwamba akiwa Kaengesa alikuwa ni kiranja msaidizi, lakini hajui ni kwa sababu gani ambazo Mwenyezi Mungu amemteua kuwa ni kiongozi wa kanisa, kiasi cha kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama kasisi, askofu na hatimaye kama kardinali,” inasema taarifa hiyo.

Inasema pia Kardinali Pengo anakiri kwamba yeye si mpenzi sana wa michezo, bali anapenda kumwimbia Mungu utenzi wa sifa, shukrani, enzi na utukufu kwa matendo makuu aliyomtendea katika maisha yake, na kupitia kwake na waandamizi wake wote wameweza kufanya yale yaliyofanyika kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu ndani na nje ya Tanzania.

Taarifa hiyo hiyo ilisema Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar (SECAM) itamkumbuka Kardinali Pengo kwa kuwa ni daraja na kiungo muhimu cha Kanisa barani Afrika wakati SECAM ilipokuwa inachechemea kwa changamoto mbalimbali katika maisha na utume wa Kanisa barani humo.

Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5 mwaka 1944 Kijiji cha Mwazye mkoani Rukwa.

Alipewa upadri mwaka 1971 na Askofu Charles Msakila, akasoma teolojia ya maadili huko Roma na kutunukiwa shahada ya udaktari mwaka 1977.

Alianza kufundisha somo la teolojia katika Seminari Kuu ya Kipalapala (Mkoa wa Tabora) na baadaye alichaguliwa kuwa gombera wa Seminari Kuu ya Segerea hadi 1983.

Aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi Nachingwea Novemba 11 mwaka 1983, akapewa daraja takatifu na Papa Yohane Paulo II Januari 6, mwaka 1984.

Oktoba 17, mwaka 1986 alihamishiwa Jimbo Katoliki la Tunduru, Masasi na Januari 22 mwaka 1990 alifanywa kuwa Askofu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na baadaye mwaka 1992, aliteuliwa kuwa askofu mkuu wa jimbo hilo baada ya Kardinali Laurean Rugambwa kujiuzulu wadhifa huo.

Aliteuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Kardinali Februari 21 mwaka 1998, akikabidhiwa kuwa kiongozi wa Parokia ya Nostra Signora de La Salette mjini Roma.

Pamoja na majukumu mbalimbali katika idara za Papa, tangu mwaka 2007 ni Mwenyekiti wa Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Afrika na Madagascar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles