ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi, ilieleza kuwa Kardinali Pengo alifikishwa hospitalini hapo juzi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Profesa Janabi katika taarifa hiyo alieleza kuwa afya ya Kardinali Pengo imeendelea kuimarika ikilinganishwa na siku alipofikishwa hospitalini hapo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kuwa Rais John Magufuli alifika hospitalini hapo kumjulia hali akiwa ameambatana na mkewe, Janeth ambapo alimpa pole na kumuombea afya njema ili aweze kuendelea na shughuli zake za kutoa huduma za kiroho kwa wananchi
Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5 mwaka 1944 katika Kijiji cha Mwazye mkoani Rukwa.
Alipewa upadri mwaka 1971 na Askofu Charles Msakila, akasoma teolojia ya maadili huko Roma na kutunukiwa shahada ya udaktari mwaka 1977.
Alianza kufundisha somo teolojia katika Seminari Kuu ya Kipalapala (Mkoa wa Tabora) na baadaye alichaguliwa kuwa gombera wa Seminari Kuu ya Segerea hadi 1983.
Aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi Nachingwea Novemba 11 mwaka 1983, akapewa daraja takatifu na Papa Yohane Paulo II Januari 6, mwaka 1984.
Oktoba 17, mwaka 1986 alihamishiwa Jimbo Katoliki la Tunduru, Masasi na Januari 22 mwaka 1990 alifanywa kuwa Askofu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na baadaye mwaka 1992, alikuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Laurean Rugambwa alipojiuzulu, aliteuliwa kushika wadhifa huo.
Aliteuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Kardinali Februari 21 mwaka 1998, akikabidhiwa kuwa kiongozi wa Parokia ya Nostra Signora de La Salette mjini Roma.
Pamoja na majukumu mbalimbali katika idara za Papa, tangu mwaka 2007 ni Mwenyekiti wa Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Afrika na Madagascar.