25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

KARDINALI KATOLIKI KUSHTAKIWA KWA ULAWITI

Na Bernard Lagan – Sydney, Australia


KARDINALI George Pell (76) kutoka Australia ambaye aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francis mwaka 2014 kudhibiti na kusimamia uchumi na fedha zote za Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican, atashtakiwa kwa tuhuma za ulawiti na udhalilishaji wa kijinsia.

Kiongozi huyo msomi wa vyuo vikuu maarufu duniani vya Oxford na Cambridge nchini Uingereza, Juni mwaka jana alichukua likizo ya muda kurudi Australia ili kujitetea dhidi ya shutuma hizo.

Jana asubuhi, alifikishwa katika mahakama iliyofurika watu mjini Melbourne, kushuhudia hakimu anatoa kauli gani kuhusu kesi ya awali.

Katika uamuzi wake, hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Belinda Wallington, aliamua kuwa ulikuwapo ushahidi wa kutosha kumshtaki kiongozi huyo wa kanisa.

Kardinali Pell atakuwa kiongozi wa juu wa Kanisa Katoliki katika karne za karibuni, kushtakiwa kwa ulawiti na udhalilishaji wa kijinsia.

Katika uamuzi ambao utaitikisa Vatican na uongozi wa Kanisa Katoliki duniani kote, hakimu Wallington, alikataa jitihada kubwa zisizokuwa za kawaida za mawakili wa Kardinali Pell, baada ya shutumu hizo za awali kutupiliwa mbali.

Kardinali Pell aliyepata kuwa nyota wa mchezo wa mpira wa Australia (Australian Rules Football) wakati akiwa chuo kikuu, na kujulikana kwa jina la Big George, jana hakuonyesha dalili zozote za kushtushwa na uamuzi huo.

Ukiondoa kugeukageuka kwa sekunde chache, kuangalia umati wa watu uliojaa mahakamani hapo kusikiliza uamuzi huo, aliweka mkono wake mdomoni na kukohoa kidogo, lakini hakuonyesha ishara nyingine ya wasiwasi.

Kardinali Pell, atakabiliwa na mashtaka ya ulawiti na udhalilishaji wa kijinsia unaodaiwa kutokea katika miaka ya 1970 wakati alipokuwa bado padre.

Baadaye katika miaka ya 1990, inadaiwa pia alishiriki tena katika vitendo vya namna hiyo alipokuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Melbourne.

Inadaiwa alishiriki katika vitendo hivyo kwa mara ya kwanza alipokuwa padre katika Jimbo Katoliki la Ballarat, mji uliopo maili 70 magharibi mwa Melbourne.

Tume ya Kifalme ya Australia ilivielezea vitendo hivyo mwaka jana kama “Kushindwa kwa hatari kabisa kwa uongozi” katika jitihada za kanisa kukabiliana na vitendo vya ulawiti, mapenzi na udhalilishaji wa kijinsia, hasa dhidi ya watoto wadogo wa kiume.

Baadaye, inadaiwa alishiriki pia vitendo vya namna hiyo mjini Melbourne.

Aliposhauriwa kuhusu utetezi wake baada ya hakimu Wallington kumshauri rasmi kwamba Jaji atakayesikiliza kesi yake angetilia maanani utetezi wake huo wakati wa kutoa hukumu, Kardinali Pell alisema: “Nakana mashtaka yote.”

Wallington alitumia zaidi ya saa nzima kutoka uamuzi wake na uamuzi wa kwanza uliondoa tuhuma kubwa zaidi dhidi ya Kardinali Pell.

Tuhuma hizo ni za kati ya mwaka 1978 na 1979 alipokuwa padre katika Jimbo la Ballarat; ambapo mlalamikaji mmoja tayari ameaga dunia tokea polisi walipomtuhumu kwa mara ya kwanza na mwingine amethibitika hana uwezo wa kiafya wa kutoa ushahidi.

Hakimu Wallington pia alielezea mkanganyiko katika ushahidi wa shahidi wa tatu.

Undani kamili wa shutuma na mashtaka yaliyobakia dhidi ya Kardinali Pell havijawekwa wazi, lakini vyote vinafikiriwa vilitokea miongo kadhaa iliyopita.

Mawakili wa Kardinali Pell wakiongozwa na Robert Richter, QC, walitaka shutuma zote dhidi yake kutupiliwa mbali, wakisisitiza zilikuwa ni za “kutunga” na ni “matokeo ya ndoto tu, matatizo ya kiafya ya akili na utunzi tu wa kusadikika” na kwamba wanaomshutumu walikuwa wanachochewa tu na hamu na mihemko ya kuliadhibu Kanisa Katoliki.

Kardinali Pell aliyewasili mahakamani akiwa kwenye gari ndogo nyeupe aliongozwa na kulindwa na kiasi cha maofisa 40 wa polisi, ambao walihakikisha hafikiwi na wananchi waliokuwa wanasubiri kuingia mahakamani kusikiliza kesi hiyo.

Walikuwapo pia waandamanaji wenye mabango yaliyosema: “Kila mtoto anastahili utoto salama na wenye furaha.”

Chini ya masharti ya dhamana, Kardinali Pell hawezi kuruhusiwa kusafiri nje ya Australia kwa sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles