23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 10, 2022

KARATA ZACHANGWA CHADEMA

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

SIKU chache tangu Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kuwa mjadala baada ya kuangushwa uenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, karata ndani ya chama hicho zinaonekana kuchangwa ipasavyo na sasa Tundu Lissu amegeuka mjadala baada ya kutangazwa kuwa anawania nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Lissu ambaye ni mbunge wa zamani wa Singida Mashariki na mwanasheria mkuu wa chama hicho, hivi karibuni alikuwa jijini Nairobi nchini Kenya na juzi kurudi Ubelgiji, lakini hakusema kama pamoja na mambo mengine alikuja kujaza fomu hizo.

Siri hiyo ilifichuliwa jana jijini Arusha na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye pia alitumia nafasi hiyo kurejesha fomu ya kuwania nafasi yake hiyo kwa muhula mwingine.

Mbowe baada ya kutangaza uamuzi wa Lissu kujaza fomu hiyo, ukumbi uliibuka kwa shangwe, huku akiwatangazia wanachama kuwa kama yupo anayetaka kuwania nafasi hiyo, nafasi ipo wazi.

Baada ya kauli hiyo ya Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, baadhi walisikika wakihoji “kama Lissu ameshachukua utawezaje kupambana naye?”

NAFASI YA DK. MASHINJI SHAKANI

Hata hivyo kitendo cha Lissu kuchukua fomu hiyo, kinaweka shakani nafasi ya Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa ingawa haipo kwenye sheria, ila vyama vingi nchini vimekuwa na utamaduni wa kuweka usawa wa kidini na muungano katika nafasi za juu.

Suala hilo liliibuliwa pia hivi karibuni na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa katika kitabu chake kuhusu maisha yake.

Katika kitabu hicho, Mkapa alisema pamoja na mambo mengine, baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alimuusia kwamba katika kuunda Serikali yake azingatie kuwa Tanzania kuna dini kubwa mbili – Uislamu na Ukristo – na makabila mbalimbali.

Hivyo ni wazi kuwa endapo Mbowe atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa kipindi kijacho na Lissu kuwa makamu wake, nafasi ya mtendaji mkuu wa chama hicho huenda ikachukuliwa na mtu mwenye asili ya Zanzibar.

UENYEKITI WA MBOWE, LISSU

Mbowe alizungumzia suala la Lissu kuwania makamu mwenyekiti jana akiwa jijini Arusha wakati wa mkutano wa sita wa Baraza la Uongozi la Kanda ya Kaskazini, ambako pia alikabidhi fomu yake ya kuwania uenyekiti taifa kwa Katibu wa Chadema Kanda hiyo, Amani Golugwa.

Aliueleza mkutano huo kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Profesa Abdallah Safari ameomba kutokuwania nafasi hiyo kutokana na umri wake na kuwa atabaki kuwa mshauri wa chama.

“Profesa Safari ameomba kwa sababu ya umri wake na tumemkubalia ila ningependa kuwataarifu Watanzania na niseme ukweli baada ya mashauriano tumemwelekeza Tundu Lissu ajaze fomu ya kuwania nafasi hiyo na ameshaijaza ila hatukatazi wengine kugombea.

“Nafasi hizi siyo tu za kufanya majaribio. Uongozi wa chama hiki siyo sumu ambayo unaijaribu kwa kuionja, siamini mimi kama mwenyekiti na nyie kama wanachama eti tuko tayari kuijaribu, kwa sababu utakapotambua ni sumu itakuwa watu wanaimba “parapanda”.

“Kwa hiyo lazima tuwe na wivu mwingi na mapenzi na chama hiki, tuna maadui wengi wasiotutakia mema.

 “Lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitashukuru wale wote waliofikiri na walioona pengine tuendelee kumkabidhi hilo Mbowe.

“Kwa upekee zaidi na kwa unyenyekevu, niwaombe radhi viongozi wangu kutoka jimbo la Hai kwa sababu hawa ndio wamekuwa wahanga wa kwanza, wamenikosa katika utumishi wa jimbo kwa sababu wajibu wa ndani ya chama hiki ni mkubwa.

“Nchi nzima inanihitaji, chama kinanihitaji, wahanga wa kwanza ni familia yangu, wahanga wa pili ni wananchi wangu wa Hai, naomba waendelee kunivumilia, ninapoendelea kuutenda wajibu ambao Watanzania wenzangu wamenipa niubebe.

“Hakika nilikusudia kutokuendelea kuwa kiongozi na  hata wale vijana walipochukua fomu Dar es Salaam, walinitafuta tukurejeshee fomu, lakini nilisita. Na siyo kwa sababu ya woga ila ni kwa sababu niliamini kutoa nafasi kwa wengine kuwa sehemu ya uongozi.

“Uongozi ndugu zangu ni dhamana, yeyote miongoni mwenu au nje anafikiria uongozi wa Chadema ni fursa, hajaelewa maumivu yanayoambatana na uongozi, ni nafasi yenye lawama nyingi, nafasi ambayo ukitekeleza wajibu wako vizuri unakuwa adui wa watu wengi.

“Chama hiki kinawindwa sana, viko vyama vingi vya siasa katika nchi yetu, siyo miujiza Chadema kuwa chama kikuu cha upinzani, ni kwa sababu mimi, wewe, wale na ninyi tuko pamoja, tumefanya kazi ya kuifanya Chadema iwe hivi.

“Kwa hiyo sihitaji sifa wala utukufu wowote kwa nafasi tuliyofika ila wote kwa pamoja tunahitaji kumshukuru Mungu, kwa kutambua mchango wa kila mmoja wetu aliye taifa hadi wanachama wa kawaida, ni lazima tuendelee kupongezana.

“Tuendelee kushirikiana kwani ndoto ya Watanzania imebebwa na Chadema, matamanio ya Watanzania yamebebwa na chama hiki, hayajabebwa na Mbowe na natambua uchaguzi wowote unaambatana na mitifuano,” alisema.

PROPAGANDA MITANDAONI

Katika hatua nyingine, Mbowe alisema propaganda zinazoendelea katika mitandao kuwa hataki wengine wagombee nafasi hiyo ya uenyekiti si za kweli.

 “Hakuna mtu yetote aliyenyimwa kuchukua nafasi katika chama chetu, hizi propaganda kwamba Mbowe hataki watu wawe wenyekiti siyo kweli. Mpaka leo (jana) mliponipa fomu hapa nilishakataa kugombea, sasa namwachia nani chama?

“Wanaopiga kelele kuhusu uongozi wa chama chetu ni watu wa CCM, tunawaambia tangu lini mkatutakia mema ili tupate viongozi wazuri, ili Chadema iwe nzuri zaidi.

“Uongozi wa juu wa chama hiki ndugu zangu siyo mambo ya kuchezeana, ni masuala ya kuaminiana, ni masuala ambayo ni kuliana yamini, jaribu kufikiria mazingira ambayo  kiongozi mkuu wa chama anaunga mkono juhudi,” alisema Mbowe.

VIPAUMBELE VYA MBOWE

Alitaja moja ya kipaumbele chake iwapo atashinda tena nafasi hiyo kuwa ni pamoja na kuboresha nidhamu kutokana na baadhi ya wanachama na viongozi kutumia mitandao kutukana na kudhalilisha wenzao.

“Nimekuwa nasoma mitandao yote, bahati nzuri kama Mwenyekiti wa Taifa, kanda zote nipo, kwa hiyo nasoma, kwa hiyo kila kanda ukiniambia nikupe watu 10 waliokosa nidhamu kuliko wote nitakwambia.

“Kwa hiyo tutumie mitandao na uhuru wako wa kujieleza siyo uhuru wa kutukana wengine, lazima tukomeshe uhuni wa kwenye mitandao, mnatukana familia za watu, wake na watoto, ni kudhalilishana, kwanini tunadhalilishana, tunapata wapi ujasiri wa kukabiliana na adui?

“Ni muhimu kujenga nidhamu kwenye ngazi zote, sisemi watu wawe waoga, watu waifahamu katiba na kuiishi, ukimuona mwenzako ufurahie, bahati mbaya wengine ni viongozi, sisemi tusiwe wakweli, tuwe wakweli lakini tujue ukweii tunaousema tunausemea wapi, kama kuna kiongozi miongoni mwenu ana makosa, hata Mwenyekiti Mbowe ana makosa, kuna vikao vya kumuonya Mbowe.

“Huwezi kwenda kwenye mitandao unampakia Mbowe, unawaambia nini Watanzania wanaosoma na mahasimu wetu unawaambia nini? Tunadhalilishana kwa makabila, imani zetu, historia zetu, tunaanza salamu ninyi wengine wageni siyo wa chama hiki,” alisema Mbowe.

HOJA YA FREDERICK SUMAYE

Akizungumzia hoja ya Frederick Sumaye alisema; “nipende kuwaambia wana Chadema akiwemo Sumaye na mnaowania nafasi, wengine mtakosa kwa sababu ya mitikisiko na ajali za kisiasa, bado tunahitajiana wote katika chama, wako watakaoshindwa.

“Tujiangalie kama chama cha siasa mwaka kesho kinaweza kukamata dola, nimesoma mitandao. Mambo yetu tutayamaliza wenyewe na kwa amani, kila mmoja awe na amani, ajali zinatokea katika siasa, siyo wakati wa kunyoosheana kidole na tunahitajiana wote,” alisema Mbowe.

Katika Uchaguzi wa Kanda ya Pwani uliofanyika mwishoni mwa wiki hii, Sumaye ambaye alikuwa ni mgombea pekee wa nafasi ya uenyekiti wa kanda hiyo, alipata kura za hapana 48 na ndiyo 28.

Hali hii kwa wengi ilifanya waone kwamba Sumaye ambaye tangu ahamie Chadema mwaka 2015 amekumbana na mikasa kama ya kunyang’anywa mashamba yake, aliangushwa kimkakati kutokana na kutaka kuwania uenyekiti taifa.

Ingawa mwenyewe alikiri kuchukua fomu ya uenyekiti taifa, alisema alikuwa hajaijaza na sasa anafikiria kama ataijaza ama ataichana.

Hata hivyo licha ya kusema kuangushwa kwake ni sehemu ya demokrasia, alisema anadhani kuwa aliadhibiwa kutokana na uamuzi wake huo wa kuwania nafasi ya Mbowe.

Kwa maoni yake anaona kutaka kwake kugombea uenyekiti wa Chadema Taifa ambao umeshikiliwa na Mbowe kwa miaka 15, ndiyo sababu ya kuangushwa ama kama mwenyewe anavyosema kuadhibiwa.

Baada ya matokeo, Sumaye alikiri kuwa ameadhibiwa kwa sababu ya kuchukua fomu za kutaka kuwania uenyekiti, ambao kwa baadhi ya wanachama wanaona ni usaliti kwa Mbowe, ambaye amekuwa kwenye kiti hicho tangu  2004.

VIJANA CHADEMA

Awali kabla ya kukabidhi fomu hiyo, Ofisa kutoka Idara ya Uenezi Makao Makuu ya chama hicho, Hemed Ally, alisema wao kama vijana hawajashinikizwa wala hakuna aliyenunuliwa na kushawishiwa kumnunulia Mbowe fomu bali wameamua kufanya hivyo kwa kutambua mchango wake katika masuala ya haki na demokrasia.

“Viongozi mbele yetu tunayo fomu ya Mwenyekiti wa Chama Taifa ambayo ilizungushwa nchi nzima kutafuta wachangiaji wa kumunulia fomu Mwenyekiti Dar es Salaam, lilifanyika tukio moja kubwa la kuhakikisha tunakwenda kumnunulia fomu.

“Lakini tukio linalofuata la kumkabidhi fomu hiyo ikiwa imejazwa yeye kazi yake ni moja tu kuisaini na kukabidhi kwa sababu shughuli zote hatukutaka mwenyekiti azifanye.

“Jambo moja la msingi ni kwanini sisi vijana sambamba na kina mama na wazee tunahitaji Mwenyekiti wetu asifanye shughuli hizi, yeye afanye jambo moja kubwa la kukubali kutupa ridhaa yake ya kuendelea kutuongoza,  amekitendea haki chama hiki tangu alipokabidhiwa.

 “Tunafanya tukiwa tunajiamini, tuna shauku kubwa ya kutaka ridhaa yake ya kuendelea kutuongoza, tunafanya tukiwa na akili timamu kabisa, hakuna mtu aliyeshinikizwa, hakuna aliyenunuliwa wala aliyeshawishiwa kinyume na utaratibu wa kawaida, tuna imani na kazi yake kubwa aliyoifanya,” alisema Ally.

KAULI YA GOLUGWA KWA MBOWE

Naye Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alimtaka mwenyekiti huyo anayetetea nafasi yake kutokuyumbishwa na kelele zinazoendelea na kuwa wanampenda.

“Kwenye mkutano huu natamani wana-Chadema wenzangu mbali na tukio la uchaguzi tutoke tukiwa na ari ya ajabu ari ambayo wapinzani wetu watashangaa tumekula nini au nini kimetutokea. Tumepigwa sana, tumeonewa sana na wakati mwingine tunahisi tumedhalilishwa sana, lakini ni wakati wa kurudisha utukufu wa Mungu kwa kufanya siasa za kiharakati kimkakati,” alisema.

mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,395FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles