Na Mwandishi Wetu, Manyoni
Kamishina wa Uhifadhi wa Wanyamapori (TAWA), Mabula Nyanda, ameridhishwa na ubora wa ujenzi wa karakana ya matengenezo ya magari na mitambo iliyojengwa Kanda ya Kati ya TAWA wilayani Manyoni.
Akiwa katika ziara yake Makao Makuu ya Kanda ya Kati, Januari 14, 2024 alikagua ujenzi huo uliogharimu zaidi ya sh million 217.
“Nimetembelea na kukagua karakana, kimsingi nimeona imejengwa vizuri na pia nimeona ina uwekezaji mkubwa wa vifaa vitavyotumika na nina imani hii karakana itatusaidia sana,” amesema Nyanda .
Akibainisha sababu za kuifanya karakana hiyo kuwa kubwa wilayani humo, amesema Manyoni ni katikati ya nchi na ni sehemu inayofikika kwa urahisi, hivyo kutokana na ukubwa wake itatumika kutengeneza magari ya taasisi nzima.
Aidha, ameelekeza uongozi wa Kanda hiyo kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa karakana ikiwa ni pamoja na kuwapeleka wataalamu wa vifaa hivyo ili iweze kusimamiwa na kuendeshwa kisasa.
Pia ametumia ziara hiyo kuwahimiza maafisa na askari wote wa TAWA kurejea mpango mkakati wa taasisi hiyo ambao unafikia kikomo 2026 ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kamishna huyo amesisitiza kuwa malengo hayataweza kutimia bila kuishi katika tunu za taasisi hiyo ambazo ni uadilifu, kufanya kazi kwa ushirikiano, ubunifu, juhudi na maarifa.
Naye Kamishna Msaidizi Ulinzi wa Rasilimali za Wanyamapori, Hadija Malongo akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa Kanda ameishukuru Serikali kupitia TAWA kwa kuwezesha ujenzi wa karakana hiyo ambayo kukamilika kwake kutasaidia kupunguza gharama za matengenezo ya magari ambayo ilikuwa changamoto kubwa