27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

KANUNI 10 ZA KUWA NA AMANI

Na Dk. Chris Mauki,

WENGI wetu tunaishi katika mazingira ambayo yanaathiri sana amani yetu ya moyoni. Yamkini tunaonekana tuna furaha, tunacheka tunahusiana vema na wanaotuzunguka lakini ukweli ni kwamba ndani yetu hatuko sawa.

Wengi tunawaona wana maisha mazuri sana kwa jinsi ya nje, wana majumba mazuri ya kuishi, wana magari mazuri ya kutembelea, watoto wazuri na kazi nzuri pia na tukiwaangalia tunadhani wana furaha ndani yao lakini nimepata bahati ya kuzungumza na wengi wa aina hii na kugundua  kuwa hawakuwa na furaha ya maisha yao kama wengine walivyofikiri.

Viko vitu vingi vinavyoweza kuiathiri amani ya moyoni mwako, kwa mfano; hali mbaya ya mahusiano baina yako na umpendaye, matatizo ya tabia za watoto wako, matatizo ya kazini kwako, kushindwa kufikia malengo binafsi, historia yako binafsi, maumivu ya moyo, mambo ya ndugu na mengine mengi.

Dhumuni langu katika makala hii ni kujaribu kuzibua kanuni chache za kusaidia kuishughulikia hali hii ili uweze kupona katika tatizo hilo.

Jitahidi kutokuingilia mambo ya wengine, labda tu uruhusiwe na mhusika

Wengi tumejikuta katika matatizo sababu tu ya kuingilia mambo yasiyokuwa yetu, tunafanya hivyo sababu mara nyingine tunafikiri tunavyojua sisi ndio sawa na  mtazamo wetu ndio uko sahihi zaidi na yeyote asiyeafikiana na mtazamo wetu anastahili kupingwa. Lazima tutambue kwamba Mungu amemuumba kila mmoja wetu tofauti.  Hakuna watu wawili watakaowaza au kutenda sawasawa. Jali yaliyo yako kwanza na utailinda amani ya moyo wako (mind your own business).

Jifunze kusamehe na kusahau

Hii ni nguzo na msaada mkubwa katika kutafuta amani ya moyoni.  Mara nyingi tunaweka hisia za maumivu moyoni dhidi ya mtu aliyetuumiza au kutuudhi, taratibu tunaumba na kulea chuki kali moyoni.  Matokeo yake wengine wanakosa usingizi, wanapata vidonda vya tumbo, wengine shinikizo la damu (BP) n.k. Chuki au maumivu haya ya moyo yalifanywa mara moja, lakini matokeo yake yanaeendelea kuharibu maisha na afya kwa muda mrefu kwa sababu tu ya wewe kuikumbuka chuki au uchungu. Achana na tabia hii mbaya. Maisha ni mafupi sana hustahili kuyaweka katika matatizo yote haya. Samehe, sahau na tembea mbele. Upendo wakati wote huchanua katika tendo la kutoa na kusamehe (love flourishes in giving and forgiving)

Kamwe usijitutumue kutafuta umaarufu, kujulikana au kutambulika

Fahamu kuwa ulimwengu huu una wabinafsi wengi sana, mara chache  watakusifia pasipo kuwa na wivu.  Wanaweza kukusifia leo kwa sababu una nafasi au uwezo fulani, lakini subiri utakaposhuka chini. Watasahau kabisa yote mema uliyofanya na kuanza kutafuta kila chafu na ovu ulilotenda, hata kama lilitendeka mafichoni. Kwanini unataka kujiua ukitafuta kutambulika na kukubalika.  Kwamwe kukubali kwao hakulingani na kero zao. Kero zao zinazidi sana. Jitahidi kufanya majukumu yako kwa nidhamu ya hali ya juu na moyo wote, ukimwogopa na kumheshimu Mungu na si mwanadamu.

Usiwe na wivu

Wote tunajua jinsi wivu unavyoweza kusumbua amani yetu ya moyoni.  Unajua kabisa kuwa unafanya kazi zaidi ya wenzako ofisini lakini wao wanapata kupandishwa cheo au faida nyingine za kikazi na si wewe.

Wewe umeanza biashara miaka  tele iliyopita, lakini haujafanikiwa kama jirani yako ambaye ana mwaka tu katika biashara. Iko mifano tele kama hii katika maisha ya kila siku. Je ndio inakufanya uwe na wivu? Hapana,  kumbuka kuwa kila maisha ya mtu hutegemezwa na mustakabali wake utakavyokuwa, ambao ndivyo unavyompeleka yeye hivyo alivyo.  Kama umepangiwa kufikia hatua fulani hakuna atakayeweza kusimamisha. Kama hujapangiwa hivyo, hakuna atakayeweza kukusaidia kufikia pale pasipo pako. Hakuna utakachokipata kwa kulaumu wengine kwa bahati zako mbaya.  Wivu hautokupeleka kokote, zaidi utakuondolea amani moyoni mwako.

Itaendelea wiki ijayo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles