MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
KANISA Katoliki limetoa tamko juu ya mauaji ya watoto ambayo kwa siku za karibuni yameripotiwa kutokea kwenye mikoa ya Njombe na Simuyu huku yakihusishwa na imani za kishirikina.
Katika Mkoa wa Njombe, watoto 10 wameripotiwa kuuawa wakiwamo watatu wa familia moja, huku baadhi ya miili ikikutwa ikiwa imenyofolewa viungo kama sehemu za siri na masikio.
Mkoani Simiyu nako kuliripotiwa kutokea matukio matatu, huku baadhi ya miili ya watoto waliouawa ilikutwa haina baadhi ya viungo kama sehemu za siri, mikono, miguu na nywele.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Flavian Kassala, alisema kanisa hilo linaguswa kwa uchungu mkubwa ndoto za watoto wasio na hatia kukatishwa.
“Baraza linalaani vitendo hivyo vya mauaji na kwa namna ya pekee linaguswa kwa uchungu mkubwa pale ambapo tumeshuhudia watoto wanakatiliwa ndoto zao, wanakatishwa maisha yao kwa sababu ambazo hazina maana yoyote.
“Kanisa limeendelea kulaani mauaji hayo, tumekuwa tukishuhudia wimbi la mauaji ya albino kwa sababu mbalimbali na hasa za kishirikina, iwe kwa sababu yoyote ile na sasa tumesikia tena mauaji ya watoto wasio na hatia na nyuma yake kuna harufu kwamba ni imani hizo hizo za kishirikina.
“Iwe kwa sababu yoyote ile kanisa linasema kwanza maisha ya binadamu ni zawadi kutoka kwa Mungu na Mungu pekee ana haki na zawadi hiyo.
“Lakini mbaya zaidi pale ambapo tunaanza kuwashambulia watoto kwa sababu ya udhaifu wao, mauaji haya tunayalaani kwa nguvu zote na kwa mamlaka yote kanisa linatoa pole kwa jamii nzima ya Njombe, kwa wazazi waliopoteza watoto wao.
“Lakini tunazidi kumwomba Mwenyezi Mungu alegeze mioyo ya hao ambao wameendelea kutumia imani za kishirikina katika kuharibu amani ya jamii na sasa imefikia hatua watoto wetu wanauawa bila sababu,” alisema askofu huyo.
ALICHOSEMA LUGOLA
Kufuatia mauaji hayo ya watoto mkoani Njombe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alitaka kutohusishwa na itikadi za kidini, kisiasa na masuala ya biashara.
Lugola alisema hayo wakati akitoa kauli za mawaziri bungeni baada ya suala hilo kutikisa Bunge na Serikali kutakiwa kutoa taarifa juu ya hali hiyo.
Mbali na kusema hayo, Waziri Lugola alikemea vitendo vya kusambaza taarifa za mauaji hayo mitandaoni akisema watafikishwa mahakamani.
Lugola alisema watoto saba wenye umri chini ya miaka 16, waliripotiwa kuuawa, mtu mmoja kujeruhiwa na wawili kupotea na baadaye kuonekana.
“Nashauri tutulie wakati Serikali kupitia wizara yangu tunaendelea kufuatilia na kudhibiti hali hiii,” alisema.
Alisema uchunguzi unaonesha kwamba mauaji yamefanyika kwa unyongaji.
Wakati mkutano huo wa Bunge la Januari ukiendelea, Lugola alisema pia vyombo vya usalama vimeshawabaini watu wanaodaiwa kutekeleza mauaji ya kikatili ya watoto hao 10 na kwamba taarifa za awali zinaonesha matukio hayo ni ya kishirikina.
Lugola alitoa kauli hiyo bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mufindi Kusini, Menrad Kigola (CCM), aliyetaka kupata kauli rasmi ya Serikali kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa baada ya kuibuka taharuki kutokana na mauaji hayo.
Akijibu swali hilo, Lugola alisema tayari wameishabaini waliohusika.
“Tayari tumeshawabaini watu wanaotuhumiwa kutekeleza mauaji hayo kutokana na imani za kishirikina na naibu waziri wangu (Hamad Yusufu Masauni) yuko huko akiendelea kuchukua hatua,” alisema.
JENERALI MABEYO
Naye Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo alienda mkoani Njombe kutokana na mauaji hayo na kusema watayakomesha.
Alisema sasa jeshi linataka kuzitoa imani potofu kwa wananchi na kuwataka kuendelea na shughuli zao za kawaida.
“Tutakomesha mauaji haya nchi nzima si Njombe peke yake, tunawaomba watu waendelee na kazi zao kama kawaida, vyombo vya usalama viko tayari kufanya kazi mchana na usiku,” alisema.
MATUKIO YA SIMIYU
Tukio la kwanza lililotokea Oktoba 10, mwaka jana wakati mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Mwabasabi, Susana Shija (9) katika Kijij cha Lamadi, alipokutwa amekufa na mwili wake kutupwa kwenye jumba chakavu huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimeondolewa.
Mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa ukiwa hauna baadhi ya viungo vyake zikiwemo sehemu zake za siri, mikono yake yote miwili, miguu yote miwili na kuondolewa kwa nywele zake zote za kichwani.
Mama mzazi wa marehemu, Dina Halili, akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio, alisema mtoto wake alitoweka nyumbani katika mazigira ya kutatanisha na akatoa taarifa Kituo cha Polisi Lamadi.
Katika tukio la pili, mtoto wa kike, Milembe Maduhu (12), mwanafunzi wa darasa la saba, naye alikutwa akiwa ameuawa ndani ya jengo linaloendelea na ujenzi maeneo ya Lamadi Desemba 13, mwaka jana.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Deusdedit Nsimeki, mwanafunzi huyo alikuwa akisoma shule moja wilayani Bunda (hakuitaja jina) na alipotea siku kadhaa akiwa anauza vitumbua mjini Lamadi, kabla ya mwili wake kupatikana katika jumba hilo.