Felix Mwagara-Mwibara
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amepiga marufuku makamanda wa polisi wa mikoa nchini kuyazuia kusafiri usiku mabasi yanayotoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda Dar es Salaam au kurudi kwa kisingizio cha kuhofia kuvamiwa na majambazi.
Lugola alisema Jeshi la Polisi lipo imara na kamwe haliwezi kucheka na majambazi wala kuwaonea huruma na kuanza kuwapangia muda gani mabasi yasafiri na yasisafiri.
Alisema mabasi hayo yanapaswa kusafiri saa 24.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Kijiji cha Namibu, Kata ya Neruma, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Lugola alisema mabasi yanayosafiri kutoka Kanda ya Ziwa kwenda Dar es Salaam yasizuiwe Morogoro na yanayotoka Dar es Salaam kwenda Kanda ya Ziwa yasizuiwe Shinyanga kwa sababu zinazodaiwa za kiusalama.
“Mimi ndiyo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, hatuwezi kupangiwa ratiba ya kusafiri na majambazi, Serikali ya Rais (John) Magufuli ipo imara, na polisi ipo imara, hivyo agizo hili ambalo pia niliwahi kulitoa lizingatiwe ipasavyo, niliagiza majambazi wote wasambaratishwe, asakwe mpaka jambazi wa mwisho, akamatwe kama kuku.
“Taarifa ya uhalifu zinaonyesha Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa ya kupambana na uhalifu na hasa uhalifu wa majambazi, niliwahi kuagiza kipindi hiki si cha kuwa na huruma na majambazi, ni kipindi cha kuwashughulikia ili wananchi waishi kwa amani,” alisema Lugola.
Alisema nchi haiwezi kupangiwa na majambazi muda wa kufanya biashara na kusafiri, hivyo maelekezo aliyoyatoa kwa polisi ni kupambana na majambazi popote walipo nchini.
“Nimeelekeza magari yanayosafiri yasizuiwe Morogoro yanapopita muda wa usiku, saa nne usiku na kuendelea, yasizuiwe Shinyanga, ili majambzi wajue popote walipo (polisi) wapo imara.
“(Polisi) wamejipanga vizuri na mimi waziri wao nipo imara kuhakikisha Jeshi la Polisi linawashughulikia majambazi mmoja baada ya mwingine ili kuwafanya wananchi katika nchi yao waendelee kushughulika na masuala ya kujijengea uchumi ili Serikali ya Rais Magufuli, iweze kuwa na uchumi wa kati na majambazi wote wakamatwe kama kuku,” alisema Lugola.
Julai 17, 2018, Lugola, alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kuhakikisha biashara zinafanyika kwa saa 24 ikiwamo mabasi kusafiri muda wote.
Akiwa katika ziara Makao Makuu ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kilichopo Ukonga, Dar es Salaam, Kangi alimpa siku 14 IGP Sirro akimtaka amweleze mikakati ya kuwawezesha Watanzania kufanya kazi saa 24 na mabasi kutembea nyakati za usiku.
“Tunataka Watanzania wafanye kazi za kiuchumi kwa saa 24. Hatuwezi tukafikia malengo ya uchumi wa kati kama Watanzania hawafanyi shughuli za kiuchumi.
“IGP aje aniambie mabasi kutotembea usiku ni kwa sababu Jeshi la Polisi limenyoosha mikono kwa majambazi, biashara mbalimbali ikifika saa 12 watu wanafunga wanakwenda majumbani ukiwauliza wanasema ni kwa sababu za usalama, hatuwezi tukakubali kupewa amri na majambazi ni masaa mangapi tufanye shughuli za kiuchumi.
“Hatuwezi kuamriwa na majambazi ni maeneo gani twende na maeneo gani tusiende,” alisema Lugola.