MBUNGE wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) ambaye amekuwa akiwachachafya mawaziri mbalimbali bungeni kutokana na utendaji kazi wao, juzi
‘alijisalimisha’kwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe baada ya kummwagia sifa nyingi kuwa ni mtendaji bora tofauti na wanasiasa wanavyomfikiria.
Lugola alitoa kauli hiyo katika Kijiji cha Mwamagunga wilayani Bunda ambako alisema hivi sasa Waziri Maghembe amekuwa na kasi ya ajabu ya utendaji kazi tofauti na wanasiasa wanavyomfikiria.
“Hivi sasa una kazi ya ajabu ya uchapaji kazi, nakuamini unafanya kazi nzuri ambayo unapaswa kuungwa mkono kuanzia hapa mpaka bungeni,
“Pamoja na pongezi hizi, Waziri Maghembe nakushukuru kutekeleza mradi wa maji wa kijiji hiki,kina mama walikuwa wanateseka mno wanatoka saa 9.00 usiku kwenda kutafuta maji,tatizo hili sasa limekwisha,”alisema Lugola.
Alisema mafanikio hayo yanatokana na kazi nzuri ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo inajawali watu wake.
Kauli hiyo ya Lugola imetafsiriwa na wachambuzi wa mambo kwamba ni sawa na kujisalimisha kwa Waziri Maghembe ambaye katika kikao cha Bunge Februari mwaka huu mjini Dodoma, alimtuhumu kwamba amekuwa akipeleka miradi mingi ya maji jimboni kwake na kubagua mikoa mingine.
“Katika jimbo langu, wananchi tayari wameibua miradi ya maji,lakini utekelezaji wake umekwama lakini bado wameendelea kuikumbatia CCM wakiamini miradi hiyo itamalizika,” alisema.
Akijibu tuhuma hizo, Profesa Maghembe alimshangaa Lugola kwa kutoa shutuma dhidi ya wizara yake wakati Mwibara limepatiwa miradi minne ya maji iliyokamilika huku mitano ikiwa imekamilika kwa asilimia 50.
Waziri Maghembe alisema juzi kuwa siku zote Lugola anaposimamia jambo amekuwa mfuatiliaji mkubwa kuona ombi lake linashughulikiwa.
“Kangi akifuatilia ni balaa, pale bungeni Dodoma utasikia anapiga kelele sana, lakini ofisini pale wizarani ndiyo usiseme anakuja kila wakati bila kuchoka,”alisema Waziri Maghembe.
Waziri aliwataka wakazi wa vijiji vya Kilamanka na Mwamagunga kutunza miundombinu ili waendelee kupata maji kwa uhakika na kwamba hana tatizo na mtu.