31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

KANGI AWAKINGIA KIFUA POLISI MAUAJI YA RAIA


Na ESTHER MBUSSI-DODOMA

Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema anashangaa kwa nini wananchi huchukua hatua ya kuchoma kituo cha polisi   inapodaiwa kuna mtuhumiwa amefia kituoni hapo lakini hawachomi kitanda mtu anapofariki dunia akifanya mapenzi.

Kangi aliyasema hayo bungeni  Dodoma jana alipojibu swali la nyongeza za Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF), aliyetaka kujua kauli ya waziri kutokana na hatua ya watu kufia mahabusu wakidaiwa kuteswa na polisi.

“Katika siku za karibuni zimejitokeza tabia mbaya na ovu za wananchi kufia kwenye vituo vya polisi mahabusu wanapokuwa wanashikiliwa wanapata mateso ambayo husababisha vifo vyao.

“Na hivi karibuni kuna baadhi ya jamii zimekataa maiti kwenda kuzizika kutokana na kufia ndani ya vituo vya polisi, mheshimiwa waziri unatoa kauli gani kali kukemea hatua hii ambayo inatia aibu nchi yetu ambayo ni ya haki na demokrasia?” alisema Khatibu.

Akijibu swali hilo, Lugola alisema mwananchi kufa anakufa wakati wowote, mahali popote na ndiyo maana sijui kwenye Kuran, kwenye Biblia Mhubiri 9:12 ni kwamba… ‘kifo ni mtego, kifo humnasa mtu wakati wowote mahali popote’.

“Kwa hiyo mwananchi anaweza akafa akiwa polisi, akiwa anafanya mapenzi, akiwa kwenye gari anasafiri anaweza akafia hata humu ndani ya Bunge.

“Kwa hiyo isije ikachukuliwa kwamba aliyefia kituo cha polisi ni kwamba ameteswa, lakini ninakiri kwamba kumekuwa na matukio ambayo wananchi wanafia mikononi mwa polisi huwa tunafanya uchunguzi na pale ambako matukio hayo yanajitokeza tumekuwa tukifanya uchunguzi na  inaponbainika kwamba polisi wamehusika.

“…tumekuwa tukichukua hatua na ndiyo maana tunazuia wananchi wasichukue sheria mikononi kwa kuanza kuvamia vituo kwa sababu mtu amefia mikononi mwa polisi na ndiyo sababu na ndiyo maana nimekuwa nikihoji huyo anayekufa akifanya mapenzi mbona hawaendi kuchoma kitanda na nyumba kwa sababu amefia mikononi mwa kitanda,” alisema Lugola.

Katika swali lake la msingi Mbunge wa Shaurimoyo (CCM), Mattar Ali Salum, alitaka kujua ni sheria gani inayotumika kuwaweka mahabusu saa 24 kabla ya kufikishwa mahakamani.

Wakati huo huo, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema),  alitaka tamko la serikali kuhusu suala hilo la kuwekwa mahabusu  zaidi ya saa 24 bila kuwapeleka mahakamani na kuwataka mawaziri kuwa na majibu sahihi na kutoa tamko juu ya hilo.

“Mawaziri wetu wanapokuja kutoa majibu hapa wajue Watanzania wanawaangalia na wanasikitika   wanapokuwa wanatoa taarifa si za kweli.

“Kwa mfano juzi amekamatwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja anaitwa Tanzania Omutima kwa tuhuma tu… amekaa siku nne ndani hajafikishwa mahakamani, amekamatwa kijana mmoja anaitwa Mdude Nyagali amewekwa ndani zaidi ya siku 30.,” alisema Heche.

Akijibu,   Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema anapingana na kauli ya Heche kwamba mawaziri wanatoa majibu ambayo si sahihi.

Alisema  ukweli ni kwamba majibu wanayotoa ni sahihi na wamekwisha kuyafanyia utafiti wa kina na wanajiamini wanachokizungumza ni sahihi kwa kiwango kikubwa.

“Lakini anataka tutuoe tamko, matamko tumekuwa tukitoa kila siku na si lazima tutoe matamko kwa sababu sheria zinajulikana kwamba sisi tunachokifanya ni kusimamia sheria ambazo tumezitunga humu ndani.

“Tunasema kila siku kwamba askari yeyote anayetumia nafasi yake vibaya kinyume na maadili yake ya kazi achukuliwe hatua na tumekuwa tukifanya hivyo,” alisema.

Hata hivyo, Lugola aliingilia kati na kusema kuwa swali la Heche linatoa fursa ya kuelimisha kidogo dhana  hiyo ya kukaa mahabusu saa 24.

Alisema kwenye sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, kwa mara ya kwanza mtuhumiwa na kuwekwa mahabusu kwa maana ya matakwa ya saa 24.

“… yale yanaendana na upelelezi wa awali ambao kuna mazingira ambayo uliyemuweka ndani hata kabla ya saa 24 hazijafika mtamtoa ndani katika upelelezi ama kuna mahala anaenda kuonyesha silaha au ushaidi fulani kulingana na maelezo yake,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Naiomba serikali iweke mfumo ambao popote pale ambapo polisi wanashutumiwa kuhusika na kifo cha raia, uchunguzi ufanywe na jopo la wanasheria na wananchi wengine ambao hawako upande wa polisi na sio vingozi serikalini. Bila hivyo, itakuwa ni vigumu sana wananchi wa kawaida kuamini kwamba haki imetendeka pale ambapo polisi “wamejichunguza” wenyewe.

Comments are closed.

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles