24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, October 6, 2022

KANGI ATAKA MABASI YASAFIRI USIKU

Na NORA DAMIAN,DAR ES SALAAM


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amempa maagizo mazito Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, safari hii akihoji kwanini mabasi hayatembei usiku huku biashara mbalimbali zinafungwa saa 12 jioni.

Mwanzoni mwa mwezi huu, IGP Sirro alipewa maagizo mengine na waziri huyo ya kupambana na ajali za barabarani.

Lakini safari hii waziri huyo alifanya ziara katika Makao Makuu ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kilichopo Ukonga na kumpa siku 14 IGP Sirro akimtaka amweleze mikakati ya kuwawezesha Watanzania kufanya kazi saa 24 na mabasi kutembea nyakati za usiku.

“Tunataka Watanzania wafanye kazi za kiuchumi kwa saa 24. Hatuwezi tukafikia malengo ya uchumi wa kati kama Watanzania hawafanyi shughuli za kiuchumi.

“IGP aje aniambie mabasi kutotembea usiku ni kwa sababu Jeshi la Polisi limenyoosha mikono kwa majambazi, biashara mbalimbali ikifika saa 12 watu wanafunga wanakwenda majumbani ukiwauliza wanasema ni kwa sababu za usalama, hatuwezi tukakubali kupewa amri na majambazi ni masaa mangapi tufanye shughuli za kiuchumi.

“Hatuwezi kuamriwa na majambazi ni maeneo gani twende na maeneo gani tusiende,” alisema Lugola.

MAAGIZO MENGINE

Tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni, waziri huyo amekuwa akitembelea idara mbalimbali zilizo chini ya wizara yake na kutoa maagizo kwa watendaji husika.

Wiki iliyopita waziri huyo alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa wapo wanaomwona kuwa chakaramu na kubainisha kuwa atahakikisha anawakimbiza watendaji wa idara za wizara hiyo ili kutenda kazi zao kwa ufanisi.

Julai 6 alivunja Baraza la Taifa na Usalama Barabarani na kamati za ngazi ya mikoa na wilaya kisha kumwagiza IGP Sirro kufungia leseni za madereva ambao wameonywa zaidi ya mara tatu.

Pia alimwagiza Kamanda Sirro kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa na askari wazembe wa mikoa 10 ya kipolisi inayoongoza kwa ajali za barabarani.

Julai 12 waziri huyo alitembelea Idara ya Uhamiaji na kuzungumza na watendaji wakuu wa idara hiyo huku akiwataka askari wa uhamiaji waliopo mipakani kujitafakari kwa maelezo kuwa utendaji wao hauridhishi.

WAKATI WA KUAPISHWA

Miongoni mwa maagizo aliyopewa na Rais Dk. John Magufuli baada ya kuapishwa ni kuwachukulia hatua Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo kutokana na kukithiri kwa matukio ya ajali za barabarani.

Pia aliagizwa kushughulikia mkataba wa uwekaji mashine za utambuzi wa alama za vidole katika vituo 108 vya polisi kati ya jeshi hilo na Kampuni ya Lugumi wenye thamani ya Sh bilioni 37, mkataba wa uuzwaji magari 777 ya Jeshi la Polisi, sare hewa za polisi, asasi zisizo za kiserikali ambazo zinafanya mambo ya ovyo na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Maagizo mengine ni ya kupandishwa vyeo kwa askari wa chini, vibali vya kufanyia kazi, wakimbizi, wafungwa kutumikishwa kazi na kuviangalia vyombo atakavyokwenda kuviongoza kama Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambalo lina upungufu wa magari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,859FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles