30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kangi ashangaa waliofutiwa kesi kurudishwa polisi

Na Mwandishi Wetu-Dar-es-salaam

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameishangaa mahakama kwa kufuta kesi za watuhumiwa na kuwarudisha katika vituo vya polisi. 

Lugola alipatwa na mshangao huo katika ziara ya kushtukiza Kituo cha Polisi Gogoni, Wilaya ya Kipolisi ya Kimara eneo la Kibamba, Dar es Salaam jana baada ya kupata taarifa ya watuhumiwa kuwekwa rumande muda mrefu.

“Nimefanya ziara katika kituo hiki, ni kweli nimekutana na mahabusu, wapo mahabusu 32 jumla yao. Lakini pia nimekutana na mahabusu 11 kwenye kituo hiki cha polisi cha Gogoni.

“Watuhumiwa hao 11 wanahusika na kesi za mauaji, lakini nilivyowahoji wengine wamekaa magereza kwa miaka saba. Sasa mahakama imewarudisha kwenye vituo vya polisi kwa kufuta kesi zao, nimewakuta Gogoni hapa wana miezi sita, mimi kama Waziri wa Mambo ya Ndani hii si sawasawa,” alisema.

Alisema baada ya kuzungumza na uongozi wa polisi wa wilaya na kumweleza ni kwanini mahabusu hao wapo kituoni hapo, ameona zipo changamoto kwa mahakama, Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai ambazo zitatatuliwa na wizara.

Lugola alisema kuna tatizo la mawasiliano ambapo taarifa kama hizo zimekuwa hazifiki wizarani hali inayosababisha mrundikano wa mahabusu.

“Mimi kama waziri, kutokuwa na taarifa ya kuwepo kwa jambo kubwa kama hili la watu wanakaa kwenye vituo vya polisi badala ya mahakama kuwaamuru magereza kwa sababu wamefikishwa mahakamani, ni jambo nimeliona si la kawaida ni jambo jipya,” alisema.

Alisema bado kuna hali ya kutoridhishwa na utoaji wa dhamana kwa watuhumiwa katika Kituo cha Gogoni licha ya yeye kutoa amri ya watuhumiwa kudhaminiwa saa 24 siku zote za wiki.

Akizungumzia tahadhari ya shambulio iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani hivi karibuni, Lugola alisema kwa sasa nchi iko salama na kuwaonya wananchi wanaotumia mitandao ya kijamii kutotisha wengine.

 “Kama kuna mwanachi kupitia mtandao wowote wa kijamii au kupitia mdomo wake au chombo kingine chochote bado anaendelea kuwatisha na kuwatia hofu Watanzania, nimeshaelekeza Jeshi la Polisi watu hao wasakwe popote walipo wakamatwe,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles