23.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 26, 2022

KANGAROO HUYACHANGANYA MAGARI YANAYOJIENDESHA

Na MWANDISHI WETU,

WAKATI wataalamu wanabuni magari yasiyo na dereva waliamini kuwa huenda ikawa ni suluhisho la ajali za barabarani na kuwaondolea watu usumbufu wa kujiendesha, lakini kangaroo wameonekana kuyapa wakati mgumu.

Magari hayo yanaongozwa kwa kutumia kompyuta pekee, huku yakiwa na uwezo mkubwa wa kuepuka au kutosababisha ajali barabarani.

Wanasayansi wa Google wanaosimamia teknolojia hiyo, waliamua kuyabuni wakiamini kwamba madereva wanafanya makosa mengi wawapo barabarani, yakiwamo ya  kizembe ama bahati mbaya.
Wakati teknolojia ya kompyuta ilipogundulika, wanasayansi walisema wamegundua mbinu ya kufuta makosa ya kibinadamu katika shughuli za hesabu.

Waliamini kuwa kila hesabu 500 afanyazo mtu ambaye ni mtaalamu wa fani hiyo, lazima kuwapo na makosa yasiyopungua mawili. Lakini baada ya
kugundua kompyuta, hesabu zimeweza kufanyika bila makosa.

Makosa ya kibinadamu yanayoweza kufanywa na mtu bila kukusudia, ndiyo hayo yanayoaminika kuweza kufanywa na dereva yeyote akiwa barabarani.

Magari yalivyo
Mtaalamu wa kompyuta katika Chuo Kikuu cha Stanford, Profesa Sebastian Thrun, aliyesimamia teknolojia hiyo akisaidiana na Mhandisi wa
Kampuni ya Google, Chris Urmson, alisema teknolojia hiyo itasaidia kuepusha ajali, foleni na pia kupunguza kiwango cha mafuta yanayopotea kutokana na uendeshaji usiofaa.

Mhandisi Urmson anasema magari hayo hayatakuwa na tofauti kwa kiasi kikubwa na mwonekano au miundo ya magari yaliyopo sasa. Kama haitoshi, yana chagua aidha liendeshwe kwa kompyuta ama dereva.

Mwonekano wake
Kimwonekano, magari hayo yanatofautiana na mengine, kwa kuwa na kifaa maalumu juu ambacho kinasaidia mawasiliano na kutambua maeneo.

Kwenye mfumo wa kompyuta zinatumika programu mbalimbali kama 3D, ambayo itasaidia kuliongoza gari kulingana na ramani ya eneo.

Magari haya yanatumia ramani ambayo lazima iingizwe kwenye mfumo wake ili itambue barabara itakazopita hatimaye kufika aneo ambalo mhusika ama wahusika wanataka.

Wasafiri katika mji Mkuu wa Uingereza London, tayari wameanza kuyatumia magari hayo yasiyo na dereva.

Magari hayo ambayo husafiri kwa hadi kasi ya kilomia 16.1 kwa saa, yanaelekezwa na kompyuta.

Hata hivyo, ndani ya gari huwa kuna mtu ambaye hulisimamisha pale inapohitajika.

Magari hayo yanawabeba watu wanne na hayana usukani wala breki. Pia yana kamera ambayo inaweza kuona umbali wa mita 100 na husimama wakati kuna kitu chochote mbele yake.

 Huchanganywa na kangaroo

Hata hivyo, magari ya Volvo yanayojiendesha yenyewe yamekuwa na wakati mgumu kutambua kangaroo wakiwa barabarani.

Magari ya kampuni hiyo ya Sweden ya mwaka 2017 ya S90 na XC90 hutumia teknolojia yake ya kutambua wanyama barabarani.

Lakini jinsi ambavyo kangaroo anavyotembea barabarani ndivyo ambavyo huyachanganya magari hayo.

“Tumegundua kuwa kangaroo akiruka huonekana kana kwamba yuko mbali, wakati anapotua ardhini huonekana akiwa karibu,” Meneja wa kiufundi nchini Australia aliliambia Shirika la ABC.

Kwa mujibu wa halmashauri ya barabara nchini Australia, asilimia 80 ya ajali za magari na wanyama nchini humo uhusisha kangaroo.

Zaidi ya ajali 16,000 za kangaroo kila mwaka, huchangia madai ya mamilioni ya dola kama bima.

Wahandisi walianza kurekodi mienendo ya kangaroo katika eneo litalotambuliwa kuwa lenye ajali nyingi mwaka 2015.

Takwimu hizo zitatumiwa kuunda teknolojia na kamera ambazo zitaweza kulifanya gari kutambua kangaroo na kushika breki ikiwa kuna hatari ya kutokea ajali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,293FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles