23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

KANDA NANE KUMPA USHINDI UHURU KENYATTA?

 

 

NA MARKUS MPANGALA,

JOTO la uchaguzi mkuu nchini Kenya limezidi kupanda ikiwa umebaki mwezi mmoja tu kabla ya kufanya Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge, ugavana, udiwani na wawakilishi wa jinsia. Uchaguzi huo utafanyika Agosti 8, mwaka huu kote nchini Kenya.

Rais Uhuru Kenyatta ni mwanasiasa anayetupiwa jicho la karibu  zaidi kutokana na mikakati yake ya kutetea kiti hicho alichoshinda mwaka 2013.

Timu ya kampeni ya Uhuru Kenyatta imepanga kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwa kuweka mikakati ya maeneo nane yatakayowapatia kura za kutosha na hatimaye kuibuka washindi.

Ili kumshindi Raila Odinga, inamlazimu Uhuru Kenyatta kufanya kazi ya ziada usiku na mchana kuwashawishi wapigakura ili wamrejeshe madarakani.

Chama cja Jubilee kimeweka wazi mikakati ya ushindi kwa kuigawa Kenya katika maeneo 8 ya kupata kura za kutosha. Tofauti na mwaka 2013 ambapo Uhuru na William Ruto walitumia kesi yao waliyofunguliwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kama ajenda ya kupigiwa kura.

Uchaguzi wa mwaka huu hakuna mambo ya kesi za ICC na wagombea hao wa Jubilee wanalazimika kuwa na ajenda mpya itakayowashawishi wapigakura dhidi ya wapinzani wao NASA.

Mgawanyo uliopangwa na chama cha Jubilee umedhamiria kujipatia kura nyingi kutoka kwenye mashina ili kuwaunganisha na kuwaweka karibu wapigakura hadi ngazi za juu.

Maeneo yaliyopangwa ni Magharibi (Western), Nyanza, Bonde la Ufa(Rift Valley), Nairobi, Mashariki (Eastern), Kati (Central), Kaskazini Mashariki (North Eastern) na Pwani (Coast).

KANDA YA MAGHARIBI

Katika ukanda huu kutakuwa na timu ya kampeni ambayo itakuwa inahamasisha wapigakura kuichagua Jubilee. Kanda hiyo itaongozwa na  gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka.

Gavana huyo atashirikiana na wanachama wengine wa Jubilee ambao ni wabunge, Ben Washiali, Mary Emase na Charles Gimose. Wanasiasa hawa wanalo jukumu ya kukiuza chama chao kwa wapigakura ili kiibuke na ushindi. Ndiyo kusema Uhuru Kenyatta na William Ruto wamekabidhi mapambano kwa wabunge wao ambao watafanya kila njia ya kuwanadi wagombea hao wa urais na umakamo.

KANDA YA NYANZA

Katika Ukanda wa Nyanza utaongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha CIC, Charles Nyachae. Huyo ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe na mwenye nguvu katika kabila la Gusii katika kaunti ya Kisii, Simon Nyachae.

Charles Nyachae amekabidhiwa eneo la Nyanza kama kete ya kupata kura za kabila la watu wa Gusii nchini humo. Katika kampeni hizo atasaidiwa na seneta wa Kisii, Chris Obure ambaye pia anawania nafasi hiyo kwa tiketi ya chama cha Jubilee. Wengine watakaomsaidia ni Albert Nyaundi, Joseph Kiangoi, Walter Nyambati, Jimmy Angwenyi na Mathias Robi.

Idadi ya Kaunti katika Kanda ya Nyanza ni 6 ambapo idadi ya kura zitagombaniwa katika maeneo ni kama ifuatavyo: Kaunti ya Siaya (wapigakura 311,919), Kaunti ya Kisumu (wapigakura 385,820), Kaunti ya Homabay (wapigakura 325,826), Kaunti ya Migori (wapigakura 283,862), Kaunti ya Kisii (wapigakura 412, 945) na Kaunti ya Nyamira (wapigakura 219,358).

KANDA YA BONDE LA UFA

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC), eneo la Rift Valley lina wapigakura 3,348,237. Makabila yanayopatikana katika eneo hilo ni Kalenjin, Maasai, Turkana, Kikuyu  na Luhya. Makabila hayo yanafahamika kuwa ndiyo uti wa mgongo wa ushindi wa William Ruto wa Chama cha Jubilee na Raila Odinga wa Chama cha ODM na Muungano wa NASA.

Timu ya Jubilee inayopiga kampeni katika Mkoa wa Rift Valley inaongozwa na Joyce Laboso ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya useneta wa Bomet mkoani humo. Laboso atasaidiwa na  wanasiasa wengine wa Jubilee John Munyes, Soipan Tuya, Joyce Emanikor na Davis Sankok ambao watakuwa na jukumu la kuhakikisha wanakisaidia chama chao kupata kura za kutosha.

Kanda ya Bonde la Ufa inajumuisha Kaunti 14 na mgawanyo wake wa kura ni kama ifuatavyo; Kaunti ya Turkana (wapigakura: 132,885), Kaunti ya West Pokot (wapigakura 120,986), Kaunti ya Samburu (wapigakura 61,114), Kaunti ya Trans Nzoia (wapigakura; 244,640), Kaunti ya Uasin Gishu (wapigakura 330,630), Kaunti ya Elgeyo/Marakwet (wapigakura 134, 568) na Kaunti ya Nandi (wapigakura 263, 264).

Kaunti nyingine ni Baringo (wapigakura 173,653), Laikipia (wapigakura 173, 905), Nakuru (wapigakura  695,318), Narok (wapigakura 211,835), Kajiado (wapigakura 304,346), Kericho (wapigakura 248,735) na Bomet (wapigakura 252,358).

KANDA YA NAIROBI

Seneta wa Jiji la Nairobi, Mike Sonko ambaye anatetea nafasi yake kupitia Chama cha Jubilee, ataongoza timu ya kampeni ya chama hicho kuhakikisha kinapata kura za kutosha katika Jiji la Nairobi ambalo ndilo makao makuu ya nchi hiyo.

Sonko atasaidiwa na wanasiasa wengine wa Jubilee jijini humo kama vile mgombea wa useneta, Johnson Sakaja, Beatrice Elachi (mgombea wa useneta na ubunge), Rachel Shebesh (mgombea nafasi ya uwakilishi wa wanawake) na Maina Kamanda (mbunge wa Starehe).

Wote hao watalazimika kupambana na NASA ili kukipatia ushindi chama chao cha Jubilee. Jiji la Nairobi lina jumla ya wapigakura halali  2,304,386.

KANDA YA KENYA KATI

Katika kanda hii mchuano utakuwa mkubwa, lakini Jubilee kimepanga vema safu yake. Jubilee kimewapatia jukumu la kusaka kura wanasiasa Kembi Gitura, Sabina Chege, Esther Murugi, Njogu Barua na Alice Ng'ang'a.

Kanda hii inaundwa na kaunti zifuatazo, Nyandarua (wapigakura 255,984), Nyeri (wapigakura 356,381), Kirinyaga (wapigakura 265,290), Muranga (wapigakura 452,841) na Kaunti ya Kiambu  yenye wapigakura 862,829.

KANDA YA PWANI

Ukanda huu Chama cha Jubilee kitaongozwa na wanasiasa watatu waliojitoa ODM ambao ni Salim Mvurya, Gideon Mung'aro na Zainabu Chidzuga. Wanasiasa hao watasaidiwa na Naomi Shaaban, Suleiman Shahbal na Danson Buya Mungatana.

KANDA YA MASHARIKI

Kiraitu Murungi ataongoza jahazi la Jubilee akishirikiana na  Kalembe Ndile, Rachael Nyamai, Kithure Kindiki, Joe Mutambo, Regina Ndambuki, Victor Munyaka na John Muchiri.

KANDA YA KASKAZINI

Kiongozi wa wabunge wa Jubilee bungeni, Aden Duale, ataongoza mapambano ya chama hicho katika ukanda huo akishirikiana na Mohamed Mohamud, Abbas Sheikh na Hassan Yussuf.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles