Kanda amezishika pabaya Simba, Mazembe

0
893

NA ZAINAB IDDY

KWA hakika maisha tunayoishi sasa ni yale yale ambayo mababu na mabibi zetu waliwahi kuishi, ingawa tupo katika zama tofauti.

Ndio uhalisia ulivyo kwani kadri dunia inayozunguka kama wanavyotueleza wanasayansi, ndivyo na sisi  tunavyokanyaga mabaki  ya waliofutika katika sura ya dunia.

Hivi ulishawahi kujiuliza kuwa ni kwanini klabu nyingi zinapomuacha mchezaji kuna muda zinatamani arejee tena ? kama ndiyo umeshajiuliza sababu vitu gani vinasababisha ? jibu pekee la maswali haya wanazo viongozi wa timu husika.

Ni miezi takribani nane tangu nyota wa Simba anayecheza kwa mkopo akitokea TP Mazembe , Deo Kanda kuonyesha umahiri wake ndani ya ardhi ya Tanzania.

Deo Kanda rafiki wa nyavu adui wa walinda mlango, alijiunga na Simba kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC).

Mazembe ililazimika kumtoa kwa mkopo Kanda ili kulinda kiwango chake kwakua ilikuwa na wakali wengine zaidi yake Meshack Elia , Jackson Muleka na Wengine.

Simba wao waliona nafasi ya Kanda kama mrithi wa Emmanuel Okwi kuja kuwapa ushindani akiwa Fransis Kahata, Hassan Dilunga ‘HD’ na Rashid Juma, ili kuongeza utamu wa kikosi.

Hatimaye Kanda akatua katika ardhi ya Tanzania na kutambulishwa siku ya tamasha la siku ya Simba yaani ‘Simba Day’.

Tamasha hilo lilienda sambamba na kupigwa mtanange kati ya wenyeji Simba na timu ya Power Dynamo ya Zambia.

Mabao saba aliyoifungia Simba na kutoa pasi tatu zilizozaa mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara, zimewafanya  Wekundu wa Msimbazi kunogewa naye, hivyo kuweka wazi mpango wao wa kutaka kumpa mkataba wa miaka mitatu mara wa kuendelea kusalia Dar es Salaam yaliko makazi yao.

Kitu kikubwa ambacho Simba hawatokisahau kwa Kanda ni pale alipowafungia bao pili katika mechi ya Watani wa jadi (Kariakoo Derby) iliyopigwa Januari 4.

Kanda alifunga bao hilo dakika ya 46, huku mechi ikimalizika kwa sare ya 2-2 kabla ya beki Juma Abdul kutia ‘shubiri kwenye pilau’ la Wekundu wa Msimbazi baada ya kumfanyia madhambi Kanda na kufanya atolewe nje ya uwanja, majeraha yaliyomuweka benchi kwa muda mrefu.

Mtafuta ridhiki hachoki, Simba wakawa wavumilivu katika kipindi chote kumlea mwana na kumuimbia nyimbo za matumaini.

Mungu si Athumani bwana,Kanda kapona na kuanza kukiwasha dimbani kucheka na nyavu.

Ubora wa Kanda dimbani ni wazi ulipeleka maudhi kwa bosi wake Moise Katumbi kuwa hakuwa na subira, kwani Wanamsimbazi wamemuoelewa kwani katika mechi 10 alizocheza za ligi amecheka na nyavu mara saba.

Rekodi hiyo ndiyo inawafanya wadau wa Simba kujijiuliza ingekuwaje kama  Kanda asingekumbwa na balaa la majeraha.

Wapo wanaoamini angefukuzana kwa karibu na mshambuliaji wao mahiri Meddie Kagere, ambaye anaongoza chati ya wafungaji akiwa na mabao 19.

Matumaini ya huenda Kanda akawa bora zaidi baadae, yamewapa nguvu ya kupanga kukaa nae mezani ili kumpa kanadarasi ya miaka mitatu kwani hadi ligi inamalizika mkataba wake na Mazembe utakuwa umekwisha hivyo atakuwa mchezaji huru.

Wakati Simba wakipanga kumpa kandarasi, klabu ya TP Mazembe chini ra Rais wake Katumbi,wanapanga kumrejesha kikosini nyota wao huyo kitu ambacho uenda kikazua vuta nikuvute baina ya timu hizo lakini ikawa nafasi kwa Deo Kanda kupanda dau.

Mazembe ilimtoa kwa mkopo Banda baada ikiamini  hana nafasi tena ya kufanya makubwa lakini, ingawa pia maelewano hafifi na aliyekouwa kocha wao Pamphile  Mihayo yanatajwa kuchangia.

Hapa ndipo ule usemi wa kuwa, mwenye kisu kikali ndiye mla nyama utakapochukua nafasi kwa maana kuwa atakayeweka dayu nono mezani kwa Deo ndiye  atakayepata nafasi ya kummiliki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here