23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kamwelwe azindua huduma za mawasiliano vijijini

Na MWANDISHI WETU-MLELE

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amezindua huduma ya mawasiliano vijijini, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi. 

Uzinduzi huo ulifanyika jana katika Kijiji cha Kanoge kwa kuzindua mnara wa mawasiliano uliojengwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kushirikiana na Kampuni ya Simu ya Vodacom Tanzania na ujenzi wake umegharimu Sh milioni 300.

Alisema kuwa kampuni za simu nyingi zipo nchini ila hazikutaka kwenda vijijini bali kwenye maeneo yenye fedha, ila Serikali imeanzisha Mfuko wa UCSAF na inatoa ruzuku kwa kampuni za simu ambapo nazo zinachangia kujenga minara vijijini ili kupeleka mawasiliano maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.

“Na kwa vile leseni natoa mimi, sasa nazielekeza kampuni za simu nenda kijijini au mahali fulani ambako hamna mawasiliano na hakuna mvuto wa kibiashara na wanakwenda ili kufikisha mawasiliano kwa wananchi,” alisema Kamwelwe.

Pia, amewaambia UCSAF kupeleka pia mawasiliano ya data na si ya sauti tu kwa kuwa bila data wanafunzi hawataweza kusoma shuleni na wananchi pia wanataka data. 

“Ndiyo maana awali nilileta kompyuta 50 kwa shule za msingi na sekondari, sasa naleta umeme ili watoto waanze kucheza na kompyuta kwa kuwa sasa hivi teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ni uchumi,” alisema. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya UCSAF, Dk. Joseph Kilongola, alisema kuwa kwa kutumia Mfuko wa UCSAF wanahakikisha mawasiliano yanawafikia wananchi kwa kuwa kampuni za simu pekee haziko tayari kupeleka mawasiliano maeneo ya vijijini.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba alisema kuwa hadi sasa usikivu wa mawasiliano umefikia kiwango cha asilimia 94 ukilinganisha na asilimia 45 mwaka 2009 wakati UCSAF inaanzishwa. 

Mashiba alisema kuwa UCSAF imetangaza zabuni za kujenga minara ya mawasiliano kwenye kata 252 nchini ambapo utekelezaji wa zabuni utakapokamilika usikivu wa mawasiliano utaongezeka na kufikia kiwango cha asilimia 96.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles