24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kamusoko, Ajib, Abdul wafunika Dar

tuzo

NA MICHAEL MAURUS,

WANASOKA Thaban Kamusoko, Juma Abdul, Amissi Tambwe, Ibrahim Ajib na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, juzi usiku walikuwa kivutio katika hafla ya utoaji tuzo za wachezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hafla iliyofanyika Hoteli ya Double Tree, jijini Dar es Salaam.

Katika tukio hilo, wachezaji hao pamoja na kipa wa Azam FC, Aishi Manula, waliibuka kidedea katika vipengele tofauti.

Wakati Abdul akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu, Kamusoko ndiye mchezaji bora wa kigeni, Tambwe (mfungaji bora), Ajib (bao bora), Tshabalala (chipukizi bora), wakati Manula aliondoka na tuzo ya kipa bora.

Kila jina la mmoja wao lilipotajwa, wadau wa soka waliokuwapo ukumbini hapo wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, waliwashangilia mno kuonyesha kuridhika kwao na tuzo walizochukua.

Kati yao hao, Abdul na Ajib ndio walioshangiliwa zaidi kama ilivyokuwa kwa wanasoka wa zamani, Mohammed Mwameja na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ waliofika kwa ajili ya kukabidhi tuzo kwa washindi.

Wakati Mwameja akikabidhi tuzo ya kipa bora iliyochukuliwa na Manula, Mmachinga alimkabidhi Tambwe tuzo ya mfungaji bora.

Ikumbukwe kuwa Mwameja anatajwa kama miongoni mwa makipa mahiri waliowahi kutokea nchini, akiwa ameidakia Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars kwa mafanikio makubwa.

Kwa upande wake, Mmachinga aliyetamba akiwa na Yanga na Taifa Stars, bado anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji mabao bora zaidi kwani rekodi yake ya mabao 26 aliyofunga haijavunjwa na mchezaji yeyote.

Awali akizungumza kabla ya tukio la kukabidhi tuzo, Mkuu wa Mauzo na Usambazaji wa Vodacom Tanzania, Dominician Mkama, alisema mwaka huu wametoa zaidi ya Sh 232,974,660 kama zawadi za washindi, ikiwa ni ongezeko tofauti na mwaka jana ambapo ilikuwa ni Sh 219,502,500.

“Pia kuna zawadi ya shilingi 9,000,000, ambapo kila mchezaji bora wa mwezi alikuwa akizawadiwa Sh 1,000,000 katika kipindi cha miezi 9 ya ligi. Zawadi hii imekuwa ikiongeza motisha ya wachezaji kucheza vizuri katika msimu mzima wa ligi,” alisema na kuongeza:

“Tunafurahi kuona timu zinazostahili kupata zawadi na washindi wote ama wawakilishi wao wako hapa kupokea zawadi hizi. Kwa mara nyingine tena tunatoa wito kwa wadau wote kushiriki kubuni mikakati ya kuboresha ligi hii na ikiwezekana wajitokeze wafadhili wengine zaidi ili wachezaji wazidi kunufaika.

“Kama sote tunavyoelewa hivi sasa michezo si burudani tu kama ilivyokuwa miaka ya zamani bali inasaidia kupunguza tatizo la ajira na kuinua uchumi wa nchi kwani wanamichezo wakiwezeshwa wanaweza kupitia mapato yao kuboresha pato la taifa kama tunavyosikia katika nchi za wenzetu ambako wachezaji na wasanii ni kundi la mamilionea wanaotambulika na hapa tukiamua yote haya yanawezekana na dalili zimeanza kuonekana.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles