23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Kampuni zakuna vichwa kukabili changamoto sekta ya nishati

TANGU mwaka 2014 dunia imeshuhudia bei ya mafuta ikiendelea kushuka kwa karibu asilimia 75 kutoka dola 140 na kufikia karibu dola 30 kwa pipa.

Mwenendo huo ambao ni furaha kwa mataifa yasiyozalisha nishati ni mchungu kwa kampuni kubwa na nchi zinazoizalisha na hivyo kupigilia msumari wa matatizo kwenye msingi wa uchumi wao.

Nchi na kampuni hizo zimekuwa zikihaha kukuna kichwa kukabiliana na si tu changamoto hiyo bali pia kuboresha nishati safi na kuzipunguza zile zilizo mchawi wa mazingira na hivyo mabadiliko ya tabia nchi.

Wadau wa nishati duniani wanajadili mikakati ya kuchukua kufuatia kufikiwa kwa makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. 

Wanasema mageuzi na uvumbuzi wa teknolojia ni muhimu kwa sekta za nishati za jadi katika kukabiliana na bei ndogo ya mafuta na changamoto zinazotokana na nishati safi.

Pia wanasema ni sehemu muhimu katika juhudi za kimataifa za kubana matumizi ya nishati na kupunguza utoaji wa hewa zinazosababisha ongezeko la joto duniani.

Kama ilivyo kwa kampuni nyingine za nishati, Chevron yenye makao yake makuu California nchini Marekani inashuhudia kipindi kigumu. 

Ikikabiliwa na bei ndogo ya mafuta na wito wa kupunguza matumizi ya nishati na utoaji wa hewa chafu, kampuni hiyo inatafuta fursa za kufanya ushirikiano na kampuni ndogo na zenye ukubwa wa kati.

Kampuni hizo inazozilenga ni zile zenye kuzingatia uvumbuzi, hatua ambazo zinaweza kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali.

Chevron na kampuni ya mafuta na gesi ya Airborne zilisaini makubaliano ya kufanya ushirikiano wa kusanifu na kutengeneza bomba la kusafirishia mafuta kwenye bahari ya mbali ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza usalama.

Mtendaji Mkuu wa Airborne, Eric van der Meer, alisema kampuni kubwa za nishati na zile za uvumbuzi zinaweza kusaidiana katika utafiti na usanifu na kupata mafanikio ya pamoja kupitia ushirikiano.

“Ni vigumu kwa kampuni zenye nguvu katika sekta fulani kufanya uvumbuzi kwa kuwa zina mambo mengi ya kufuatilia. Uvumbuzi unahitaji juhudi zisizokoma na makosa, lakini cha muhimu ni kuwa na moyo wa uvumbuzi. 

“Hiyo ni sababu inayofanya kampuni za uvumbuzi kuwa mbele huku zile kubwa zisizofanya uwekezaji katika eneo hilo zikishindwa kufanya chochote,” anasema.

Kwa kawaida mkutano wa CERAWeek ulikuwa ni baraza la watu mashuhuri wa sekta ya mafuta na kemikali. 

Katika miaka ya karibuni, mkutano huo pia umeanza kuhudhuriwa na wadau wa sekta za umeme, nishati mbadala na huduma za nishati. 

Hata hivyo, wadau wa mafuta, gesi ya asili, umeme na nishati mpya wana maoni ya pamoja kuwa katika mazingira ya bei ya chini ya mafuta na makubaliano ya Paris, sekta ya nishati inakabiliwa na mabadiliko yasiyo na kifani. 

Walisema kusipokuwa na mageuzi kwa wakati, sekta ya mafuta na gesi itapotea.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Nishati ya Centrica ya Uingereza, Iain Conn amesema, hamasa ya mabadiliko ya sekta ya nishati inatokana na mahitaji mapya ya wateja, teknolojia mpya na mchango wa ‘Big Data.’ 

Conn amesema, kutokana na hamasa za nguvu hizo, uzalishaji na muundo wa usafirishaji wa nishati vitashuhudia mabadiliko mapya na kutatanisha zaidi mageuzi ya sekta ya nishati.

Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Umeme ya Schneider ya Ufaransa, Jean-Pascal Tricoire, amesema kama kampuni haziwezi kuzoeya kwa haraka mabadiliko hayo zitashindwa katika ushindani wa ndani na nje ya nchi.

“Katika zama za leo, naona wateja wanaweza kuwa na haki ya kujiamulia kuhusu matumizi ya umeme, ikiwemo kuchagua rasilimali za kuzalisha umeme, hali ambayo inaweza kugeuka kuwa halisi kutokana na uwazi unaoletwa na teknolojia mpya. Hii inamaanisha kuwa kama kampuni zisipofuata njia sahihi hakika zitashindwa kushindana.”

Kwa mujibu wa makadirio ya kampuni kubwa ya mafuta ya Exxon Mobil, hadi kufikia mwaka 2040, mahitaji ya nishati duniani yataongezeka kwa asilimia 25, ongezeko litakalochochewa zaidi na mahitaji ya nchi zinazoendelea. 

Pamoja na ujio wa nishati mbadala, nyuklia, mafuta yatabaki kama nishati kuu kwa miaka mingi ijayo

Kampuni hiyo imekadiria kuwa matumizi ya nishati mbadala na nishati ya nyuklia yataongezeka lakini sekta mbadala za kemikali na mafuta zitachukua asilimia 80 ya nishati zote huku mafuta yakiendelea kuwa nishati kuu.

Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya uzalishaji na Usafirishaji umeme ya Edison International yenye makao makuu California, Marekani, Theodore Carver, amesema;

“Mbali na kutumia nishati safi kuzalisha umeme, kupunguza utoaji wa hewa ya carbon kunahitajilka kuboresha mfumo wa usafirishaji wa umeme.

“Uzalishaji wa umeme kwa nishati safi za aina mbalimbali unahitaji mfumo wa kisasa wa kusafirisha na kugawa umeme. Kwa mfano, kuna mtu anayeweka vifaa vya kuzalisha umeme wa jua kwenye paa wakati uwezo wake wa kuzalisha umeme unazidi mahitaji na anaweza kuwauzia wengine.”

“Lakini pia wakati mwingine kama umeme unaozalishwa ni mdogo kuliko unaohitajika, pia unahitaji nyongeza. Mfumo wa kisasa wa kugawa umeme unaweza kutatua tatizo hilo. Hili ndilo soko la kimkakati tunalolilenga,” alisema.

Hata hivyo, kutokana na ukubwa wa biashara na athari kubwa kwa wafanyakazi na mazingira, si rahisi kuhimiza teknolojia mpya katika sekta ya nishati. Aidha, fedha pia ni muhimu kwa kampuni za nishati katika kufanya uvumbuzi na mageuzi ya teknolojia mpya. 

Wakati bei ya mafuta iko chini, kampuni za mafuta zinapunguza matumizi kwenye utafiti kutokana na kupungua kwa mapato. 

Pamoja na taratibu zenye uangalifu za kuthibitisha mipango mipya, kampuni nyingi za uvumbuzi zinakabiliwa na changamoto zinaposhirikiana na kampuni za nishati zenye nguvu.

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Airborne, Eric van der Meer, bei ndogo ya mafuta si tu imezuia maendeleo ya kampuni za nishati, bali pia imetoa changamoto kwa kampuni za nishati zenye uvumbuzi na kukwamisha mchakato wa uvumbuzi na mageuzi ya sekta ya nishati.

“Kupunguza matumizi ni suala moja lakini kampuni kubwa ambazo siku zote zinataka kudhibiti hatari zao pia zina urasimu, ni wachache wanaopenda kutoa maamuzi yenye hatari. Kwa hiyo suala tunalokabiliana nalo ni upungufu wa fedha na muda mrefu wa kufanya maamuzi.”

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles