33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

KAMPUNI ZA SIMU ZATOZWA FAINI BIL 10.7/-

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezipiga faini ya Sh bilioni 10.7 kampuni sita za simu za mkononi kwa kosa la kushindwa kuzingatia utaratibu katika usajili wa namba za simu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, alizitaja kampuni hizo kuwa ni Airtel, Tigo, Vodacom, Zantel, Halotel na Smart na faini hizo zinatakiwa kulipwa kabla ya Oktoba 14, mwaka huu.

Pia alisema walifanya ukaguzi na kubaini kuwa, watoa huduma wanasajili namba za simu holela bila kuomba vitambulisho vinavyokubalika katika usajili, kutowapiga picha wateja, kutopata uthibitisho wa sahihi ya mteja na kutumia kitambulisho cha mtu mwingine.

“Mtu atakayehitaji kununua laini ya simu ahakikishe inasajiliwa kikamilifu kwa kutumia taarifa zake sahihi, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake, aliyemsajili na kampuni ya simu husika,” alisema.

Kilaba alisema vitambulisho vilivyoruhusiwa kisheria ni Kitambulisho cha Taifa, cha Mzanzibari Mkaazi, hati ya kusafiria, kitambulisho cha mpiga kura au leseni ya udereva.

Kutokana na makosa hayo, alisema Airtel imetozwa faini ya Sh bilioni 1.08, Smart imetozwa Sh milioni 75, Tigo imetozwa Sh bilioni 1.3, Vodacom imetozwa Sh milioni 945, Zantel imetozwa Sh milioni 105 na Halotel imetozwa Sh bilioni 1.6.

Pia alisema kampuni hizo zimetozwa faini kwa kurudia kukiuka sheria ambapo Airtel imetozwa Sh milioni 542.5, Smart imetozwa Sh milioni 37.5, Tigo imetozwa Sh milioni 652.5, Vodacom imetozwa Sh milioni 472.5, Zantel imetozwa Sh milioni 52.5 na Halotel imetozwa Sh milioni 822.5.

Alisema kampuni hizo zimetakiwa kulipa kila mmoja faini ya Sh milioni 500 kwa kuathiri na kuhatarisha usalama wa umma na jamii ya Watanzania.

Alizitaka kampuni za simu nchini kubaki na nakala ngumu au laini ya vivuli vya nyaraka za usajili wa namba ya simu na kutoruhusu laini kutumika kabla ya usajili kukamilika.

“Usajili usiozingatia taratibu unaficha taarifa za watumiaji na kusababisha wapate mwanya wa kufanya vitendo vya uhalifu kama wizi na utapeli, kwa sababu katika miongo hii uhalifu unaenda kidijitali zaidi,” alisema.

Julai, mwaka jana, TCRA ilitoa adhabu ya faini kwa watoa huduma waliokiuka utaratibu wa kusajili namba za simu na kuwataka kuzifungia namba zote ambazo hazijasajiliwa zilizokuwa zinatumika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles