Na ESTHER MNYIKA-DAR ES SALAAM
SERIKALI imeitaka Kampuni ya M/s China Civil Engineering Construction Corparation (CCECC) kukamilisha mradi wa ujenzi wa barabara za juu ‘interchange’ katika makutano ya Ubungo ndani ya miaka ya mitatu.
Mkataba uliofikiwa unamtaka Mkandarasi ambayo ni Kampuni ya CCECC kutoka China kuanza ujenzi huo mara moja na ujenzi huo ambao unatarajiwa kutumia takriban miezi 30 kukamilika
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Patrick Mfugale aliyesema hayo Dar es Salaam jana baada ya kusaini mkataba na kampuni hiyo ya ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Barabara ya Sam Najoma, Morogoro na Mandela.
“Zaidi ya Sh bilioni 177.4 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo ambao utakawekewa jiwe la msingi Machi mwaka huu.
“Hakikisheni mnaanza ujenzi mara moja kwa sababu Serikali imeshakamilisha taratibu zote na tayari Sh bilioni 2.1 zimelipwa kwa ajili ya fidia kwa wananchi walioguswa na mradi huo,” alisema Mfugale.
Alisema ujenzi wa Ubungo interchange unatekelezwa kwa fedha ya mkopo kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya uboreshaji miundombinu ya usafiri Dar es Salaam.