25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Kampuni yadaiwa bilioni 3/- za wakulima wa pamba

Derick Milton – Simiyu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Simiyu, imesema Kampuni ya NGS ya mjini Bariadi, ambayo ilikuwa miongoni mwa kampuni zilizonunua pamba mwaka jana, imekuwa na usumbufu kulipa madeni ya wakulima na tozo nyingine.

NGS ilikuwa miongoni mwa kampuni 10 zilizohojiwa na Takukuru na kutakiwa kulipa madeni ya wakulima ndani ya wiki moja.

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Simiyu, Alex Mpemba wakati wa kukabidhi Sh milioni 26 za wakulima wa pamba wa Kijiji cha Mwasamba wilayani Busega, ambazo zilirejeshwa na viongozi wa Amcos baada ya kufanyia matumizi mengine.

Mpemba alisema kampuni nyingine tisa zimetekeleza makubaliano hayo kwa kiwango kikubwa, huku baadhi zikimaliza madeni yao kwa wakati ikiwamo Kampuni ya Nsagal Co Limited, na nyingine ziko hatua za mwisho.

Alisema kuwa NGS inadaiwa zaidi ya Sh bilioni tatu yakiwamo madeni ya wakulima, ushuru wa Amcos pamoja na halmashauri, huku wakulima wengi ambao hawajalipwa ni kutoka katika Jimbo la Itilima.

 “Hata halmashuari inamdai kiasi kikubwa cha fedha. Toka tumewekeana hayo makubaliano, kampuni hiyo haijaonyesha jitihada zozote za kuanza kulipa deni hilo, wakati wengine wakifanya jitihada za kumaliza madeni yao na wametuletea mrejesho, NGS hakuna ilichofanya,” alisema Mpemba.

Alisema kuwa Takukuru itawachukulia hatua kali viongozi wa kampuni hiyo kwa kushindwa kutekeleza makubaliano hayo, huku akibainisha kuwa wameiongezea muda wa siku mbili ihakikishe inalipa deni hilo.

“Tumewasiliana na viongozi wa kampuni, lakini tunaona hawana dalili zozote za kulipa deni hilo, na ndiyo kampuni iliyobaki ikidaiwa deni kubwa sana, tumewapa tena siku mbili walipe deni lote, wakishindwa tutachukua hatua nyingine kali zaidi,” alisema Mpemba.

Aidha Mpemba alisema kuwa wamefanikisha kurejesha zaidi ya Sh milioni 100, fedha ambazo zilikuwa za wakulima kwa ajili ya kulipwa baada ya kutumiwa kwenye matumizi mengine na viongozi wa Amcos.

Katika ulipaji wa fedha hizo, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Ibrahimu Kadudu aliwataka wakulima kuanza maandalizi mapema ya kufungua akaunti benki, kwani malipo ya msimu wa mwaka huu yatafanyika kwa njia hiyo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,530FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles