31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KAMPUNI YA HALOTEL KUWAWEZESHA WAFANYABIASHARA

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


MTANDAO wa simu wa Halotel umezindua huduma itakayowawezesha wateja wake ambao ni wafanyabiashara kuweza kutangaza biashara zao bure kwa kutumia huduma mpya iliyozinduliwa na kampuni hiyo inayojulikana kama ‘Halo SAINI’.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika uzinduzi wa huduma hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Ziada wa Halotel, Caroline Majaliwa, alisema mapinduzi hayo ya teknolojia yatawawezesha mamilioni ya wafanyabiashara nchini  wanaotumia mtandao huo kuweza kutangaza biashara zao hasa kwa wale wanaowapigia na hata wanaopokea simu zao.

“Licha ya kuendelea kuwa na huduma nzuri za kuvutia, tumeendelea kubuni na kuja na huduma zitakazowawezesha wateja wetu kuendelea kufurahia huduma zetu kadha wa kadha na sasa kuwawezesha kutangaza biashara zao kwa watu wanaowapigia au kupokea simu zao, ambapo baada ya kuwezesha huduma hiyo wataweza kupokea ujumbe maalumu ambao atahitaji yeye mwenyewe ufike kwa wateja wake,” alisema Majaliwa.

Alisema ili mteja aweze kufurahia huduma hiyo, atatakiwa kutuma neno ON kwenda namba 15614 kujiunga na kisha atapaswa kutuma neno SAINI kisha ujumbe ambao anataka watu waupate pindi watu watakapokuwa wakimpigia au yeye kuwapigia kwenda kwenye namba 15614.

Kwa Upande wake, Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo, Stella Pius, alisema licha ya kuwawezesha wateja wao kuweza kutumia nafasi hiyo kutangaza biashara zao, wameamua kuwazawadia wateja wao wote ambao wameendelea kuwaunga mkono kwa kuwawezesha kushinda zawadi mbalimbali kila watakapokuwa wanaweka muda wa maongezi.

“Tunathamini sana mchango wa wateja wetu na tumeamua nasi kuendelea kuwazawadia kwa kuwawezesha kujishindia zawadi kem kem kila wanapoweka vocha za mtandao wa Halotel.

“Kila mteja wa Halotel atakapoweka vocha katika simu yake atapokea ujumbe wenye namba ya bahati ambayo atatakiwa kuituma kwenda namba 0901220004 na ataingia katika droo ambayo itamwezesha kujishindia zawadi ya muda wa maongezi au Smartphone zitakazokuwa zinatolewa kwa siku, wiki na kila mwezi kwa washindi watano (5),” alisema Stella na kuongeza:

“Tutakuwa tunachezesha droo kwa siku, wiki na kila mwezi na washindi watajishindia muda wa maongezi wa hadi shilingi 50,000  pamoja na simu za Smartphone zenye teknolojia ya hali ya juu. Hili linatuwezesha sisi kuendelea kuthamini mchango wa wateja wetu ambao wameendelea kutuunga mkono siku hadi siku,” alisema.

Hatua hiyo imekua kutokana na kampuni hiyo kuboresha huduma nyingine ambazo zitawawezesha wateja wa mtandao huo kuweza kusikiliza redio katika maeneo mbalimbali yaliyo na mtandao wa Halotel, hata kama hakuna masafa ya FM/AM ya radio hiyo katika eneo husika.

Huduma nyingine iliyozinduliwa sambamba na huduma hizo ni pamoja na huduma ya Halosoka ambayo itamwezesha mteja wa mtandao huo kuweza kupata matokeo ya mpira wa miguu papo hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles