Na GABRIEL MUSHI – DODOMA
HATIMAYE Serikali imempata mwendeshaji wa pili wa mradi wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (DART), baada ya mwendeshaji wa kwanza wa mradi huo, Kampuni ya Uda-Rapid Transit (Uda-RT), kuonekana kusuasua.
Katika siku za karibuni, Uda-RT imekuwa katika mgogoro na kampuni inayosimamia ukusanyaji wa malipo ya tiketi katika mradi huo, Maxcom Tanzania, hali iliyosababisha kero kwa baadhi ya watumiaji wa usafiri huo.
Pia mabasi yanayotumika katika mradi huo kwa sasa, yameelezwa kutotosheleza, jambo linalosababisha msongamano vituoni na katika mabasi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege, akizungumza na MTANZANIA, alisema ili kumaliza kero hizo, tayari kandarasi imeshatangazwa na mwendeshaji mpya ameshapatikana.
“Kandarasi imeshatangazwa na ameshapatikana mmoja anayejiita Emirates kutoka Dubai, nao wataingiza mabasi yao.
“Siwezi kusema ni lini ataanza kuingiza mabasi na kuendesha mradi kwa sababu taratibu za zabuni zipo kwenye ‘ku-award’, ila niwahakikishie tunakwenda vizuri. Kuna mambo machache ambayo hayajawa ‘confirmed’ (thibitishwa).
“Jambo la msingi ni kuhakikisha tunapata ‘operator’ (mwendeshaji) mzuri ili wananchi wa Dar es Salaam waendelee kufurahia usafiri mzuri,” alisema.
Alisema uendeshaji wa mradi huo kwa sasa ni wa awamu ya kwanza, ambao unafanywa na Kampuni ya Uda-RT inayomilikiwa kwa ubia na Kampuni ya Simon Group na Serikali.
Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.