KAMPUNI YA CHAI UNILEVER YAWEKEZA BIL 1/-

0
1162

 

Na Mwandishi Wetu, Iringa


KAMPUNI  ya Chai ya Unilever Tanzania (UTT), imewekeza Sh bilioni mia moja nchini katika kipindi cha miaka minne, imeelezwa.

Akizungumza jana mjini hapa na timu ya wanahabari waliotembelea wilayani Mufundi, Mkurugenzi Mtendaji wa UTT, Ashton Eastman, alisema uwekezaji huo ni juhudi za kampuni yake katika kutekeleza makubaliano na Serikali yaliyoingiwa mwaka 2013 yakilenga kuboresha zao la chai kwa manufaa ya wakulima wadogo na uchumi wa Taifa kwa jumla.

Lengo la ziara hiyo ni kufanya tathmini ya maendeleo ya zao la chai na jinsi linavyowanufaisha wakulima wadogo.

Kutokana na hali hiyo, UTT iliahidi kuongeza uwezo wa kuchakata chai katika viwanda vyake vitatu vilivyopo Mufindi na kuongeza ukubwa wa mashamba.

Kampuni hiyo pia iliahidi kuboresha makazi, huduma za afya na elimu kwa wafanyakazi.

Pamoja na hali hiyo, UTT ilitangaza ahadi yake ya kujenga kiwanda kipya na miundombinu itakayorahisisha ukusanyaji wa majani ya chai mabichi kutoka kwa wakulima wadogo, huku ikiwahudumia kwa kuwapa huduma za ugani, mbegu, mbolea na kuanzisha mashamba darasa.

“Kwa kiasi kikubwa, ahadi hizi zimetekelezwa. Sasa tuna kiwanda kipya pale Njombe ambacho ujenzi wake umegharimu Sh bilioni 18. Kiwanda kina uwezo wa kuchakata tani 50 za chai kwa siku. Katika kuendeleza wakulima wadogo, asilimia 70 ya majani ya chai yanachakatwa Njombe hutoka kwa wakulima wadogo,” alisema.

Katika makubaliano hayo, Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, iliahidi kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji kupitia maboresho ya sera, kodi na tozo. Serikali pia iliahidi kuwezesha upatikanaji wa eka 1,602 za eneo la Ngwazi ili litumike katika kuendeleza zao la chai.

Kampuni ya UTT ilinunua shughuli zote za Kampuni ya Brookside miaka ya 1980, lakini katika makubaliano iliahidi kushirikiana na wadau wengine ili kuliendeleza eneo la Ngwazi endapo Serikali ingesaidia kurejeshwa katika umiliki wa kampuni.

Hata hivyo, katika kusaidia juhudi za Serikali za kulinda raia na mali zao, UTT imetoa Sh milioni 80 katika ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Kibao. Katika sekta ya afya, Hospitali ya Unilever ya Lugoda ndilo kimbilio la wakazi wa Mufindi.

Akizungumzia mafanikio ya ushirikiano baina ya Serikali na UTT, Ofisa Utawala wa hospitali Lugoda, Dk. Linus Nchimbi,  alisema hospitali hiyo inahudumia watu wapatao 8,697 wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) ambao asilimia 70 si wafanyakazi wa kampuni.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Unilever ya Lugoda, Dk. Mattias Mwandu, alisema hospitali hiyo ina vitanda 70 na hutoa huduma za maabara, X-Ray, Ultra Sound na upasuaji kwa bei za kawaida.

“Kwa mfano, mtu analipia Sh 10,000 tu ili kuonana na daktari bingwa,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here