28.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 3, 2024

Contact us: [email protected]

Kampuni ya CCCC yanadi fursa kwa wanafunzi DIT

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya Serikali ya China (CCCC) imewahamasisha wahitimu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuchangamkia fursa za ajira katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na kampuni hiyo nchini.

Akizungumza Agosti 14,2024 na wanafunzi wa fani ya uhandisi, sayansi na teknolojia ambao wanatarajia kumaliza masomo yao baadaye mwaka huu, Naibu Meneja wa CCCC Tawi la Tanzania, Li Yuliang, amesema DIT inatoa wahitimu mahiri ndio maana wamevutiwa kwenda chuoni hapo kunadi fursa walizonazo.

“Tumekutana na wanafunzi hawa kwa lengo la kuwaelezea shughuli tunazozifanya na fursa zilizopo katika miradi mbalimbali, aina ya miradi tunayoifanya na watu tunaohitaji, DIT inatoa wahitimu mahiri kwahiyo tunawahamasisha waje kufanya kazi katika kampuni yetu,” amesema Yuliang.

Amesema fursa hizo ziko katika miradi inayoendelea maeneo mbalimbali nchini kama vile ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) Dar es Salaam, Masasi mkoani Mtwara, Kagera na Mkomazi mkoani Kilimanjaro.

Mmoja wa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye kwa sasa ni mwajiriwa katika Kampuni ya CCCC, Edson Edward, amesema tangu alipoingia katika kampuni hiyo amejifunza vitu vingi ikiwemo kutumia vifaa vya kisasa na kufahamiana na kampuni kubwa zinazojihusisha na masuala ya ujenzi.

“Wanafunzi wapende kujifunza vitu vingi zaidi kwa sababu mwingine anaweza kusoma IT au ‘computer science’ halafu anasema hawezi kufanya kitu kingine, wawe na elimu mbadala zaidi ya ile wanayoipata darasani ili kuongeza ujuzi,” amesema Edward.

Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano Viwandani wa DIT, Dk. Sosthenes Karugaba, amesema kupitia dhana ya mafunzo viwandani wahitimu wa chuo hicho wana uwezo wa kufanya kazi kwa umahiri mkubwa.

“Tunashukuru Kampuni ya CCCC imezungumza na wanafunzi wetu ambao wanatarajia kumaliza masomo yao mwaka huu wajue ambacho watakutana nacho katika ulimwengu wa ajira, tunahakikisha wanafunzi wetu wanapokuwepo chuoni wanapata mafunzo ya vitendo zaidi na kutembelea viwandani, tumekuwa tukishirikiana na viwanda na wadau mbalimbali katika shughuli za nje ili wanafunzi waweze kupata uzoefu na kuwarahisishia kufanya vema zaidi wanapokwenda kutafuta ajira au kujiajiri,” amesema Dk. Karugaba.

Kampuni ya CCCC ilianza shughuli zake nchini mwaka 2009 ambapo imeshiriki katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na sasa inaendelea na miradi mingine ukiwemo ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (BRT).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles