27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Array

kampeni za vyama vitatu

 NORA DAMIAN, AHMED MAKONGO Na RAMADHAN HASSAN SIMIYU/DODOMA, BUNDA

IKIWA imetimia wiki moja tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iruhusu kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020 kuanza ni vyama vitatu tu kati ya 15 ndivyo vilivyozindua ilani zao hali kadhalika wagombea wake wakionekana kukata mbuga kunadi sera zao.

Vyama hivyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM),Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha ACT-Wazalendo ambavyo wagombea wake wakiwamo wale wa urais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania wametawanyika katika maeneo mbalimbali nchini.

Wagombea urais wengine wawili wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe na Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba wameanza kutoa ahadi.

Ingawa taarifa zilizopo ni kwamba mgombea wa Chaumma, Rungwe ambaye amebeba sera ya ‘kula ubwabwa na kuku bure’ anatarajiwa kuzindua kampeni zake leo, Manzese, Dar es Salaam. 

Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli aliyezindua kampeni zake Dodoma Jumamosi iliyopita, Tundu Lissu wa Chadema aliyezindua kampeni Zakhiem-Mbagala Ijumaa iliyopita na Bernard Membe wa ACT-Wazalendo aliyeanzia Lindi wanaendelea kuchanja mbuga katika maeneo mbalimbali nchini kunadi sera zao.

Ratiba ya awali ilikuwa inaonyeha kuwa CUF ilikuwa izindue kampeni zake Septemba 3 Mtwara.

UPDP kwa upande wake ilisema itazindua kampeni zake Lindi Septemba 19.

SAU nayo ilisema itazindua kampeni zake jijini Dar es Saalaam Septemba 3, NCCR- Mageuzi ilisema ingezindua Septemba 5, Dar es salaam DP Septemba 15.

AAFP ilisema ingezindua Septemba 5 Pwani pia ADC waliahidi kuzindua Kigoma Septemba 9 na vyama vingine NRA, NLD na ADA-Tadea bado vilikuwa vinajipanga.

Jana mgombea urais wa CCM, Dk.Magufuli alikuwa amefika Simiyu kwa ajili ya kunadi sera zake wakati mgombea wa Chadema, Lissu akitua Dodoma kwa ajili hiyo hiyo.

MGOMBEA WA CCM

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk.Magufuli amesema ndani ya miaka mitatu vijiji vyote vilivyosalia nchini 2,600 vitakuwa na umeme.

Takwimu zinaonyesha mwaka 2015 vijiji 2,018 ndivyo vilikuwa na umeme na hadi sasa vimeongezeka na kufikia 9,570 kati ya vijiji 12,228 vilivyopo nchini.

Alitoa ahadi hiyo jana wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Somanga Bariadi mkoani Simiyu.

“Tuliyoyafanya ni makubwa tunataka mtupe miaka mitano tukamalizie vijiji 2,600 kuviwekea umeme, ndani ya miaka mitatu kila kijiji kitakuwa na umeme.

“Nafikiri tunaweza ndiyo maana nilifikiri ni wakati muafaka kwa wana Simiyu kunipa tena kura nimalizie yaliyobaki.

“Kuongoza ni kutoa lengo ndicho tunachokifanya kwa maendeleo mapana ya nchi yetu, mimi bado naamini tuna mambo mengi ya kufanya katika nchi hii na hasa kuibadilisha,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema pia hivi karibuni walitangaza ajira 13,000 kwa walimu wa shule za msingi na sekondari na kwamba wataendelea kuimarisha miradi mbalimbali kama ya ujenzi wa reli, barabara na viwanda ili kutoa fursa zaidi za ajira.

YALIYOTEKEKELEZWA SIMIYU

Dk. Magufuli alisema miaka mitano iliyopita Simiyu haikuwa kama inavyoonekana sasa kwani kuna mabadiliko makubwa hasa ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, hospitali, shule na usambazaji umeme vijijini.

Aliitaja baadhi ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa, hospitali za wilaya ya Bariadi, Busega na Itilima, vituo vitatu vya afya na zahanati 14 ambavyo vimegharimu Sh bilioni 16.4.

Alisema pia Sh bilioni 15.86 zimetumika kununua dawa na vifaa tiba na kufanya miradi yote sekta ya afya kugharimu Sh bilioni 32.3.

“Mabadiliko ni makubwa hongereni sana, huu ni mkoa mpya lakini maendeleo yake utafikiri una miaka 50 unaona tu mambo, safi sana.

“Katika nchi yoyote ukitaka kujenga uchumi ni lazima uanze na vitu vinavyochochea uchumi, huwezi ukataka uchumi wakati vitu vinavyochochea uchumi hujaviendeleza.

“Niliona tutumie mbinu ya kujenga uchumi wa kisasa ndiyo maana tulianza na miundombinu, mafanikio haya halafu nikose kura ndugu zangu…hata wanaonitukana inawezekana wanasahau kwamba wananitukana wakiwa kwenye lami,” alisema Dk. Magufuli.

Dk. Magufuli alisema hivi sasa wanawake wanaojifungulia hospitali wameongezeka kutoka asilimia 53.8 (2015) hadi asilimia 88 (2019) huku vifo vya watoto vikipungua kutoka 392 hadi 100.

Alisema pia wametumia Sh bilioni 73.8 kununua madawati 88,105, kujenga madarasa 966, nyumba na maabara 78, mabweni 17, kukarabati Shule ya Sekondari Maswa na vyuo vya maendeleo pamoja na kuajiri walimu 1,116.

Kwa upande wa barabara alisema Sh bilioni 206.2 zimetumika kutengeneza kilomita 117.1 za lami na kilomita 293.4 za changarawe.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli baadhi ya barabara hizo ni ile ya Bariadi – Maswa – Mwisumbi kimomita 102, Bariadi Mjini kilomita 7.8, kilomita mbili za lami Maswa, daraja la Sibiti, stendi na maegesho ya magari pamoja na uwekaji taa za barabarani.

Aidha alisema Sh bilioni 81.1 zimetumika kufikisha umeme katika vijiji 299.

Dk. Magufuli alisema nusu ya pamba inayozalishwa nchini inatoka Simiyu na kwamba Serikali ilitoa zaidi ya Sh bilioni 12 kulipa madeni ili kuendelea kuwalinda wakulima.

“Tutajenga viwanda hapa badala ya kusafirisha pamba ghafi tufanye kila kitu hapa hapa nchini,” alisema.

Alisema pia ubovu wa barabara ya Nsokolo tayari zabuni imetangazwa na kwamba utajengwa uwanja wa ndege ili wakazi wa mkoa huo wasiwe wanalazimika kwenda Shinyanga au Mwanza.

“Mashine ya dawa za usingizi Hospitali ya Wilaya ya Bariadi hayo ni madogo, kama tumejenga hospitali hili nalo tutalishughulikia, tunayosema ni ya kweli yanatoka moyoni.

“Uongozi huwa haujaribiwi, uongozi unapimwa na sisi ndugu zangu mmeshatupima vya kutosha, haya tumeyapanga na kuyaweka kwenye ilani ya uchaguzi kwa sababu tunataka tujenge nchi yenye uchumi wa kweli,” alisema Dk. Magufuli.

KUHUSU CHENGE, CHEGENI

Dk. Magufuli aliwataka wana CCM kuwapuuza wanaotaka kuwagawa kwani kwa utaratibu waliojiwekea chama kwanza halafu mtu baadaye.

“Sisi CCM mtu akishateuliwa huyo ndiye mnaenda naye mbele, chama kwanza matakwa yetu baadaye. Zamu ya ubunge sasa hivi ni Kundo (mgombea Bariadi) na ndugu zangu wa Bariadi na wa Simiyu yale maneno yanayopitishwa na wapinzani achaneni nayo,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema wabunge wa zamani Andrew Chenge (Bariadi), Raphael Chegeni (Busega) na Salim Nguzi (Meatu) wamefanya kazi zao vizuri lakini bado anawahitaji.

“Bado tunawahitaji hata jana (juzi) nilizungumza kazi bado ziko nyingi, Chenge hapa mtemi ni kaka yangu kweli kweli wala si uongo, nilipoingia ubunge mwaka 1995 mke wangu alikuwa na mimba aliyenisaidia hela kwenda hospitali Sh 200,000 alikuwa mheshimiwa Chenge,” alisema Dk. Magufuli.

Naye Chegeni alisema; “Sisi bado ni mtaji wako kazi ulizozifanya nafarijika chini ya uongozi wako ubunge wangu umekuwa na tija sana kwa wananchi wa Busega…sasa hivi kwanza chama mtu baadaye.

Kwa upande wake Chenge alisema atahakikisha jimbo hilo linaendelea kuongozwa na CCM huku akihidi kura za kishindo kwa wagombea wote wa ubunge na udiwani.

“Umenena vizuri sikutegemea historia ya 1995 utaisema mbele ya wananchi hawa, nakushukuru sana, namshukuru sana Janeth kwa moyo wake wa upendo.

“Jimbo hili ambalo mimi niliteuliwa na CCM na kulikomboa toka upinzani tutahakikisha wembe ni ule ule kwa ushindi wa CCM, niwahakikishie kijana wetu tutafanya kazi ya uhakika ili kura za mbunge na madiwani wetu ziwe za kishindo,” alisema Chenge.

WAGOMBEA UBUNGE

Mgombea ubunge Jimbo la Bariadi, Andrea Kundo, alisema; “Mambo mengi umeyafanya, umekuwa ukitenda tunakushukuru sana kwa sababu umeokoa kinamama ambao walikuwa wanataabika, umeme mpaka sasa asilimia 75 ya wananchi wana umeme wanafanya biashara zao.

Naye mbunge wa Maswa Mashariki, Mashimba Ndaki, alisema; “Mtu akikutendea mema na wewe lazima umtendee mema, mheshimiwa rais ametutendea mema Mkoa wa Simiyu na nchi hii, tarehe 28 twende tukampe kura.

Kwa upande wake Leah Komanya ( Meatu) alisema; “Meatu tutakupatia kura za kishindo uweze kutufanyia mambo makubwa kama ulivyosema katika ilani ya uchaguzi.

Akiwa Bunda jana, mgombea huyo wa CCM, Magufuli alisema akichaguliwa, serikali yake itaendelea kutekeleza miradi mingi ya maeendeleo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi na kutoa mikopo kwa wanavyuo.

Akiwa kwenye mkutano wa kampeni, uliofanyika katika mji wa Bunda, alisema kuwa serikali yake kwa kipindi cha miaka mitano ya kwanza imefanya mambo makubwa katika suala zima la maendeleo hivyo wananchi waendelee kumchagua ili azidi kuwaletea maendeleo.

Aidha alisema kuwa anaipenda Wilaya ya Bunda kwa sababu ni wilaya ambayo imetoa viongozi wengi wa taifa hili na pia ni jirani na wilaya iliyotoa muasisi wa taifa hili Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hivyo atakapochaguliwa ataendelea kutoa miradi mingi ya maendeleo katika wilaya hiyo.

“Ninaipenda sana wilaya ya Bunda kwa sababu ni wilaya ambayo imetoa viongozi wengi, hata mkuu wa jeshi la polisi ametoka katika wilaya hii….Warioba katoka wilaya hii na wengi tu na hata Wassira” alisema.

LISSU DODOMA

Mgombea uras wa Chadema Lissu akiwa Dodoma jana alisema iwapo watanzania watamchagua atafanya marekebisho ya sheria ya jinai ambapo hakutakuwa na kosa ambalo halina dhamana.

“Sasa kwa sababu kumekuwa na ukandamizaji sana mapolisi wanaonea watu, watu wanafunguliwa mashtaka yasiyokuwa na dhamana Serikali ya uhuru na haki itafanya marekebisho makubwa katika sheria zote za jinai hakutakuwa na kosa ambalo halina dhamana.

“Serikali ya Chadema itayaondoa yote haya na tukifuta makosa yasiyokuwa na dhamana hii dhana ya mapolisi na waendesha mashtaka na mahakimu ya kufunga watu na kuwaweka mahabusu ili watoe rushwa itakwisha kwasababu sheria inasema ukinikamata unapata dhamana, tufanya haya na haya mambo ya kuenguana katika uchaguzi yatakoma kwa sababu tunataka nchi ya haki,”alisema Lissu.

Vilevile alisema kipaumbele chake kingine ni kuhakikisha kila mtanzania anapata bima ya afya ili aweze kupata huduma za afya kwa uhakika.

“Kuna watu nimesikia kwamba hizi ni ahadi hewa hizi sio ahadi hewa sijasema tutaifanya keshokutwa, baada ya kuwa Rais nafahamu zina gharama zake nafahamu haitatekelezwa kwa siku moja lazima tuwe na ‘plan’ tuwe na ramani.

“Na ramani yetu ni kwamba kila anaekaa Tanzania awe na bima ya afya ili anapohitaji kujifungua asiambiwe toa 50,000 kwa ajili ya mtoto wa kiume na ndio maana tukasema tunahitaji kufanya marekebisho makubwa katika mifumo yetu.

AIZUNGUMZIA SEPTEMBA 7

Katika mkutano huo,Lissu aliitumia Septemba 7 siku aliyopigwa risasi Jijini Dodoma kusema atahakikisha awanawatetea watu wanaopitia mateso katika nyanja mbalimbali.

“Itakapofika tarehe 7 Septemba Jumatatu ijayo nitakuwa nimetimiza miaka mitatu tangu wale wasiojulikana walipojaribu kuniua,sasa nafahamu katika hii miaka mitatu watu wengi wanajua kilichotokea.

 4

“Na kuna marafiki wameniambia niache kuzungumza yaliyotokea Septemba 7 nyinyi mnafahamu kwamba sio kila mtu katika miaka hii mitano amefanywa kama walivyonifanya mimi sio kila mmoja wenu amepigwa risasi.

“Sio kila mmoja wenu amenyanyaswa kama nilivyonyanyaswa mimi inawezekana watu wakasema kwamba haya ni ya kwangu ila nawaomba ndugu zangu mtafakari jinsi ambavyo sio mimi peke yangu nimeumizwa kila mmoja wapo ameumizwa kivyake.

“Tunapozungumzia habari ya Septemba 7 hiyo ni hadithi yangu binafsi kila mmoja wetu amepigwa na yeye kinyake kila mmojawetu ana Septemba 7 yake,”alisema Lissu.

Lissu alisema alipigiwa simu akiwa mkoani Tabora na baadhi ya wafanyakazi wa Serikali kwamba wamekatazwa wasihudhurie mkutano wake wa Dodoma hivyo alidai huo ni unyanyasaji kwani wafanyakazi hao wana muda mrefu hawajawahi kuongezewa mishahara.

“Lazima niwazungumzie hawa wafanyakazi wa Serikali waliohamia hapa Dodoma wote mnafahamu kwamba mmelazimishwa kuhama kama operesheni ya kijeshi. Hawa nao wana Septemba 7 yao nani ataisemea?

“Mfanyakazi wa Serikali ameitumikia nchi anapewa pension ya shilingi 50,000 kwa mwezi hawa nao Septemba 7 yao nani ataisemea? Ni yupi Boda

 boda ambaye hajadakwa na Polisi,”alihoji Lissu.

Alisema kinachowaumiza watanzania wengi ni kuwa na hofu ya kufa.

“Mimi nilipoamka baada ya Septemba 7 nilisema madhali Mungu ameniokoa nitarudi Tanzania kuendeleza mapambano hofu ni mbaya nani ataishi milele nani anayejua kesho yake.

“Hofu ya kifo, ni mbaya lakini kila mmoja wetu atakufa wanatutisha na hofu ya kifo wakati hata wao wataenda, kwahiyo walikuwa wanasema hatakuja sasa nimekuja, ninachotaka kuwaambia adui mkubwa unaekabiliana nae ni hiyo hofu ukiweza kuishinda tutaiondoa CCM,”alisema.

ATINGA NA KANZU

Mgombea huyo wa Chadema alifika katika viwanja hivyo vilivyopo jirani na uwanja wa Jamhuri saa 4.15 jioni akiwa ameambatana na mkewe pamoja na mgombea mwenza huku akiwa amevaa kanzu na kofia.

Mashabiki wa chama hicho walionekana kumshangilia.

NYALANDU NA TUME YA UCHAGUZI

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu liitaka Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kutoa majibu ya rufaa zilizokatwa na wabunge 15 na madiwani zaidi ya 200 ili waweze kujua hatma yao.

“Mungu ametuletea zawadi nzuri hii ya Lissu yeye ni mpole na amebeba matumaini ya kila mmoja,”alisema.

KATIBU MKUU CHADEMA

Naye, Katibu Mkuu wa Chadema,John Mnyika aliomba kura za ndio kwa Chadema kuanzia ngazi ya udiwani ubunge na urais 

 Baada ya hapo ikawa ni zamu ya mgombea mwenza Salum Mwalim ambaye amewataka Watanzania kupiga kura kwa chama hicho ili kuweza kushika hatamu 

Mwalim alisema iwapo atachaguliwa na kuwa Makamu wa Rais, serikali yao itasimamia uhuru haki na maendeleo ya watu.

MKE WA LISSU ASIMULIA

Kwa upande wake, mke wa Lissu, Alice alisema mara ya mwisho aliondoka na Lissu mkoani Dodoma akiwa mahututi hivyo anashukuru amerudi akiwa anatembea.

“Niwashukuru sana kwa upendo wenu,huyu baba(Lissu) nimekutana naye Jeshini Mafinga na kisha Chuo Kikuu cha Dar es salaam Kitivo cha Sheria nilivutiwa nae japo nilikuwa nadengua dengua.

“Na nilivutiwa nae sababu ya ujasiri wake, kupenda kupigania haki, na katika kipindi chote hajawahi kubadilika,”alisema.

Alisema alipokuwa anataka kurudi nchini yeye aliingiwa na wasiwasi kama atakuwa salama lakini anamshukuru Mungu mambo yote yamekaa vizuri”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles