KAMPENI YA USAFI YAUNGWA MKONO KIMATAIFA

0
469

 

 

Na MWANDISHI WETU,

KAMPENI ya usafi wa mazingira ya ‘Nipo Tayari’ inayoratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imeungwa mkono na mashirika kumi ya kimataifa.

‘Nipo Tayari’ iliyozinduliwa mwezi uliopita mjini Dodoma, imelenga kuhamasisha wananchi umuhimu wa usafi wa mazingira, hasa ujenzi wa vyoo bora kuanzia ngazi ya familia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mratibu wa kampeni hiyo, Anyitike Mwakitalima, alisema ‘Nipo Tayari’ inahamasisha jamii kujua umuhimu wa kutunza mazingira ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.

Alisema ili jamii iweze kupata uhakika wa huduma bora ya maji safi na salama, inatakiwa kuzingatia umuhimu wa kutunza mazingira.

“Kwa kujitokeza wadau wetu wa maendeleo na kuunga mkono kampeni yetu, ni kitu cha kupongezwa sana na pia ni ishara kwamba malengo yetu ya kuwa na mazingira salama yatafanikwa,” alisema Mwakitalima.

Alisema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Maji na Umwagiliaji zimeungana kuendesha kampeni hiyo.

Mwakitalima alisema baada ya kuzinduliwa kwa kampeni hiyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Benki ya Dunia, Shirika la Misaada la Uingereza (DFID), Shirika la Miradi la Ujerumani (GIZ) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) yamejitokeza kuwaunga mkono.

Alisema kampeni hiyo ya usafi wa mazingira na matumizi bora ya choo inatarajiwa kuwa chachu ya upatikanaji wa maji safi na salama na kuboresha afya za Watanzania wote, mijini na vijijini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here